LONDON, Uingereza
HATIMAYE Gordon Brown amesafishiwa njia ya kuvaa viatu vya Tony Blair katika nafasi ya waziri mkuu na kiongozi wa chama cha Labour kuanzia Juni 27 mwaka huu.
Ameingia katika maisha mapya kwa kishindo cha kura 313 kati ya 352 zilizopigwa na wabunge wa chama chake.
Brown mwenye kuonyesha msimamo katika mambo mengi anayoyazungumza ametangaza rasmi kuwa na siasa tofauti na waliomtangulia.
Lakini kubwa lililowaingia waliompigia kura na pengine wanachama wake ni kauli yake kwamba atakuwa msikivu na kujifunza.
“Naahidi kujenga imani ya katika harakati za kisiasa,” anasema Brown anayesubiri siku rasmi ya kuvaa viatu vya Blair.
Si ajabu Brown akajenga ukuta wa kujitofautisha na kiongozi anayemaliza wake. Jambo hilo linawezekana kutokana na hali hali kwamba mara nyingi anayeingia ofisini kwa mara ya kwanza sharti aje na falsafa zake.
Hilo huenda likatimia kwani ameshaapa kubadili baadhi ya sera na kwamba kuingia kwake ofisini kutakwenda pamoja na ziara katika shule, polisi na kuwatembelea viongozi wa kijamii.
“Naamini Serikali hufanya kazi kama itajitoa kwa moyo mmoja kuwahudumia watu wake.
"Tujenge na kuimarisha demokrasia na nadhani tunahitaji wigo mpana na kuwa wazi zaidi kwa kuruhusu wanasiasa na wananchi wa kawaida kujadili kwa pamoja matatizo na njia za kuyatatua.
"Ni siasa za mtazamo tofauti, uwazi na ukweli,” anasema.
Kama ilivyosemwa awali kwamba si ajabu Brown akafanya mabadiliko ya haraka katika muda mfupi katika ofisi yake mpya.
Ushahidi wa hilo umo katika matamshi yake ya hivi juzi hasa alipozungumzia vita ya Irak.
Anasema kumekuwa na mgawanyiko mkubwa wa maoni katika jamii ya Waingereza kuhusiana na ushiriki wake wa vita nchini Irak.
Kutokana na mgawanyiko huo, Brown ameahidi kufuata mfumo wa ‘wengi wape’ na kwamba atawasikiliza wote ambao ‘sauti zao hazikusikika’ juu ya suala hilo.
Kwamba chini ya utawala wake, lengo kuu ni kurejesha imani kwa waliokuwa wamekata tamaa katika masuala ya siasa.
Ni wazi kwamba Brown ambaye kwa muda mrefu amekuwa akionyesha dalili za kumrithi Blair, atafanya mageuzi makubwa na hivyo kurejesha imani kwa watu wake.
Idadi kubwa ya kura alizopata ni ishara kwamba walio wengi wana matumaini makubwa kutoka kwa mwanasiasa huyo aliyepigiwa chapuo na Jack Straw.
Straw naye ameonyesha mshangao wake juu ya kukubalika kwa mtu wake akisema kuwa amestaajabu na kilichotokea.
Brown mwenyewe anasema kinachoonekana hapo ni kwamba Labour waliamua kufuta mabaya ya nyuma na kuweka msimamo wa pamoja kuhakikisha kuwa chama chao kinabaki madarakani.
Lakini wapinzani wake katika siasa wameshapiga ‘kelele’ kwamba Brown hawezi kubadili mawazo ya raia wake.
Kiongozi wa Liberal Democrat, Menzies Campbell anasema ipo haja ya kuitisha uchaguzi.
Kauli kama hiyo inafanana na ya kiongozi wa Conservative, David Cameron anayesisitiza umuhimu wa kufanya uchaguzi kabla ya Brown kupewa Serikali.
Anaongeza: "Tutakuwa na wiki kadhaa ambazo waziri mkuu atakuwa katika ziara ya kuaga na wakati huo hatutakuwa na mtu wa kuiongoza Serikali.”
Lakini wakati wapinzani wakitamka hayo, Brown mbali na kusema kuwa atasikiliza maoni juu ya ushiriki wa vita nchini Irak, ameahidi kuendeleza uhusiano mwema na Marekani.
Wakati Brown anashinda, Blair alikuwa jijini Washington akifanya mazungumzo na Rais George Bush na Brown alipoulizwa uhusiano wa Uingereza na White House bila kumtaja Bush, alisisitiza kujenga uhusiano wa miaka mingi.
“Uhusiano na Marekani utaendelea kuwa imara,” anasema Brown. “Lakini si kwamba nitaegemea sera za nje pekee bali pia nitaboresha huduma za jamii.”
Msimamo wake wa kuendeleza uhusiano na Marekani unaleta shaka pia kama ataridhia kuyaondoa majeshi ya Uingereza nchini Irak.
James Gordon Brown alizaliwa Februari 20 mwaka 1951 mjini Glasgow, Scotland.
Anatajwa kuwa mmoja wa wanasiasa wenye ushawishi mkubwa nchini Uingereza. Mara baada ya kuapishwa kwake atakutana na Malkia wa Uingereza kuunda Serikali.
Alianza elimu ya sekondari ya Kirkcaldy ambako alifanya vizuri sana katika masomo yake na hivyo kumrusha madarasa.
Alikubaliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Edinburgh akiwa na umri wa miaka 16 na kujiunga na masomo ya historia.
Hata hivyo, katika kipindi hicho alikumbwa na tatizo la jicho na kuna maelezo kwamba hitilafu hiyo ilitokana na pilika za kucheza rugby.
Jitihada mbalimbali za madaktari waliomfanyia upasuaji mara kadhaa zilimnusuru kuwa kipofu.
Brown alipata shahada ya pili mwaka 1972, ikiwa ni ya daraja la kwanza na baadaye kuupata udaktari mwaka 1982.
Amepata kufundisha Chuo Kikuu cha Edinburgh na baadaye kuwa mwandishi wa habari katika televisheni ya taifa ya Scotland.
Monday, September 3, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment