Monday, September 3, 2007

Dk. Kibatala: Taaluma ya udaktari haihitaji majungu

Na Innocent Munyuku

SIKUWAZA kama safari yangu ya dharura ya kifamilia mkoani Morogoro hivi karibuni ingenikutanisha na mmoja wa madaktari bingwa katika upasuaji nchini.

Huyo ni Dk. Pascience Kibatala ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali Teule ya Mtakatifu Francisco ya Ifakara mkoani Morogoro. Wadhifa huo ameushikilia tangu mwaka 1994 akiwa Mweusi wa kwanza kukamata nafasi hiyo hospitalini hapo.

Pamoja na nafasi hiyo, Dk. Kibatala ambaye ni mwenyeji wa Ifakara ni Makamu wa Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Madaktari Wapasuaji Vijijini.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na MTANZANIA Jumapili, Dk. Kibatala anasema pamoja na umahiri wa hospitali yake katika utoaji wa huduma za afya, bado kuna vikwazo au visa kutoka kwa wananchi wasioitakia mema hospitali hiyo.

Chuki hizo ni zipi?

Anasema katika siku za hivi karibuni anaamini kumejengwa mtandao wa kulichafua jina zuri na huduma za hospitali hiyo teule iliyoanzishwa mwaka 1927.

“Siku chache zilizopita kumekuwa na taarifa potofu ndani ya jamii kuhusiana na hospitali hii. Baadhi ya vyombo vya habari kwa makusudi kabisa wamekuwa wakichapisha taarifa zisizo sahihi.

Anatoa mfano kwamba Mei 18 mwaka huu akiwa chumba cha upasuaji alitaarifiwa kuwa kuna maiti anatakiwa kufanyiwa uchunguzi.

“Kwa kawaida ninapokuwa na majukumu mengine, huwa nawaagiza madaktari wengine wazoefu kufanya kazi hiyo. Hivyo nikawateua Dk. Eric Ngaula na John Mkony waende badala yangu.

“Nikajua wazi kuwa shughuli itakwenda kama ilivyo kawaida kwa mujibu wa taratibu zetu na ndivyo ilivyokuwa. Lakini cha kushangaza, Jumapili ya Mei 20 wakaja ndugu wa marehemu wakidai wapewe mwili wa marehemu wakisema kuwa ndugu yao aliuawa na polisi.

“Sikuelewa kwanini kuna madai hayo, nikampigia simu Dk. Ngaula akaja na nikaomba feedback akasema siku ya uchunguzi kulikuwa na mashuhuda wanane. Polisi wanne na ndugu wanne.

“Ndugu walidhani alipigwa risasi katika harakati za kuwaondoa wafugaji eneo la Utengule,” anasema.

Anaongeza kuwa maiti Shigela Sahani aliletwa hospitalini hapo usiku wa kuamkia Mei 15 lakini ndugu wakarudi kuomba uchunguzi Mei 18.

Anasema waliamua kushirikiana nao na walivalishwa gloves ili kusiwe na shaka kwa jambo lolote. Ikabainika kulikuwa na majeraha mawili kichwani na mguuni lakini hayakuwa ya risasi.

“Wakampasua mwili, ndani ya tumbo hapakuwa na damu, wakafungua kifua hawakuona mvujo wa damu na hata ubongo haukuwa na damu,” anasema Dk. Kibatala na kisha kuongeza:

“Sasa habari kwamba huyu marehemu aliuawa baada ya kunyongwa zinanishangaza kwani katika uchunguzi wetu hakuna mfupa ulioonekana kuvunjika.”

Dk. Kibatala anasema alianza kupata shaka kutoka kwa ndugu pale walipolazimisha kuwa mwili upigwe picha za x-ray wakati ulishaanza kuoza.

“Nikawaambia maiti ameoza na kwamba kitendo cha kuuchukua mwili hadi chumba cha x-ray ni cha hatari kwa afya za watu wengine kwani kungekuwa na uwezekano wa kuleta magonjwa mengine.

“Ndugu wakaomba mwili uhamishiwe Morogoro, polisi wakapiga simu na wakajibiwa kuwa haiwezekani. Kilichofuata polisi wakaukabidhi mwili kwa ndugu.”

Anasema baada ya siku chache akashangaa kusoma katika gazeti kwamba maiti alibainika kuvunjika mfupa baada ya kufanyiwa uchunguzi Hospitali ya Muhimbili.

“Naamini kwamba kilichofanywa na hospitali yetu hadi hatua ya mwisho ni cha usahihi kwani hakuna mahala ilibainika kavunjika. Kuvunjika kwa mfupa kunaweza kutokea kutokana na njia ya usafirishaji wa maiti kutoka Ifakara hadi Dar es Salaam.

“Kama alinyongwa mbona alifikishwa hospitali ya Mlimba akiwa hai?

“Sasa ndio maana nasema kuwa hapa kuna majungu yanapikwa nami sitakubali kudhalilishwa taaluma yangu au sehemu yangu ya kazi.

“Jamii ielewe kuwa hospitali hii haijaanza kufanya uchunguzi juzi. Hii si mara ya kwanza kufanya uchunguzi ila ni mara ya kwanza kupata utata huu.”

Chimbuko la Hospitali ya Mtakatifu Francisco

Ilianza mwaka 1927 kama zahanati chini ya Masista wa Baldegg. Wakati huo haikuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa.

Miaka mitatu baadaye zahanati ikawa na uwezo wa kulaza wagonjwa 30 na daktari wa kwanza alifika katika zahanati hiyo mwaka 1951.

Mwaka 1960 ikawa hospitali rasmi. Uongozi wa awali ulikuwa chini ya wauguzi wa Baldegg na kisha askofu. Hata hivyo, kwa sasa uongozi uko chini ya ushirikiano wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Dayosisi ya Kanisa Katoliki.

Hospitali ina uwezo wa kulaza wagonjwa 371 ikiwahudumiwa wagonjwa 600,000 na ina vitengo vyote muhimu.

Ina chuo cha wauguzi na madaktari wasaidizi. Lakini pia ni moja ya vituo vikuu vya utafiti kwa magonjwa mbalimbali.

“Wanafunzi hapa wanapata elimu kwa viwango vya kimataifa, mara kwa mara wanakuja wataalamu kutoka Italia, Uswisi na Ujerumani.”

Hata hivyo, anapoelezea matatizo ya hospitali hiyo, Dk. Kibatala anasema kuna upungufu wa wauguzi, madaktari, wataalamu wa miozi na wafamasia.

Dk. Kibatala alitokea wapi?

Alizaliwa Februari 16 mwaka 1952 Ifakara mkoani Morogoro. Alipata shahada ya kwanza ya mwaka 1979 Chuo Kikuu Dar es Salaam na mwaka 1989 akapata shahada ya pili chuoni hapo.

Mwaka 1994 alipata shahada ya pili ya
utawala na uongozi wa hospitali katika Chuo
Kikuu cha Leeds, Uingereza

Amewahi kusomea upasuaji katika Chuo Kikuu cha Tel Aviv, Israel mwaka 1999. Amewahi kupata kozi za upasuaji na uongozi katika vyuo mbalimbali duniani.

Alianza kuitumikia taaluma ya udaktari kuanzia mwaka 1979 akiwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mufindi hadi mwaka 1985.

Tangu wakati huo pia amekuwa akiendelea na ufundishaji wa elimu ya utabibu. Amepata kuwa Mganga Mkuu wa Upasuaji Mkoa wa Kigoma kati ya mwaka 1989 na 1992 na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa.

Mwaka 1994 akateuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali Teule ya Ifakara.

Kati ya mwaka 1996 na 2005 alikuwa mhadhiri mwalikwa wa Chuo Kikuu cha Insbruck cha Austria. Mwaka 2000 alipata uteuzi wa Rais kuwa mganga mkuu wa upasuaji.

Mwaka huu ameteuliwa kuwa mshauri wa
Shirika la Afya Duniani (WHO) na Mratibu wa Mkutano Mkuu wa Mkutano wa Kimataifa wa Madaktari wa Upasuaji utakaofanyika Septemba mwaka huu mjini Ifakara.

Amehudhuria mikutano mbalimbali ya kimataifa na kutoa mada za afya katika taaluma ya udaktari.

No comments: