Na Innocent Munyuku
AGHALABU jambo likifanywa pasipo utaratibu unaoeleweka basi wajuvi wa Kiswahili husema kwamba jambo hilo ni hobelahobela.
Pengine husemwa jambo husika limekaa ovyoovyo na wakati mwingine hujulikana kuwa ni tabia ya mtu kushika huku na huku. Yawezekana kuwa mtu huyo hajui kipi afuate.
Mzee wa Busati yu babarani tena kutimiza majukumu yake ya kila siku hasa Jumatatu kama hii ambayo kishajitia kitanzi cha kuleta porojo zake kwa waungwana wake.
Kitanzi hiki chafanana na ile methali ya mwana wa mbuzi kwamba kamba ni yake labda kama atakuwa amezaliwa Ulaya. Hakikwepeki kikombe hiki lazima kinyweke.
Wiki hii iliyopita imekuwa ngumu kidogo kwa Mwandika Busati. Si kwamba alikosa ngwenje za kukaa viti virefu kusafisha koo kwa maji yafananayo na rangi ya mende la hasha! Bali taabu ya kuupindisha ubongo kusikiza wenye kutoa maoni juu ya uteuzi wa timu ya taifa maarufu kama Taifa Stars.
Imekuwa hoja kuu au mada kuu kwenye vijiwe vya wajuzi wa soka na wasiojua. Kila mmoja anafuata haki ya kikatiba katika kutoa maoni pasipo kuvunja sheria.
Kelele zimepigwa lakini waendesha jahazi wameonekana kuwa baadhi ya makocha wazalendo ambao kwa mtazamo wao wanasema kwamba Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Marcio Maximo kutoka Brazil hajafanya uteuzi mzuri.
Kisa? Wanasema kafanya kosa kwa vile kawaacha wachezaji nyota katika timu hiyo! Mzee wa Busati akahoji wa wapi hao maarufu? Akaambiwa eti ni pamoja na Gaudence Mwaikimbika na Juma Kaseja.
Wengine ni Hamis Yusuph, Haji Mbelwa, Said Swedi, Athumani Idd na Mussa Hassan Mgosi.
Mzee wa Busati si mwepesi wa kutoa hukumu au hoja za ghafla. Mara nyingi husubiri wenye akili timamu waseme naye awe wa mwisho kupayuka.
Lakini hivi kweli madongo kwa Maximo yanatoka moyoni au kuna utani unaendelea hapa? Wakati timu hiyo wakipokea kipigo cha mabao 4-0 Machi 24 mwaka huu mjini Dakar nchini Senegal hao wachezaji wanaopachikwa jina la nyota si walikuwapo dimbani? Walileta miujiza gani?
Tusidanganyane katika hili. Kama vipi ni bora mkae pembeni msubiri maji ya moto yaliyochanganywa na mahindi yaliyounguzwa. Wengine wakiamini kuwa wanakunywa kahawa.
Kwa hakika Mzee wa Busati haoni ubaya uliofanywa na Maximo katika uteuzi wa kikosi cha Stars katika mechi ya marudiano na Senegal Juni Pili jijini Mwanza.
Haoni ubaya kwa sababu Mwenye Busati anaamini kuwa anachofanya ni sahihi na kama mlitegemea kina Mwaikimba watuvushe hilo si sahihi.
Hoja hapa ni kwamba hata kama wachezaji hao waliotemwa watakuwa uwanjani Juni Pili bado kibarua ni kigumu.
Tatizo la wachezaji wetu wa Tanzania si la Maximo. Huu mzigo ni wa kwetu pamoja na hao wanakaza misuli ya koo kumlaani.
Ndiyo! Ni Tatizo letu Watanzania ambao huko nyuma hatukuwaza kujenga vitalu vya soka. Sasa je, mwataka Maximo awakunje samaki wakavu? Ubavu huo atautoa wapi?
Bila shaka ndicho wanachowaza hawa wadau wenye ‘uchungu’ na soka ya Tanzania. Wanataka huyu mwana wa Barcellos aonyeshe miujiza ya kutembea juu ya maji kama alivyofanya Yesu aliyenenwa kwenye Biblia.
Mtazamo wa Mzee wa Busati kwamba kuna wachezaji nyota wameachwa ni sawa na kutetea matumizi ya wanjamanga kwenye jicho lenye chongo.
Bila kificho wanjamanga katu hauwezi kuwa dawa ya chongo. Chongo ni chongo hata ukipata wanja si rahisi kufuta kilema hicho. Ndiyo haya ya Taifa Stars tusikae na kuanza ndoto za kuwanyamazisha Senegal kwa kuwapanda kina Mwaikimba au Kaseja. Hawana jipya hawa.
Hebu inueni midomo na mseme bila woga, ustaa wa wachezaji hawa ni wa kimataifa au wa huku kwetu Maneremango? Lini basi walitoka nje ya Tanzania na kuwika huko ughaibuni?
Kama si hao basi wapo wengine waliojaribu kwenda nje ya ardhi ya Wadanganyika kuuza matunda na maduka ya vipuri huko ughaibuni. Hamkusikia na habari ya wengine waliokuwa wakiokota matunda bustanini?
Hebu tumwache huyo Maximo afanye kazi yake ambayo hapa kwa Mwenye Busati imani ni kwamba analenga kujenga timu kwa ajili ya miaka ijayo.
Mzee Marcio Maximo Barcellos kaza buti fanya kazi yako na ukiona wanakukera wakumbushe kauli yako ya awali ulipotua Bongoland kwamba hukuja na miujiza ya soka. La maana ni kumpa moyo na si kumvunja moyoni. Mpeni nafasi!
Wasalaam,
Monday, September 3, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment