Monday, September 3, 2007

Upinzani: Mkianguka hapa tundikeni madaruga

Na Innocent Munyuku

KATI ya wanaharakati na wapigania uhuru ninaowaheshimu katika maisha yangu ni pamoja na marehemu Stephen Bantu Biko. Huyu aliuawa na utawala wa makaburu nchini Afrika Kusini Septemba 12 mwaka 1977.

Namheshimu kutokana na msimamo aliokuwa nao na moyo wa ujasiri wa kuwatetea watu wake. Hakuwa mwoga licha ya Afrika Kusini wakati huo ‘kuwaka’ moto wa kibaguzi. Makaburu wakiwabagua Weusi na kuwanyima haki za kibinadamu.

Mengi yamesemwa juu ya hali ya hatari ilivyokuwa wakati huo. Lakini Biko hakuwahi kutetereka katika kusimamia imani yake ya kuwakomboa watu Weusi kutoka kwenye makucha ya makaburu.

Mara kadhaa alisikika akisema: “Ni heri kufa ukitetea mawazo yenye uhai kuliko kuishi kwa mawazo yatakayokufa.”

Msemo wake huo ulijenga hamasa kubwa kwa wafuasi wake na kujipatia umaarufu mkubwa kutokana na ushawishi wa kuwaunganisha Watu Weusi nchini Afrika Kusini.

Wakati mwingine Biko alitamka: "Kitendo kidogo tu cha kujitambua kuwa wewe ni mweusi basi tayari umeshaanza safari ya kusaka uhuru wako. Tayari umeanza vita dhidi ya wanaotumia rangi yako nyeusi kukuona kuwa si mwanadamu.”

Nimeanza na kumbukumbu ya Biko baada ya kuona vyama vya vinne vya upinzani katika siasa nchini Tanzania vikianza mbio za muungano kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.

Vyama hivyo ni Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na TLP ambavyo kwa pamoja Alhamisi wiki hii vilitiliana saini katika pamoja la nia yao ya kuungana.

Katika tamko hilo pamoja na mambo mengine wanasema kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya kuelewa kwamba mageuzi ya dhati hayawezi kupatikana bila kwanza vyama vya kisiasa vya upinzani kuunganisha nguvu zao.

Kwamba wasipofanya hivyo litakuwa jambo gumu kukiondoa Chama Cha Mapinduzi katika dola.

Wakadai pia kuwa muungano wa aina hiyo hauna budi kuja kwa wakati huu kwani mfumo uliopo umeendelea kuzuia demorasia, umedidimiza haki na uchumi wa Tanzania unazidi kudidimia.

Lakini hawakuishia hapo wakasema kuwa kuna ukandamizwaji unaendeshwa na Serikali na rushwa nayo inawatafuna Watanzania huku ufisadi ukipambana moto miongoni mwa watawala.

Nilikuwapo katika hafla hiyo ya kutiliana saini tamko hilo kwenye Makao Makuu ya Chama cha Wananchi (CUF) eneo la Buguruni jijini Dar es Salaam Alhamisi wiki hii na moja ya kauli iliyonivuta kuandika makala hii fupi ni ya Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema kwamba hataomba madaraka katika muungano huo.

Nilivutwa na Mrema kutokana na historia ya mwanasiasa huyo machachari ambaye wakati fulani ilisemwa kwamba linapokuja suala la muungano yeye hutaki awe kinara kwa maana ya kiongozi wa juu.

Hata alipopata nafasi ya kujibu maswali mbalimbali ya waandishi wa habari siku hiyo, Mrema alisisitiza dhamira yake ya kweli kukubali yaishe kwa jina la muungano.

“Tupone kwa pamoja au tufe kwa pamoja,” alisema Mrema na kuongeza kuwa muda wa kusaka ushindi wa chama kimoja kimoja umepitwa na wakati.

Siku ya pili yake yaani juzi Ijumaa nikazungumza tena na Mrema nikamweleza kuwa watu mitaani wameanza minong’ono kwamba si rahisi kwake kukubali kuwa chini ya mwingine.
Alichonijibu Mrema ni kwamba kila jambo na wakati wake na sasa imetosha hataki tena kuona wanashindwa kwa uchaguzi eti kwa sababu tu vyama vya upinzani vimeshindwa kuungana.

Lakini pia akatamka tena kwamba hana haja ya madaraka kwani alishawahi kuwa na nafasi za juu katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Jibu hilo la Mrema ndilo nikumbuke falsafa za marehemu Stephen Biko kwamba kitendo cha kujitambua wewe ni nani tayari umeanza safari kusaka uhuru wako. Tayari umeanza vita dhidi ya wanaotumia udhaifu wako kukutenga na haki zako.

Pamoja na msimamo huo wa vyama hivyo na kauli njema ya Mrema ningali na jambo moja moyoni ambalo nisipolitema nitakuwa sijatenda haki kwa wanaosafiria boti hiyo ya muungano wa upinzani.

Kwamba dira hapa isiwe katika uchaguzi wa mwaka 2010 pekee bali muungano huo ulenge mapambano ya kweli miaka ijayo.

Nasema hivyo kutokana na ukweli kwamba nawafahamu Watanzania wenzangu. Walio wengi ni waoga wa mabadiliko ni wepesi wa kusahau machungu ya leo. Jengeni utaratibu mwafaka wa kutoa elimu kwa wanachama wenu.

Waelewe nini dhamira yenu na mwelekeo wa muungano wenu. Vinara wa umoja huo wawe mfano kwa wanaowaongoza. Na kilichoahidiwa siku ya kusaini tamko hilo kiwe kweli na isiwe kama hadithi za kale. Mkianguka hapa tundikeni madaruga!

No comments: