Monday, September 3, 2007

Msimu wa mapromota na mapromosha

Na Innocent Munyuku

SIKU zinapita, pilika zinazidi na kwa walio wengi wanaendelea kukaza buti ili kutimiza dhamira kuu kwa mwaka 2007.

Imekuwa desturi karibu kila mwaka kwa wana wa Adam kujiwekea malengo kwamba mwaka mpya nitatenda haya. Wapo waliodhamiria kuacha ulevi na wakafanikiwa hali kadhalika wazinzi na mafisadi. Lakini si kila anayedhamiria hufanikiwa kutimiza ahadi hiyo.

Mzee wa Busati kama ilivyo ada yu katika nafasi yake ya kujidai akileta porojo zisizokinai na wala si mtenda jinai. Ametua hapa leo kwa ajili ya kuteta na waungwana wake.

Juma hili Mwenye Busati kaamua kuteta juu ya haya mashindano ya kuwasaka walimbwende ambayo kasikia yako katika hatua za awali.

Vigoli wanapishana na kupanga foleni kwa washauri wakitaka waelekezwe namna ya kupata kura nyingi zitakazowapa jina jipya kama vile ‘Miss Kitangali’, ‘Miss Mwanamkude’, ‘Miss Kishimundu’ na majina mengine yafananayo na hayo.

Ni muda mgumu kwa mabinti hawa wabichi ingawa nyakati nyingine Mwenye Busati kishasikia eti kuna washiriki waliowaacha watoto nyumbani. Hawa kwa maneno mengine wanavunja sharti au miiko ya mashindano haya tunayoiga kwa wazungu.

Kama binti anatamani kuitwa ‘Miss Kauzeni’ basi sharti mojawapo awe mbichi, ambaye hajajua uchungu wa kuzaa. Eeh usishangae mwanakwetu ndio mambo yenyewe yalivyo.

Lakini waandaaji wa shughuli hii ya kuwasaka warembo bora wamebadilika na wameboresha mashindano hayo kwa kiwango gani?

Je, baadhi yao wataendelea kuwa wahuni wenye tamaa ya fedha pasipo kujali maslahi ya wengine? Au wataendelea kuziba masikio ili wajaze matumbo yao kila uchao?

Si jambo la ajabu kusikia mwandaaji kaingia mitini na zawadi za washindi. Si jambo geni kuambiwa kuwa katika shindano burudani itatolewa na Bambo na asionekane. Haya yamekuwa ya kawaida na watu wakishapiga kelele humezea na bia basi koo likawa shwari.

Mzee wa Busati kishaambiwa pia kwamba wapo waandaaji mhhh hapana hawa hupenda kuitwa mapromota kwamba baadhi yao wana tabia ya kuwaomba tendo la ndoa washiriki.

Kasikia pia kuwa hata kwa majaji wakware msimu huu huwa neema kwao. Wanachagua vigoli wabichi na kuwadhulumu miili yao. Hiyo ndiyo hulka yao kwani hujui ile methali isemayo mkware hajiingilii mwenyewe?

Kwa tamaa ya ushindi binti hukubali kudhalilishwa ili apate runinga au motokaa yake atambe nayo bila fadhaa na wenyewe mitaani husikia wakisema mambo waawaaa!

Tumefikia hapa wajameni? Hivi kweli na huko yalikoanzia mashindano mambo haya hutokea? Kwanini twapenda kupandikiza maovu yanayoepukika? Huu ni uendawazimu.

Wakati Mzee wa Busati anaanza porojo zake hapo juu alinena kwamba kwa binadamu wengi malengo ya mwaka ni jambo la lazima. Naam! Hata Mwandika Busati alishaweka mkakati kwa mwaka 2007.

Mkakati wake haukuwa wa kuhubiri Injili, wala kuacha kalamu na kuingia mwituni. La hasha! Alilenga kuwashikia bango hawa wanaojiita mapromota kumbe ni mapromosha.

Msimu kama huu unakera na kuufanya mtima ugande baridi. Hawa watu wanachefua kwa ulaghai wao. Hawana huruma wala roho njema ya ujenzi wa taifa.

Wakiachiwa waendelee kuwaharibu hawa warembo wategemea nini katika kipindi cha miaka 10 ijayo?

Mzee wa Busati anasema kwa uchungu kwani naye ana kibinti chake ambacho baadaye kinaweza kupata wazo la kuwania taji la Miss Tanzania. Sasa akiacha haya mambo ya aibu yaendelee si itakuwa balaa? Naapa tutaonana wabaya.

Si jambo la kucheka tuungane na kuwamaliza hawa wahuni wasiojali utu. Wanachekelea wanapoona hundi zimeenea tarakimu nene kutoka kwa wafadhili wao. Wanakenua kwa vile wana uhakika wa kuendeleza ubazazi.

Mzee wa Busati kwa Jumatatu hii anafikia ukomo. Awapishe warembo waendelee kujikwatua na kuzifanyia mazoezi ndimi zao ziseme ‘NO’.

Mnaojibana kula ili mpate miili ya ki-miss heri yenu lakini angalieni msije anguka kwenye msongamano wa kuwania daladala za Mbagala, Kimara au Mwenge. Hakika mtaanguka kwa vile miili yenu imekosa lishe bora.

Wasalaam,

No comments: