Tuesday, September 25, 2007

Vunju sasa limewekwa hadharani

na innocent munyuku

VUNJU husemwa na Waswahili kuwa ni vumbi linatokea kwenye maji baada ya kutibuliwa. Kwamba waweza ona maji yako safi lakini ukishayatibua vumbi hujitokeza na taka nyinginezo.

Ndicho kilichotokea wakati wa mechi za awali za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa wakongwe wa soka nchini Simba na Yanga baada ya kukubali kufungwa.

Walitinga dimbani wakijiona wasafi wa soka na wenye ubavu lakini kumbe ndani yake kungali vumbi kibao. Yanga ndiyo iliyoanza kupokea kipigo.

Lakini kwa mshangao Simba wakasahau kwamba mwenzako akinyolewa nawe tia maji.

Jumamosi iliyopita, mashabiki wa Yanga hakika walikuwa kwenye wakati mgumu baada ya timu yao kutekenywa kwa bao 1-0 na Ashanti United kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Vijiwe vikagauka kuwa vichungu kwani mahasimu wao walikuwa wakitamba kwa kejeli kwamba Jangwani kwisha habari yao. Wekundu wa Msimbazi, Simba ya Darisalama ikawa mstari wa mbele kukenua wakifurahia kichapo walichopata Yanga.

Hao waliotamba jana yake nao kesho yake wakapata kipigo kama cha masahiba kutoka kwa wagosi wa kaya, Coastal Union. Nani wa kumcheka mwenzake?

Hapa kwa Mzee wa Busati mambo ni murua kwa sababu kila jambo laenda sawia. Pengine Mwandika Busati aseme tu kwamba mwanzo wa ligi umewafumbua macho wengi.

Kwamba kitendo cha Yanga na Simba kuyeyuka kama konokono kwenye chumvi kimeleta neema na upeo kwamba majina makubwa kwenye soka si lolote bali ufanisi.

Hiyo imekuwa faraja kwa wengi na bila shaka mwanzo mzuri wa timu nyingine zinazoshiriki ligi hiyo. Kwamba sasa huenda wamejua kuwa soka si kwa Simba na Yanga tu hata wao wanaweza kuwa vinara dimbani.

Tuseme nini Jumanne hii ambayo wengi wanaishi kwa matumaini ya kujazwa sarafu mifukoni ili wazidi kujinafasi kwa sababu mifuko yao itawaruhusu kufanya hivyo.

Leo watakuwa baa ile na kesho watahamia kwingine na wapambe wao pembeni. Wanakula raha na kuponda mali kwa vile kufa kwaja! Mambo hayo wakwetu.

Hoja kuu ya Mzee wa Busati wiki hii ya neema ni kwamba kusiwe na hoja ya kujenga ukuta kwamba fulani anaweza na mwingine hajui. Kwa vile wote mpo katika kapu moja la ligi kila timu iwe na jukumu la kutoa burudani kwa mashabiki wake.

Soka si la Simba na Yanga tu. Kwa maana hiyo hata wageni wa ligi msimu huu nao wafanye mambo ya maana ili kubadilisha soka nchini.

Kwani hamkuwahi kuambiwa kwamba Simba na Yanga ni kaburi la wachezaji? Hamkuwahi kusikia kuwa wakongwe hao wa soka nchini hawana jipya zaidi ya sifa za historia?

Angalia ulimbukeni wao kwenye usajili kila msimu. Ni mgogoro kwa kwenda mbele. Wakati mwingine wanaingizwa mjini kama Simba wakati uleee walipoingizwa mjini na Ssentongo.

Limekuwa tatizo sugu hapa kwa wabongo kila msimu na kutokana na hali hiyo ndiyo maana baadhi ya timu kama Simba na Yanga zimejikuta zikiwa kama makaburi ya wachezaji.

Hii ni kwa vile usajili wao kwa kawaida hutawaliwa na mizengwe ya makomandoo na wanachama wanaojiita wakongwe.

Imekuwa ni fitna mtindo mmoja na kutokana na hilo si ajabu kwa Simba na Yanga kusajili wachezaji na kabla msimu haujakoma ukasikia maneno mengine kwamba mchezaji huyo kachuja.

Baada ya kipigo cha Morogoro na Tanga maneno yameshaanza na kwa hakika kinachosemwa ni kwamba usajili wao mwaka huu ni mbovu. Hawachelewi kulalama hawa. Wakiguswa kidogo tu lazima waruke.

Nani anabisha hili? Mifano yaweza kujaa vikapu hadi kutapika. Ni mambo yasiyofichika kwa sababu wenye macho wanaona na wenye masikio wanasikia vishindo vya uvundo huo.

Lakini nani basi atakuja na dawa ya masuala haya? Ni nani ataibuka na kutokomeza hali hii ya wachezaji kutumika kama makopo ya chooni? Je, ni malaika wa Kimakonde au wale kutoka juu mbinguni?

Usajili wa Simba na Yanga unategemea zaidi makapi ya wachezaji kutoka nchi jirani. Eti wenyewe wanawaita kuwa ni wachezaji wa kulipwa!

Kama kungelikuwa na vya soka ni nani leo hii angewababakia wachezaji makapi kutoka nchi jirani? Wachezaji ambao huko kwao si lolote. Kama wangelikuwa lulu wasingelithubutu kuja kwa Wabongo.

Kama kweli hao ni wa kulipwa mbona hawaendi Ulaya na nchi nyingine zilizo juu katika soka? Hao nao wanaganga njaa tu.

Lakini yote heri kwani sasa maji yameshatibuka na vunju laonekana. Kwamba utulivu uliokuwa umezoeleka ni batili kwani ndani ya maji yanayoitwa Simba na Yanga kuna vumbi kibao na hilo ndilo vunju linalosemwa na Mzee wa Busati.

Wasalaam,

No comments: