Monday, September 3, 2007

Subirini kufurushwa

Na Innocent Munyuku

WAHENGA walipata kusema kuwa asiyesikia la mkuu huvunjika guu. Upo usemi mwingine ufananao na huo ‘sikio la kufa halisikii dawa’.

Husemwa pia kuwa hakuna jema lililonenwa na wahenga ambalo litapita pasipo faida kwa jamii husika.

Kwamba kina haambiliki daima huonja joto ya jiwe. Sumu haionjwi hali kadhalika moto wa tanuru haizimwi kwa petroli.

Leo hii katika fani ya muziki hasa huu mnaouita wa kizazi kipya kumejaa kina haambilikiz. Hawa hawasikii la mtu na vichwa vyao vimejazwa sifa za kijinga.

Mzee wa Busati kaona leo aweke wazi mambo ambayo anadhani yanawaumiza hawa wasanii. Lakini wakati huo huo uhalisi wa vitu ni kwamba wengi wao wanajiumiza.

Mada yangu inalenga hakimiliki. Kwamba wanamuziki hao wako mbali na sheria ya hakimiliki. Mzee wa Busati si mpenzi sana wa muziki wa kizazi kipya lakini mara kwa mara unapenya kwenye masikio yake.

Huwezi kuukwepa. Ukipanda kwenye daladala, kondakta na dereva wake ni wa kizazi kipya. Unategemea atakuwekea vibwagizo vya Msondo Ngoma?

Anyway tuachane na hayo. Kinachosemwa na Mzee wa Busati ni kwamba wasanii hawa wa kizazi kipya wamekalia bomu. Bomu ambalo likija lipuka itakuwa balaa.

Mwandika Busati ameshasikiliza nyimbo ambazo kwa hakika ni za wizi kwa wasanii wa ng’ambo. Marekani na Ulaya. Tungo hizi si zenu wajameni acheni wizi.

Hii midundo mingi katika nyimbo zenu si kazi za mikono yenu. Mnakwiba kupitia utundu wa kompyuta. Je, huu ndio utandawazi? Bila shaka huu ni ujambazi wa wazi.

Mwasema mna vipaji? Hapa ni kudanganyana. Kama mtaendelea kusisitiza kwamba mna vipaji basi ni ‘karama’ za kupanga kazi za wizi kama mnavyofanya.

Na ndio maana wengi wenu hamtaki kwenda kusajili kazi zenu COSOTA. Mnahofu kwamba leo hii umesajili wimbo wenye midundo ya wimbo wa Beyonce Knowles mwenye umiliki halali akisikia hali itakuwaje? Hali hii ndiyo inayowafanya mkae mafichoni.

Lakini yawezekana hamjui madhara yake. Ipo siku mtafurushwa na wenye midundo yao. Sasa hiyo albamu yako inayomvimbisha tumbo msambazaji nawe ukabaki hohe hahe itaweza kulipa fidia?

Waambieni hao wanaojiita maproduza kwamba hiyo tabia ya kuiba midundo ya muziki kutoka nje ni mbaya kwani inawaharibia safari yenu kuelekea katika mafanikio.

Hamtakuwa na ubavu wa kuuza tungo zenu nje ya Tanzania. Hamtathubutu kwa sababu mwajua wazi kuwa huko ughaibuni mtanaswa.

Mtaendelea kupiga miayo na kukimbizana kwenye foleni ya chips dume. Yawezekana mmekubali kwamba mwana wa mbuzi kamba ni yake.

Mmekubali kwamba nyie umasikini ni wenu. Utajiri mko mbali nao kama ilivyo ardhi na mbingu. Mwasubiri kutoa singo ya mapenzi na kufanya uzinduzi mikoani. Kwisha habari!

Haya ndiyo maisha mliyoamua kuwa nayo. Maisha ya hofu. Maisha ya kutothubutu kuuza nyimbo zenu nje ya nchi. Sana sana mtaishia kwa Mzee Kibaki au kwa Museveni.

Siku Mzee wa Busati akiamua kuimba mtakoma ubishi. Hatasubiri midundo ya kompyuta. Atakwenda studio na gitaa lake na zumari kwapani. Halafu tupimane ubavu ni nani mwanamuziki halisi?

Tupate kujua nani hasa aitwe supa staa. Huyu anayesubiri kuiba midundo ya muziki kutoka ughaibuni au huyu anayepiga gitaa lake na marimba?

Hivi mwawezaji kujiita wanamuziki wakati hamjui hata namna ya kushika gitaa achilia mbali filimbi. Acheni ubabaishaji la sivyo mtawenda na maji.

Huu ndio ukomo wa Mzee wa Busati kwa wiki hii ambayo bado mazungumzo ni juu ya Taifa Stars na safari yao ya Burkina Faso. Twazidi kupiga dua njema ili tukaione Ghana.

Wasalaam,

No comments: