Na Innocent Munyuku
KWA umri wake, Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) ungetarajia kuona tija ya hali ya juu katika shirika hilo lililoanzishwa mwaka 1974. Lakini ÔwajanjaÕ wachache walitumia nafasi zao kujinufaisha.
Kwa hali hiyo, katika kipindi kirefu, shirika hilo kongwe limekuwa katika wakati mgumu huku vitendea kazi vikichakaa na kusababisha hasara kwa shirika hilo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na MTANZANIA Jumapili mapema wiki hii, Meneja wa UDA, Victor Milanzi, anaeleza mengi, lakini kubwa likiwa namna alivyofanikiwa kuziba nyufa zilizotumika ÔkutafunaÕ mapato.
ÒNilipoingia hapa Agosti mwaka jana kwa kweli nilikuta hali ikiwa mbaya sana,Ó anasema Milanzi na kisha kuongeza:
ÒKulikuwa na vitendea kazi vibovu, mabasi yalikuwa mabovu. Nilikuta mabasi mazima 13 kati ya 25 ya shirika.
ÒTukaweka mkakati wa kuyafufua kwa kununua vipuri na baada ya miezi tisa tayari tukawa na magari 19 barabarani.
ÒKabla ya hapo nilifanya maamuzi ya kuvunja makubaliano kati ya supplier wa magari yetu, Kampuni ya Quality Motors ambao walikuwa wanahusika pia katika kuyafanyia matengenezo.
ÒNilivunja uhusiano huo kwa sababu gharama zao zilikuwa juu mno. Kwa hiyo nilichofanya ni kuunda technical team hapa ya kukarabati magari.
ÒKwa hiyo kazi ikaanza na kweli ilishangaza wengi, kwani ilikuwa nzuri na wanaendelea na utaratibu huo.Ó
Hata hivyo, Milanzi anasema pamoja na kufanikiwa kuyafufua magari kwa gharama nafuu, bado kulikuwa na kikwazo katika mapato.
ÒKulikuwa na ufujaji mkubwa wa mapato kwa wakati huo. Nilikuta mapato kwa siku ni shilingi lakini nne. Nikaona hapana haiwezekeni hali ikawa hivi. Kwamba mabasi yote haya yalete fedha hiyo,Ó anasema Milanzi.
Je, alitumia mkakati gani?
Anasema baada ya kutoridhishwa na mapato hayo aliamua kufuatilia kwa karibu mwenendo wa kazi wa mabasi ya shirika.
ÒMapato mengi yalikuwa yakiingia mifukoni mwa watu na si katika shirika.
ÒTuliunda tume maalumu ya kuratibu mabasi barabarani na katika hilo tulifanikiwa, kwani mapato yanafikia hadi shilingi milioni moja kwa siku.
ÒTulichofanya ni kuwaajiri makondakta wanawake ambao kimsingi ni waaminifu na baadaye tukaanzisha utaratibu wa kutoa motisha kwa wafanyakazi. Motisha tunayotoa ni fedha taslimu na hakika imesaidia.
ÒLakini kwa muda mfupi niliokaa nilibaini kuwa wafanyakazi wengi walikosa lugha nzuri ya kibiashara au mawasiliano mema na wateja.
ÒKwa hiyo tukawapa mafunzo mafupi ya huduma kwa wateja kwa wiki mbili na wataalamu wa kozi walitoka Tanzania Bureau for Staff Empowerment.
ÒNa hali sasa ni nzuri kwani wafanyakazi wengi wamekuwa mahiri zaidi na kwa kuongezea ni kwamba mafunzo hayo yatakuwa yakitolewa baada ya miezi sita kulingana na mahitaji.Ó
Milanzi hasiti kueleza namna uendeshaji wa shirika hilo ulivyo mgumu. Anasema gharama za uendeshaji ni kubwa tofauti na mapato.
Anasema gharama ni kubwa mno na ili wajiendeshe kwa faida, yafaa nauli kwa mtu mmoja iwe Sh 950 badala ya Sh 250.
Hata hivyo, katika kukabiliana na hali hiyo, Milanzi anasema shirika lake limeandaa mpango maalumu wa kibiashara kwa miaka 10 ijayo.
ÒKuna mpango wa muda mrefu na mpango wa muda mfupi. Katika mpango wa muda mfupi tumenunua mabasi matatu mapya na matatu mengine yanakaribia kununuliwa.
ÒLakini katika mpango wa muda mrefu tumeomba msaada kutoka Uholanzi. Wamekubali kutusaidia mabasi makubwa 150 yenye uwezo wa kubeba abiria kati ya 120 hadi 130.
ÒKatika hilo tutapata msaada wa kiufundi kutoka kwao na vipuri pia na mradi huo utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 48.
ÒSerikali imeshatoa notification namba NLD/07/003 kuonyesha kuwa mradi huo umekubalika, kilichobaki ni utekelezaji.
ÒKama mambo yatakwenda kama yalivyopangwa, mabasi yataanza kuingia nchini kuanzia Novemba mwaka huu.
ÒHii itaondoa kero ya usafiri, hasa kwa wanafunzi katika jiji la Dar es Salaam.Ó
Anasema kuja kwa mabasi hayo kutabadili mfumo wa uendeshaji, kwani yataratibiwa kwa njia ya kisasa.
Kwamba badala ya kufukuzana na basi barabarani kudhibiti mapato, kitakachofanyika ni kufunga mitambo maalumu ya kujua basi liko wapi kwa wakati huo.
ÒKutakuwa na mtambo maalumu utakaotuonyesha mabasi yetu yote yakiwa barabarani. Sasa kama dereva atabadili njia tutamuuliza anakwenda wapi na kwa sababu zipi.
ÒHata ukatishwaji wa tiketi nao utakuwa makini. Kwa hiyo utaona kuwa mapato yatadhibitiwa.
ÒWenzetu Ghana wamekwenda mbali, wao wana kifaa maalumu mlangoni kinachohesabu idadi ya abiria walioingia.
ÒLakini kama nilivyosema awali kwamba wanawake ni waaminifu katika ukusanyaji fedha, kwa hiyo mkakati wetu ni kuwaajiri wanawake wengi zaidi pindi mradi huo utakapoanza.Ó
Shirika hilo lina makondakta sita wanawake kati ya 24.
Mbali na mpango huo, Milanzi anasema wameamua kukitumia kiwanja chao kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kitega uchumi.
ÒTunakusudia kujenga ghorofa 10, tutaingia ubia na baadhi ya kampuni ili kufanikisha jambo hilo. Lengo letu ni kutengeneza faida na vile vile kulipa kodi serikalini,Ó anasema Milanzi.
Anapozungumzia changamoto katika nafasi yake ya umeneja, anasema ni kuwabadili wafanyakazi katika utendaji kazi wa kila siku.
ÒSi kazi rahisi kuwabadili watu mtazamo, lakini najitahidi kuwaeleza kwamba lazima tufanye kazi kwa ushindani wa biashara, tuache mazoea.
ÒNa nawaahidi abiria kwamba kwa sasa wajiandae kwa huduma bora kutoka UDA, tunataka kuwa mfano bora katika usafirishaji wa abiria jijini Dar es Salaam.
ÒPengine nitoe maoni yangu kwa Serikali kwamba ijitahidi kuondoa kero ya usafiri jijini kwa sababu watu wengi wanataabika.
ÒHao wanaotaabika ndio wachapakazi wanaotakiwa kuijenga nchi. Kwa hiyo wanatakiwa kuwa na usafiri usio na kero.Ó
Milanzi ambaye mkataba wake na UDA unakoma mwaka 2011, alizaliwa Julai 29 mwaka 1954 Ndanda wilayani Masasi.
Alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Wailes, Temeke Dar es Salaam kati ya mwaka 1961 hadi mwaka 1967.
Mwaka 1969 hadi 1972 alikuwa Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Joseph kwa elimu ya sekondari kidato cha nne. Alihitimu kidato cha sita mwaka 1974 katika shule ya Aga Khan.
Mwaka mmoja baadaye alihudhuria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kambi ya Bulombora na mwaka uliofuata akapata kazi ya ukarani katika Shirika la Bima la Taifa.
Kazi hiyo aliifanya kwa mwaka mmoja na kisha kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kutunukiwa shahada ya kwanza ya uchumi mwaka 1981.
Mwaka 1982 aliajiriwa na Shirika la Utalii kwa nafasi ya Mchumi na mwaka 1986 alikwenda masomi nchini Uholanzi kwa mwaka mmoja.
Alirejea Shirika la Utalii lakini mwaka 1988 aliacha kazi na kuwa Meneja wa Benki ya Nyumba na mwaka 1992 alipanda hadi nafasi ya Mkurugenzi Mwendeshaji.
Mwaka huo huo alikwenda nchini Italia kuchukua shahada ya masuala ya kibenki kwa mwaka mmoja.
Amepata pia kufanya kazi Mtwara RETCO kati ya mwaka 1996 hadi 2005 akiwa Meneja Mkuu kabla ya kampuni hiyo kubinafsishwa.
Milanzi, mwenye mke na watoto wanne, lengo lake baada ya kuondoka UDA ni kufanya kazi katika mashirika ya kimataifa.
Monday, September 3, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment