na innocent munyuku
INATIA uchungu! Ni mengi yanayotia uchungu lakini hili la Taifa Stars kunyukwa na Msumbiji linaumiza zaidi.
Kwamba furaha yote ya kuiona Stars ikitinga Fainali za Kombe la Mataifa Afrika mwakani huko Ghana imetumbukia nyongo. Tanzania imegota labda tuwaze bahati ya Kombe la Dunia.
Lakini mbali na kufungwa na Msumbiji Jumamosi iliyopita, Mwandika Busati ana uchungu mwingine uliotokana na kero za mashabiki wa soka nchini.
Hao wameshaanza kumsema vibaya Kocha Mkuu wa Stars, Marcio Maximo eti hajui kazi yake. Hakika hili nalo linatia uchungu.
Mzee wa Busati amepata na butwaa asijue aanzie wapi. Kinachoshangaza ni kwamba hao wanaopiga kelele ndio hao hao waliokuwa wakimshangilia Maximo baada ya kuilaza Burkina Faso na pia Uganda.
Ni hao hao waliokuwa wakiimba sifa hata wakiwa ndotoni kwamba Maximo ni kiboko yao. Leo hii wamegeuka, wanamwona kocha huyo kutoka Brazil kuwa ni mwenye mikosi. Hili linashangaza!
Hao wanaobwata kama wendawazimu bila shaka hawajui wanenalo na wamesahau historia ya soka nchini Tanzania. Wao wanaishi leo, ya jana na yajayo hawayatambui.
Mzee wa Busati si msemaji wa Maximo lakini kwa leo anaomba ajaribu kuteta kwa uwazi kwamba Mbrazili huyo anatwishwa lawama asizostahili. Anaonewa na yafaa aachwe.
Huu si muda wa kumlaumu Maximo hata kidogo. Kusema kwamba uwezo wake umekoma huku ni kukosa adabu. Hiyo ni sawa na kumchungulia mkwe maliwatoni.
Maximo alipotua nchini aliweka kila jambo kwa uwazi hasa alipoelezea majukumu yake katika timu ya taifa. Kila alipopata mwanya hakusita kusema kwamba kilichomleta nchini ni kusuka vipaji upya na kwa mwendo wa kuridhisha.
Hilo kalifanya na bila shaka anaendelea nalo. Maximo hakuja nchini kutupeleka Ghana. Hilo hakulisema, alichotamka ni kuwa anaomba ushirikiano wa kila hali ili mambo yasiende upogo.
Maximo hakuwahi kutamka kwamba lazima tufike Ghana katika Kombe la Mataifa Afrika. Daima amekuwa akisisitiza uboreshaji wa vipaji vya soka kwa miaka ijayo.
Huyu si malaika na wala si mfalme njozi. Tuache kumshambulia kwa makombora ya lawama. Mwacheni apumzike aangalie namna ya kukisuka upya kikosi chake kwa mashindano yajayo.
Isingelikuwa rahisi kwa Maximo kwenda Ghana na Stars yenye wachezaji ambao huko nyuma hawakuandaliwa vizuri.
Nani asiyejua kuwa soka ya Tanzania ilikuwa kama yatima aliyekosa malezi? Nani hajui kwamba mamlaka za soka enzi hizo zilijaa ubabaishaji? Nani hajui kwamba ofisi za soka ziligeuzwa sehemu za kupiga soga?
Hawa wachezaji waliopo ni kizazi kile kile ambacho walezi hawakuwa makini kuwatumikia. Waliachwa wajiamulie mambo yao. Viongozi wao hawakufunda nidhamu.
Wachezaji hawa wangali wanahitaji muda kuandaliwa kwa umakini. Na ndio maana wengine husema kwamba ni vigumu kumfuza mbwa mbinu mpya.
Hao wanaomlaani Maximo na wasimame waseme ni wapi kuna kitalu cha soka hapa nchini? Kwamba kuna mahala waweza kwenda ukawakuta wachezaji wakipikwa? Hakuna!
Wachezaji waliopo ni wale wa kuokotwa Simba, Yanga na Mtibwa. Huko kuna kitu gani kipya? Miaka nenda rudi wamekuwa wakiendesha kile kinachoitwa fitna ndani ya soka.
Mwandika Busati haoni kama kuna haja ya kumnyooshea Maximo vidole vya uhasama. Kajitahidi na kwa kasi yake akipewa muda ataweza kuwapa Watanzania furaha katika miaka ijayo.
Hebu msikizeni Maximo, mpeni muda kama alivyoomba na juzi kasema wazi kuwa kushindwa kwa Stars kwenda Ghana si mwisho wa programu zake.
Mwacheni anywe mvinyo wake kwa raha. Msimpe karaha kiasi hicho. Hao waliovurunda zaidi hadi soka ikageuka kuwa mchezo wa wahuni mbona hamuwataji? Hofu yenu i wapi?
Hubirini mabaya yao pia. Kuna wengi wamechangia soka kuwa kijiwe. Wakila posho za wachezaji na hata wafadhili walipojitolea kuweka fedha kwa maendeleo ya soka, viongozi hao pasipo soni wakainua vinywa na kubwia fedha hizo. Mbona hamuwasemi?
Mzee wa Busati anakomea hapa kwa msisitizo kwamba kuendelea kumsimanga Maximo ni kumfanyia makosa. Mpeni muda Mwanawane.
Jumanne hii Mwandika Busati anaweka miguu juu akiangalia namna wapenda amani wanavyokumbuka mlipuko ulioua Wamarekani kwenye ardhi yao miaka sita nyuma. Wakasema Osama bin Laden alihusika.
Vinginevyo kila jambo laenda sawia, ngwenje za maji ya kunywa zingalipo na hata yale maji ya dhahabu hayampigi chenga kwa tarehe kama hizi. Neema ingalipo.
Wasalaam,
Tuesday, September 11, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment