na innocent munyuku
MZEE wa Busati juma hili anakuja akiwa chini na hasiti kupiga goti kwa wadau wake kwa vile wiki iliyopita hakutia mguu mahala hapa.
Hakuna namna ya kujitetea labda aweke wazi kuwa majukumu yalizidi kipimo na kwa wengine husikika wakisema ati sababu za kiufundi ambazo hazikuweza kuzuilika. Sasa hakuna matata Mwenye Busati yu kazini.
Jumanne hii kaja na hoja kwa rafiki zake wanaojiita wanamuziki wa kizazi kipya. Wakati ule wasanii hao wakichipukia Mzee wa Busati alikunwa na hilo jina-‘wanamuziki wa kizazi kipya’. Kwamba hawa wanakuja na mapinduzi katika sekta ya muziki.
Mzee wa Busati aliamini kuwa sasa dunia itashuhudia mageuzi chanya katika muziki na hivyo kuwaongezea uhondo mashabiki wake. Hali haijawa hivyo!
Badala yake ushuhuda pekee kwa sasa ni kwamba walio wengi wamebaki kuwa malimbukeni. Hawana jipya kama ilivyodhaniwa.
Iweje leo hii wasanii wapange foleni kwa watayarishaji wao wa muziki na kisha kwenda studio wakiwa na nyimbo lukuki za mapenzi pekee? Huku ni kupotoka.
Hivi kweli jamii ya Kitanzania haina kitu kingine cha kusikiliza zaidi ya mapenzi kati ya binti na mvulana? Huku ni kupotoka na kwa hali ilivyo, Mzee wa Busati hawezi kukaa kimya atapayuka tu.
Mwenye Busati wakati fulani alipata kusema kuwa kuna hatari kwamba wanamuziki wetu hawa tunawaoita wa kizazi kipya wakafika mahala wakaishia shimoni. Naam wataishia shimo baya kwa sababu wengi hao mipango yao haieleweki.
Kati ya mambo aliyoyasema Mwandika Busati wakati huo ni kwamba wanamuziki hao hawajui faida ya hakimiliki na ndio maana wanadiriki kuiba kazi za wanamuziki wa nje.
Si mara moja au mbili, wengi wao wameshaiba midundo ya muziki kutoka ughaibuni na hata tungo na wao kazi yao ikabaki kutafsiri kwa lugha ya Kibongo. Mwisho wa siku ati wanaitwa masupa staa! (?).
Tuachane na hilo tuendelee na hoja kuu ya leo kwamba hivi kweli kuna ulazima wowote kwa wanamuziki hao kung’ang’ania nyimbo za mapenzi pekee?
Nani asiyeyajua mapenzi katika dunia hii? Nani hajui uchungu na uhondo wa mapenzi? Semeni ni nani huyo ambaye mwataka aendelee kujifundwa. Kuna mambo mengi taifa hili linahitaji kupewa changamoto ili watu wake waishi kwenye neema.
Wangapi wameshika maikrofoni zao na kukemea uozo wa ubinafsishaji na utata wa baadhi ya mikataba ya ubinafsishaji huo? Nani kaimba juu ya hatari ya utandawazi ambao pasipo umakini tutamezwa kama dagaa majini? Kama wapo hawajai kiganjani!
Leo hii mmekaa na kuanza kujisifu habari ya mavazi, uzuri wa sura na mitindo ya nywele. Hamuwaoni wanasiasa mafisadi ambao kwao kura ya kuendelea kuwa bungeni ndicho anachojali kuliko masilahi ya nchi.
Macho yenu hayaoni meza za wanasiasa hao na vidole vyenu havithubutu kuwagusa wala kuwatupia mawe ya sanaa ili wapate kujirekebisha.
Wanaingia bungeni baada ya lugha tamu wakati wa kampeni za uchaguzi. Wakisema wataleta hiki na hiki badala yake wanaigeukia jamii yao kwa namna ya kutisha kwa kukubali bajeti yenye kila aina ya maumivu. Msanii gani kaliona hilo?
Pengine hamjui nguvu ya sanaa katika jamii na ndio maana mwaendelea kugusa vitu rahisi rahisi tu kama majigambo ya mavazi na vidani vya dhahabu.
Wanamuziki mmeridhika na namna kina mama wanavyopata taabu hospitalini kwa kukosa huduma muhimu hasa wakati wa uzazi. Wagonjwa wengine wanaoteseka na kufariki dunia kwa kukosa dawa nao hamuwaoni na wala hamna huruma nao. Mngekuwa na huruma juu yao mngewatetea kupitia sauti zenu.
Nani anataka kujua habari ya binti mwenye kiuno namba nane au miguu ya bia? Pengine mwawaiga wanamuziki wa Marekani. Basi kama ndivyo mnazidi kupotoka kwa sababu hao enzi zao hawakuanza muziki kwa kujisifu.
Wanamuziki hao walikemea ufisadi na kupambana na wadhalimu katika nchi yao na leo hii mambo yao yako mstari mnyoofu wanakula kivulini.
Hawakuanza na majigambo hawa na wala kupigana vijembe. Waliungana kuitetea nchi yao na ndio maana leo hii wamefikia hapo walipo.
Amkeni sasa, habari ya kuimbiana mapenzi kila leo haikubaliki. Chambueni masuala nyeti ya kijamii, mambo ambayo yanajenga nchi na ustawi wa watu wake.
Kuendelea kuimba nyimbo nyingi za mapenzi ni kukosa fikra pevu. Huo ni ubutu wa akili. Amkeni wajameni wakati wa mabadiliko ni huu.
Vinginevyo Mwandika Busati anaelekea kufikia ukingoni. Apate nafasi naye ya kufanya tafakuri kwa mambo mengine yajayo.
Manake mwaka waishia ukingoni na ahadi alizojiwekea ni kama ngumu kumalizika kwa mwaka huu wa 2007. Kwa maana hiyo lazima Mzee wa Busati akandamize kwa ‘high speed’.
Wasalaam,
Monday, September 3, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment