na innocent munyuku
MAMBO yanasonga mbele na bila shaka mdau wa safu hii waendelea kujinafasi na kulijenga taifa la Wadanganyika. Lakini ni taifa jema kwani wenyeji wake wamefundwa kuwa wapole.
Mambo yamekuwa magumu kila kukicha, walalahoi wanabaki kulalama chini kwa chini. Ndimi zao haziteti kwa mapana. Watasema vipi wakati ukisema sana waitwa mchochezi au mpinga uzalendo?
Tuachane na hayo kwani yawezekana hapa si mahala pake lakini Mzee wa Busati aliona agusie japo kidogo kwani huo ni utaratibu wa salamu za Kiafrika. Huwa ni ndefu kupidukia. Kwa utaratibu wa salamu za Kiafrika si ajabu mkaulizana hata afya ya mifugo nyumbani, jirani zako na mengine mengi.
Wiki hii Mwandika Busati katumbukia kwenye Kombe la Tusker ambalo Jumamosi hii litaanza kunguruma kwenye dimba la Jamhuri mjini Morogoro.
Simba ndiyo itakayokuwa ya kwanza kufungua michuano hiyo dhidi ya Tusker ya Kenya na siku inayofuata Yanga itapepetana na SC Villa ya Uganda.
Timu nyingine zinazowania kombe hilo ni bingwa mtetezi Kagera Sugar na wakata miwa wa Mtibwa Sugar.
Mzee wa Busati ana lake la kusema juu ya washiriki wa michuano hiyo ambayo kwa miaka sita sasa inazidi kuwavutia mashabiki wa soka katika Afrika Mashariki. Kwamba washiriki wa mashindano hayo kwa mwaka huu hawana budi kuonyesha ukomavu dimbani.
Lakini kuna kitu kingine ambacho kimemfanya Mwandika Busati apate cha kusema. Nacho ni juu ya kauli ya aliyewahi kuwa kocha wa Simba na baadaye Mtibwa Sugar, James Siang’a kwamba kuna tabia ya viongozi wa klabu kununua mechi.
Siang’a hakuwa msiri katika jambo hilo aliweka wazi kuwa viongozi wa Simba wakati fulani waliwahi kuwahonga waamuzi ili waibuke na ushindi.
Kauli hiyo ilimduwaza Mzee wa Busati lakini kwa namna mbili. Mosi ni kwamba iweje kocha huyo aibuke kunena hayo wakati huu au ni kwa vile ‘biashara’ ilishakwisha? Pili ni kwamba kuna uhondo gani wa kujigamba kwamba weye ni bingwa au mshindi kwa kununua mechi?
Pamoja na ukweli kwamba kocha huyo wa zamani amechelewa kutoa kauli hiyo bado kuna haja ya kuifanyia kazi hasa wakati huu mashindano ya Kombe la Tusker yanapokaribia.
Kilichonenwa na Siang’a yawezekana kinafanywa kwenye timu nyingine pia. Kama yapo basi yadhibitiwe ili kulinda heshima ya soka na maendeleo yake kwa maslahi ya wadau wake.
Yafaa nini basi kulalama kwamba soka laenda upogo wakati twajimaliza kwa kuwapa waamuzi vijisenti vya kupindisha sheria za soka dimbani?
Kumbe mwajidanganya kwa vilio vyenu. Mnajua wapi mmejaza halafa na uzandiki wenu. Hayo yote mwayajua lakini mwawafanya wengine kuwa mabahau kwa ndimi zenu zenye fitina.
Kinachosemwa na Mzee wa Busati ni kwamba katika mashindano ya Tusker kusiwepo na uovu wa aina hiyo. Waamuzi wafuate kanuni na misingi ya kazi zao. Hakuna haja ya kuendekeza njaa huku mnawanyonga wengine.
Inasemwa kuwa waamuzi wanalazimika kuchukua kitu kidogo kwa sababu posho hazitoshi. Huenda hiyo ikawa hoja ya msingi kabisa kwamba waongezewe lakini je, ndio mhalalishe rushwa kiasi hicho?
Amkeni sasa kumaliza tatizo hilo. Tambueni kwamba upendeleo usio wa lazima uwanjani husababisha vurugu kwa mashabiki na si ajabu yakatokea maafa pia.
Na ndio maana Mzee wa Busati analilia umuhimu wa kuiweka akilini kauli ya Siang’a kwa kuwafichua au kuwanyoshea kidole wapenda mlungula.
Waambieni kuwa wanachofanya ni kuua soka nchini na mwisho wa siku watabaki kulaumiwa kwa vile walitumia filimbi zao vibaya. Kwamba walisikilizia njaa zao wakanyoosha mikono kupokea kile walichokiita mafao.
Lakini kwa upande mwingine hawa ni kama hamnazo kwani bongo zao zimejaa uozo unaosababisha mizozo.
Mzee wa Busati anafika ukomo kwa Jumanne hii akiamini kuwa machache aliyonena yamewaingia wahusika. Soka isiharibiwe kwa njaa zenu.
Vinginevyo kwa wadau wa Mwandika Busati jioni ya leo mwakaribishwa kwa ajili ya karamu kwani leo hii ni siku muhimu kwake. Hata kama una mdomo mpana usihofu, maakuli yamejaa tele na vimiminika kwa kwenda mbele.
Mwashangaa? Endeleeni kushangaa kwa mwaliko lakini msije mkasema kwamba ni harusi au kipaimara ni siku ya shukurani kwa Allah kwani kaendelea kumsogezea miaka ya kuishi.
Wasalaam,
Monday, September 3, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment