Monday, September 3, 2007

Panya wa SUA sasa watafiti magonjwa ya binadamu

Na Innocent Munyuku
Wiki hii MTANZANIA Jumapili ilifanya mahojiano maalumu na Mratibu wa Kituo cha Utafiti na Udhibiti wa Viumbe Waharibifu katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Profesa Robert MachangÕu, anayeelezea kwa undani utafiti wa panya unaoendelea kufanyika chuoni hapo na mwelekeo wake.

KWA miaka mingi jamii mbalimbali zimekuwa zikiwatumia panya kama kitoweo maarufu katika maisha ya kila siku. Sasa panya si kitoweo safi tu, bali wanatumika pia katika ulimwengu wa utafiti wa sayansi.
Katika miaka ya 1980, kulianzishwa mpango maalumu wa udhibiti wa panya waharibifu, hasa baada ya wakulima wa mazao mbalimbali kuathirika.
ÒKikaanzishwa kituo cha udhibiti kwa sababu kwa wakati huo si wakulima tu walioathirika, bali pia wafanyabiashara,Ó anasema Profesa Robert MachangÕu na kuongeza kuwa baadaye likaja wazo la kufanya utafiti juu ya panya hao.
ÒSerikali ikasaka msaada kutoka DANIDA (Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Denmark) kwa ajili ya kutengeneza kituo cha utafiti hapa SUA. Wakati huo, chuo chetu kikiwa kama kitivo cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
ÒBaadaye katika miaka ya 1980 wakaja watafiti kutoka Ubelgiji, hawa walikuja si kwa ajili ya udhibiti, bali kufanya utafiti wa kina.
ÒWalitaka kujua hawa panya wanazaaje, aina zao, adui zao na tabia zao ni zipi. Kulikuwa na mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Ubelgiji juu ya hilo.
ÒWalipofika katika kituo cha udhibiti wakawakuta DANIDA, sasa ikawa ngumu kidogo kwao kuchanganyika kwa sababu malengo yalikuwa tofauti. Kwamba kuna wadhibiti na watafiti.
ÒKwa hiyo wakaja hapa SUA tukaulizana tufanyeje. Tukaona ni heri kuwa na kituo ambacho kingeshughulikia utafiti wa panya,Ó anasema na kisha kuongeza:
ÒMwaka 1984 nikawa miongoni mwa watafiti waliokuwa wanaangalia kiini cha ugonjwa uliokuwa umewakumba wakulima, hasa katika mashamba ya mpunga na miwa.
ÒTukabaini kuwa magonjwa hayo yalitokana na mkojo wa panya. Ni katika kipindi hicho tukabaini kuwa kuna aina 34 za panya kote nchini.
ÒMwishoni mwa mwaka 1984 ikaonekana kwamba kuna ulazima wa hawa panya kuwatumia vinginevyo, na hii ilitokana na ukweli kwamba panya hutumia pua kunusa katika kusaka chakula au kumtambua jike au dume.
ÒMbelgiji mmoja akatoa wazo kuwa hawa panya pengine wangeweza kunusa milipuko itokanayo na baruti inayotumika kutengenezea mabomu au risasi.Ó
Profesa MachangÕu anasema baada ya utafiti kati ya aina 34 za panya, ikabainika kuwa panya buku angefaa katika mradi huo.
Kwa nini panya buku?
ÒPanya buku ni mtulivu kuliko aina nyingine ya panya. Lakini pia haoni vizuri kama panya wengine kwa hiyo hutegemea kunusa zaidi na ni rahisi kumfuga ndani.
ÒLakini utulivu huo ni wakati akiwa katika mazingira yake ya asili, vinginevyo huwa si watulivu, ni wakorofi.Ó
Anasema walianza kuwanasa panya hao katika Milima ya Uluguru na kisha kuwasafirisha hadi Ubelgiji.
ÒMwanzo ulikuwa mgumu, kwani walikuwa wanapigana wao kwa wao na kwa hakika awali walikufa wengi. Ilichukua kama mwaka mmoja hivi kuanzia mwaka 1998 hadi walipoanza kuzoeana.
ÒLakini nikawaambia wenzangu wa kule Ubelgiji ni bora turudi nyumbani Tanzania katika mazingira yao ya asili. Ndipo mradi ukaanza rasmi hapa mwaka 2000,Ó anasema Profesa MachangÕu.
Kwa bahati jirani na SUA kuna kambi ya kijeshi ya Mzinga ambako wazo hilo la utafiti lilikubalika baada ya kuwasiliana na Wizara ya Ulinzi.
ÒMkuu wa kambi wakati huo akatoa baruti kidogo kwa ajili ya utafiti.
ÒTraining (mafunzo) katika siku za awali yalikuwa magumu, kweli ilikuwa kazi ngumu. Tulichofanya ni kuwatengenezea panya mashimo madogo.
ÒKwa hiyo tukawa tunatofautisha kwamba shimo moja linakuwa na baruti na jingine bila baruti. Sasa walikuwa wakipita shimo wananusa mmoja mmoja.
ÒAkifika kwenye shimo lenye baruti anatumia muda kidogo pale nasi tunampigia alama fulani na kumrushia ndizi. Kwa hiyo ikawa anaona kuwa akinusa harufu fulani kuna zawadi ya ndiziÉbaada ya miezi miwili wakaanza kuelewa vema kabisa,Ó anasema Profesa MachangÕu na kuongeza kuwa hadi sasa kuna panya 250.
Baada ya kufanikiwa kuwafundisha kunusa baruti, Profesa MachangÕu anasema likaja wazo jipya na safari hii panya hao watumike kunusa makohozi ili kubaini kama yana wadudu wa kifua kikuu.
ÒTukaanza kuwanusisha bakteria wa TB na wakafuzu na sasa tunaendelea kuwafundisha kunusa makohozi.Ó
Profesa MachangÕu anasema mradi huo ulioanza miaka miwili iliyopita unaonyesha mafanikio na wamekuwa wakishirikiana na Wizara ya Afya kitengo cha magonjwa ya kifua kikuu.
Cha kufurahisha ni kwamba panya wamekuwa wakifanya vema katika unusaji na kubaini wadudu wa kifua kikuu kwa haraka zaidi kuliko darubini.
ÒKinachofanyika ni kwamba tunagawana makohozi, hospitalini wanapima kwa darubini nasi tunawatumia panya. Tunapokuja kulinganisha mara nyingi panya anakuwa amepata alama za juu kuliko vipimo vilivyofanywa na binadamu kwa kutumia darubini.
ÒLakini si hilo tu, panya kwa saa moja ana uwezo wa kupima sampuli 150, wakati binadamu akijitahidi sana atafanya vipimo vinne tu,Ó anasema Profesa MachangÕu.
Anaongeza: ÒKwa vile panya wanafanya mchanganuo wa haraka, nadhani ni vema tukaipitisha teknolojia hii na Serikali ituchangie.
ÒTunaweza kutengeneza kliniki yetu tukazunguka sehemu kubwa ya Tanzania kama vile katika kambi, shule na vijiji.Ó
Profesa MachangÕu anasisitiza kuwa kuna umuhimu wa kuuimarisha mradi huo kwa sababu hata kama wafadhili wataondoka bado unabaki nchini kwa faida ya taifa.
Ni wazi kuwa katika mpango huo upo uwezekano wa kukabiliana na magonjwa kama hayo ambayo mara nyingi huwa ngumu kuyadhibiti kutokana na mlolongo wa upimaji.
Kwamba kwa kuwatumia panya hao kutambua wadudu wa ugonjwa wa kifua kikuu itakuwa rahisi kwa madaktari kuwaanzishia tiba waathirika wa ugonjwa huo ambao mara nyingi huambatana na ukimwi.
Lakini Profesa MachangÕu anaeleza kuwa utafiti huo ukipewa nguvu na mkazo zaidi, taifa litanufaika kwa kiasi kikubwa na kwamba si ajabu panya hao wakatumika katika masuala mengine ya kubaini vijidudu vya magonjwa mengine.
Mbali na kufanikiwa kubaini kuwa panya buku wana uwezo wa kunusa baruti na makohozi ya TB, kwa sasa wanaendelea na utafiti mwingine katika kubaini mabomu yaliyotegwa ardhini.
ÒMafunzo haya yanaendelea na kuna panya wengine wamepelekwa Msumbiji kwa ajili hiyo.
ÒKama tutafanikiwa kwa hili ni wazi kuwa gharama zitapungua, kwani wale commercial de-miners (wategua mabomu wa kulipwa) wana gharama kubwa sana na mabomu ni mengi.
ÒUzuri wa panya ni kwamba wanaweza kuwa juu ya bomu la kutegwa ardhini na lisifyatuke kwa sababu uzito wao ni mdogo tofauti na mbwa au binadamu.Ó
Hata hivyo, anasema katika jitihada zao hizo mara kadhaa wamekuwa wakishutumiwa na wanaharakati wa haki za wanyama kwamba wanawatesa panya buku.
Anasema pamoja na shutuma hizo, wanajaribu kuwapa ufafanuzi kwamba kazi ya panya hao si kutegua mabomu, bali kunusa na kuonyesha mahala yalipo.

No comments: