Monday, September 3, 2007

Pepo la makocha Simba halipungwi kwa ungo

Na Innocent Munyuku

Kwa jina la mweza wa yote nakupa salamu za heri mdau wa Busati la Burudani. Mwenye Busati hana shaka wala dhiki kwani mambo yanakwenda kwa neema.

Hata hivyo, Mzee wa Busati ameona ni jambo la heri akiri kwamba kwa juma hili atakuwa adimu kwenye viunga vya kawaida. Hakika atakwenda mafichoni kwa ajili ya kupumzisha ubavu wake baada ya siku tele za kuwania nafasi kwenye daladala.

Lililo moyoni mwaka juma hili ni hili la Wekundu wa Msimbazi ambao kila kukicha wanasaka kocha na kumtimua. Kina Tupasyege wameandika juu ya hilo lakini Mzee wa Busati ana mtazamo tofauti.

Hataandika kuhusu ubovu wa uongozi na wala hatasema habari ya viongozi kuwa na uelewa mdogo katika masuala ya soka. Hilo anawaachia wenye ubavu wa kutema cheche. Mzee wa Busati hajazoea tafrani.

Mwataka aseme eti vinara wa Simba ni wabovu? La hasha! Au mwaridhia Mwenye Busati aseme kwamba kuna uvundo katika uongozi mzima wa Simba? Hapana. Hilo msitarajie hadi kiama kije.

Kama kuna wanaodhani kwamba Mwandika Busati atasimama kidete kusema ya kuwa ndani ya Simba kuna uzembe, hao wamenoa kwani siku kama hiyo haitafika.

Kwanini asimame atete juu ya maovu ya Simba wakati kuna Simba wa Yuda? Huyu aliyesifika kwa makali yake wakati alipokalia kiti cha Katibu Mkuu wa chama cha soka. Mwacheni aendelee kuwamo humo.

Lakini Mzee wa Busati angali na dukuduku juu ya hawa ndugu zake wenye maskani yao Mtaa wa Msimbazi jijini Darisalama. Wana mkosi gani hawa? Mbona makocha hawakai kwa muda mrefu kabla ya kutimka?

Je, ni kweli kwamba hao makocha wanaotua Msimbazi hawajui wanachokwenda kukifanya ndani ya Simba? Au mwataka tuamini kuwa huko wanakosaini mikataba kumejaa uvundo?

Yu wapi Trot Moloto? Neider dos Santos, mzee mzima wa Zambia Patrick Phiri nao walijaribu bahati yao na leo hawapo. Wameondoka na hivi karibuni katoweka Nielsen Elias aliyeamua kurejea kwao nchini Brazil.

Mara baada ya kuondoka ikaelezwa kuwa Elias ameshindwa kuendelea kukaa nchini kutokana na madai kuwa viongozi wa klabu hiyo wameshindwa kutekeleza majukumu yao na kusababisha kufanya kazi yake katika hali ngumu.

Mbrazili huyo ameondoka wakati Simba inashiriki Ligi Ndogo Tanzania Bara na hakufanya mkutano na uongozi wa timu kabla ya kuondoka kwake.

Hilo hawezi kulaumiwa kwani yasemwa kwamba wakati mwingine ni heri kuiga ujinga kuliko kuendeleza ustaarabu mbele ya mazuzu.

Mwaka juzi, Mzee wa Busati alikuwa nchini Zambia wakati huo Simba ilikuwa ikicheza na Zanaco kuwania fainali za Klabu Bingwa Afrika huku Phiri akiwa kocha wa Simba. Kulikuwa na mjadala mrefu juu ya majaliwa ya Simba katika mechi hiyo ambayo ilimalizika kwa wenyeji kushinda kwa mabao 3-1.

Katika mazungumzo mafupi kwenye Hoteli ya St. Andrew’s jijini Lusaka, Phiri alionyesha wasiwasi wake juu ya hatima yake ndani ya Simba. Alikuwa akilalama juu ya maisha halisi kama kocha nchini Tanzania.

Akaweka wazi kwamba ahadi nyingi zilizotolewa na uongozi wa Simba hazijatekelezwa na kulikuwa na kila dalili ya kutotekelezwa. Akarejea Darisalama na baada ya muda mfupi akachomoka akiiacha Simba chini ya Jamhuri Kihwelo.

Tatizo kama hilo ndilo lililowakuta kina Santos na Nielsen. Ahadi za Simba hazitekelezeki, kuna ubabaishaji mwingi ndani ya klabu hiyo. Kutekeleza ahadi limekuwa jambo gumu kama vile kuzikutanisha mbingu na ardhi.

Basi kama mmeshindwa kuwa na makocha kutoka ughaibuni ni heri mchukue nafasi hii kuwaajiri wenyeji waliozoea longolongo zenu. Kinachoonekana hapa ni kwamba pepo la makocha Simba haliwezi kupungwa hata kwa ungo.

Msilete aibu kwa taifa letu kwani matokeo yake huko mbele ya safari ni mabaya kuliko mnavyodhani. Tekelezeni ahadi zenu na kamwe msimwige tembo maliwatoni.

Kama mna senti 10 semeni uwezo wenu ni huo na msije mkajidanganya kwamba mna ubavu wa kutoa senti 20 mtapasuka msamba.

Vinginevyo Mwenye Busati anafikia mwisho wiki hii ya neema. Wiki ya kumwaga maharagwe na kupisha vipapatio vya kuku vifanye kazi yake tumboni.

Nyama ya ng’ombe, mbuzi haziliki kwani RVF imetawala. Hata panya buku wa Pachoto nao hawaliki. Basi imekuwa balaa.
Wasalaam,

No comments: