Na Innocent Munyuku
KAMA kuna mambo yanayowasumbua wasanii wa muziki katika sehemu mbalimbali duniani basi ni hatua ya kukubalika kuingia studio kurekedi.
Kikwazo hicho mara nyingi huwakumba wasanii wachanga ambao hawakuwahi kusikika kabla.
Lakini pia kuna tatizo jingine kwa wasanii hao. Nalo ni kukosa uwezo wa kulipa kwa ajili ya kurekodi nyimbo zao. Hapo huwa shughuli nzito kwa maelfu ya wasanii.
Nchini Tanzania mambo magumu kama hayo yameendelea kuwakumba wanamuziki kila kukicha. Wanaweza kupata wasimamizi lakini walio wengi wanakuwa hawana lengo la kutoa msaada.
Wanachofanya wasimamizi hao ambao wakati mwingine huitwa mameneja ni kulinda vipaji vya wasanii ili baadaye waviwinde.
Kwamba wanachofanya mameneja hao ni kuvipalilia vipaji vya wasanii kwa hila ili wanufaike wao huku wakiwaacha wahusika wakitaabika.
Baada ya kubaini tatizo ndipo vijana watatu wakaamua kuungana na kuikarabati studio ijulikanayo kama Active Studio.
Katika mahojiano maalumu na Mtanzania hivi karibuni, Msemaji wa Active Studio, Gota Warioba anasema waliamua kuwa na studio kwa lengo la kuwasaidia wasanii.
Anasema katika sera zao, wanaamini kuwa kama wanamuziki wachanga hawatasaidiwa ni wazi kuwa hawatafika mbali.
“Hapa kwetu hakuna umwinyi, wakija tunawakaribisha na kuwaelekeza nini cha kufanya.
“Hapa ni sawa na nyumbani kwao, wakija tunawakaribisha na kuwaelekeza nini cha kufanya tunawajenga wasanii tunaumia kuona wakipoteza muda kwa kutoelekezwa,” anasema Gota.
Anasema wapo wamiliki wa studio ambao hawako wazi katika utaratibu wao mbele ya wasanii. Kwamba badala ya kumweleza msanii wanabaki kuwazungusha.
“Kama haiwezekani unamweleza. Lakini pia si uungwana kulipua kazi za wanamuziki. Ni heri warekodi nyimbo zenye ubora wa kimataifa.”
Studio hiyo iliyopo karibu na Kanisa Katoliki la Manzese jijini Dar es Salaam ina vifaa vya kisasa na hivi karibuni wameongeza software maalumu za kuchanganyia muziki.
Baada ya kurekodi nyimbo, wasimamizi wa rekodi hizo huzipeleka sehemu nyingine kujaribia ubora wake kabla ya kupeleka sokoni.
“Kwa kawaida tukisharekodi hapa tunakuwa hatujajiridhisha kwa hiyo tunapeleka wimbo kusikiliza sehemu tofauti kama nne hivi.
“Unajua spika za hapa studio zinaweza kukupa mwelekeo mzuri lakini kumbe kazi bado. Kwa hiyo tunasikiliza katika kumbi za disko na ndio maana muziki uliotoka hapa Active hauwezi kuwa mbovu,” anaeleza Gota.
Studio hiyo ni sawa na nyumba ya sanaa au shule kwa wasanii mbalimbali wanaopenda kuimba.
Baadhi ya wasanii waliopikwa na studio hiyo ni Vitali Maembe maarufu kama Sumu ya Teja. Mwanamuziki huyo ameshafyatua vibao kadhaa kwa kutumia studio hiyo.
Mwingine ni Carola Kinasha ambaye kama ilivyo kwa Maembe ni mmoja wa wanamuziki wanaovuma kwa nyimbo zao zenye midundo ya asili.
Kuna baadhi ya wasanii wa kizazi kipya waliofaidika na studio hiyo. Hao ni Mackdizo na KD Mapacha.
Uzuri wa Active Studio ni kwamba waratibu wote ni washauri kuhusiana na mambo ya kitaalamu katika fani ya muziki.
“Hapa tunawajenga wasanii na midundo yote inatengenezwa hapa kwa ufundi wa hali ya juu. Hakuna anayeiba midundo kutoka katika intaneti,” anasema Gota.
Katika hatua za awali hakuna msanii anayetozwa fedha kwa ajili ya ushauri. Huduma zote ni bure lengo likiwa ni kuwajenga.
Tayari wameshaanzisha programu ya kuunganisha vipaji vya reggae kabla ya kutoa albamu za pamoja. “Kuna wasanii wengi wanaendelea kuweka mashairi katika muziki,” anasema Gota na kuongeza kuwa idadi yao ni zaidi ya 22.
Hata hivyo, Gota ana ushauri kwa wasanii nchini. Wawe na ari na kutokata tamaa. “Wawe na dhamira ya dhati katika sekta hii, kwani muziki ni biashara.”
Monday, September 3, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment