na innocent munyuku
HERMAN Kirigini si jina geni katika ulimwengu wa siasa nchini Tanzania. Ameshaliwakilisha bungeni jimbo la Musoma Vijijini kuanzia mwaka 1975 hadi 1985. Hivi karibuni mkongwe huyo wa siasa amezungumza na RAI katika mahojiano maalumu kuhusu mustakabali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kagusia Muungano na kurejeshwa kwa Serikali ya Tanganyika.
Akizungumzia juu ya mchakato wa Shirikisho la Mashariki, Kirigini anasema kimsingi watawala wa nchi zote tatu yaani Kenya, Uganda na Tanzania wamewaburuza wananchi wake.
Kwa mtazamo wake, nchi kama Tanzania inaburuzwa kuingia katika muungano huo na kwamba rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa anastahili lawama kwa kuridhia jambo hilo.
“Huyu wa kwetu niseme kwa uwazi kabisa aliburuzwa. Ndiyo! Mkapa aliburuzwa kwa sababu alikuwa dhaifu,” anasema na kuongeza kuwa Tanzania inakimbilia huko pasipo kujua udhaifu wao kiuchumi.
Anasema kuwa kwa kasi ya ukuaji wa uchumi unaofanywa na Kenya ni wazi Tanzania itamezwa katika jumuiya hiyo.
Kwamba Tanzania na Uganda si ajabu zikawa dampo la bidhaa kutoka Kenya kutokana na takwimu za mwaka uliopita juu ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi.
Mwaka jana, Kenya iliiuzia Tanzania na Uganda bidhaa mbalimbali za viwandani zenye thamani ya dola za Marekani milioni 593.351 wakati Tanzania na Uganda zikiiuzia Kenya bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani milioni 186.200.
Katika mwaka huo huo, Uganda na Tanzania ziliagiza kutoka Kenya bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani milioni 638.992 na hii kwa mtazamo wa Kirigini nchi hizi hazina uwezo sawa kiushindani.
“Uchumi wa Tanzania na Uganda unategemea zaidi kilimo cha mazao wakati ule wa Kenya ukitegemea viwanda na huduma,” anasema Kirigini na kisha kuongeza:
“Hali hii inaufanya uchumi wa Kenya kuwa imara zaidi kushinda wa Tanzania na Uganda unaotegemea hali ya hewa wakati ule Kenya ambao daima unategemea uzalishaji wa bidhaa za viwandani.”
Lakini pia Kirigini anasema kuwa nchi hizi tatu katika suala la mapato na bajeti zake kwa mwaka hayalingani. Kwamba Kenya inapata dola bilioni 3.715 na matumizi yao ni dola 3.88.
Tanzania inapata dola za Marekani bilioni 2.235 huku matumizi yake yakiwa dola 2.669. Uganda inapata dola bilioni 1.845 na inatumia dola bilioni 1.904 kwa mwaka.
“Ndiyo maana nasema wananchi wanaburuzwa na viongozi wa kisiasa katika jambo hili,” anasema.
Hata hivyo, anasisitiza kuwa hili suala la watu kutangaza kutaka maoni juu ya wananchi kuhusu shirikisho ni hadaa kwani maamuzi yalishafanywa.
“Leo hii unawauliza wananchi inasaidia nini? Hii ni hadaa, wangepewa nafasi ya kwanza kutoa maoni. Hivi kweli hatukumbuki tulivyoumia baada ya Jumuiya ya awali iliyovunjika mwaka 1977? Nani walifaidika zaidi kama sio Wakenya?”
Anasema wakati jumuiya inavunjika njia kuu za uchumi zilikuwa zikishikiliwa Kenya na wao wakaziendeleza kwa maslahi yao.
“Tuliumwa na nyoka na je, leo tuna uhakika gani kama muungano huu hautavunjika?” anahoji Kirigini.
Akizungumzia suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Kirigini anaeleza kuwa Rais Jakaya Kikwete ameachwa peke yake.
“Kikwete analia peke yake katika kutatua mgogoro wa kisiasa Visiwani na kasoro za Muungano. Hawa viongozi wa CCM hawampi ushirikiano kukemea maovu ya Zanzibar.
“Kasimama bungeni (Kikwete) na kusema kuwa kuna mpasuko wa kisiasa Zanzibar lakini mbona hawamsaidii kuyakemea?
“Zanzibar kuna tatizo kubwa sana, Karume ni sawa na Salmin Amour wanalewa madaraka.”
Anasema kutokana na kasoro hizo ipo siku hoja ya Serikali ya Tanganyika itaibuka upya.
“Mimi nasema Serikali ya Tanganyika lazima itarudi na kosa alilofanya Nyerere ni kutokubali kubaki na Tanganyika, amefariki dunia akilijua hilo na hakuweza kurudi nyuma,” anasema Kirigini.
“Lakini mbali na jambo hilo, jambo jingine ni kwamba wengi waliomfuata Nyerere walikuwa wanafiki, walimwogopa badala ya kumshauri.
“Mimi sikutaka kuwa katika mkumbo huo na ndio maana wakati fulani bungeni nilichachamaa kwa kuwatetea wakulima wa pamba.
“Hili si Bunge, nakumbuka katika utetezi wangu kwa wakulima, Mwalimu alitaka kunikamata, alidai mimi na wenzangu tunapinga chama ndani ya Bunge.”
Anasema alichofunza katika miaka yake kama mwanasiasa ni kwamba CCM haitaki kuukubali upinzani na kutokana na misimamo yake, wana-CCM wengi wamekuwa wakimtenga kwa kumwona msaliti.
“Mwaka 1987 niliomba ujumbe wa NEC nikapewa alama ya E na kwamba mimi ni msaliti wa kisiasa, nikaandika barua Halmashauri Kuu lakini hadi hii leo sijajibiwa.
“Nikaonekana mbaya kwa watu wa mkoa wangu lakini upinzani ule leo hii ndio huo ambao umekubalika. Kuna chama kama CUF ni vema kikaendelea kuwepo ili pawe na criticism.”
Anaeleza kuwa mawazo makongwe hasa kutoka kwa baadhi ya wanasiasa wasiokubali mabadiliko yamesababisha CCM wakati mwingine kukosa mwamko.
“Lakini bado nakubali kwamba hawa walioko CCM baadhi yao wakitoka na kuunda chama kingine chama hicho kitakuwa bora kwani wapinzani wa kweli wangali humo.”
Kuhusu mwaka mmoja wa Serikali ya Kikwete, Kirigini anaeleza kuwa mtawala huyo anakubalika na wengi lakini kasi yake wengi hawaiwezi.
“Kikwete ana kasi ya ajabu na mtu mzuri lakini watu wake (viongozi) hawaendi naye. Wameachwa nyuma na kama mpiganaji, anatakiwa arudi nyuma aangalie majeshi yake mfano ni hizi Serikali za Mitaa zimeoza.”
Hata hivyo, anapingana na utaratibu wa Serikali kuwachangisha wananchi kwa ajili ya sherehe za Uhuru. Anasema kimsingi ni heri jambo hilo likawa katika bajeti.
“Waliochanga wengi ni wafanyabiashara na kwa kawaida wafanyabiashara hawana nia nzuri, wanakuwa na lao jambo.”
Kirigini ambaye kitaaluma ni Bwanashamba alizaliwa Desemba 22, 1955 ameoa na ana watoto wanane mmoja kati ya hao ni Rosemary Kirigini ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM).
Kirigini amewahi kuwa Waziri wa Mifugo kati ya mwaka 1980-83 na kati ya mwaka 1983-85 akawa Waziri wa Nchi anayeshughulikia mifugo.
Amewahi pia kuwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga na Arusha kati ya mwaka 1993-96. Ana shahada ya kilimo aliyoipata Chuo Kikuu cha Makerere mwaka 1970.
Monday, September 3, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment