Monday, September 3, 2007

Mwisho wa jitimai Jangwani

na innocent munyuku

MAMBO shwari kwa Yanga baada ya kufanikiwa kuinywa Tusker jijini Mwanza hivi karibuni. Kombe ni lao na bila shaka sasa wanatembea kwa matao wakitamba wawezavyo.

Utawaambia nini kwa sasa? Midomo i wazi kwa furaha iso kifani. Hali ndivyo ilivyo kwani kwa miaka kama minne hivi walikuwa wakiishia kuliona kwa mbali kombe hilo.

Pilau imeshaliwa na soda za kushushia zimejaza matumbo yao kwani kubeba kombe hilo halikuwa jambo rahisi. Kipute kilijaa upinzani mkali.

Zile enzi za jitimai sasa zimekoma, hakuna tena majonzi Jangwani ni nderemo. Husemwa kuwa jitimai ni huzuni, hali ya kukosa furaha. Sasa mambo ni safi, wamesahau uchungu wa kulikosa Kombe la Ligi Kuu Tanzania Bara.

Sasa hawa pengine wanaweza kuitwa majagina au majabari yaliweza kuutafuna mfupa ulioishinda Simba ambayo tangu awali walitangaza kujitoa katika mashindano hayo.

Simba waliamua kuachana na michuano hiyo kwa kile kilichoelezwa kuwa kutoridhika na kiwango cha fedha kwa ajili ya ushiriki wa mashindano hayo.

Ni halali yao na kimsingi Simba walikuwa na haki ya kufanya hivyo kwani wenye kuingia gharama ni wao pindi mambo yanapokwenda upogo.

Kwamba kama wachezaji wangelazimika kulala njaa au kupata mlo mmoja hafifu kwa siku lawama zingekwenda kwa uongozi wa Simba moja kwa moja na si kwa waandaaji wa mashindano hayo.

Hoja ya Mzee wa Busati leo imelalia katika Kombe la Tusker msimu ujao kwamba kujitoa kwa Simba katika mashindano hayo kisichukuliwe kuwa ni jambo la kubezwa.

Ujengwe mtandao miongoni mwa timu bora za soka nchini kwa ajili ya kupata neema badala ya kutumika kutangaza bidhaa za wengine kwa njia iliyo rahisi.

Mtaani kwa Mzee wa Busati kuna mengi yamesemwa juu ya kujitoa kwa Simba katika kinyang’anyiro cha Tusker. Kwamba Wekundu wa Msimbazi walikuwa wanaiogopa Yanga.

Kinachosemwa ni kuwa mara baada ya Yanga kupokwa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Simba, Wanajangwani hao wakawa katika mbio za kusaka pahala pa kulipa kisasi.

Huenda kuna ukweli ndani yake. Lakini Mwenye Busati hawezi kujua ukweli u wapi? Anachoelewa ni kwamba kulikuwa na haja katika hilo kuungana ili timu ziwe na masilahi mazuri.

Mwandika Busati haandiki kuzilaumu timu zilizoshiriki Kombe la Tusker la hasha! Anachosema kwamba wakati mwingine ipo haja ya kuungana katika mambo ya msingi yanayohusu ujenzi wa klabu na soka kwa ujumla wake.

Kuendelea kujirahisi hakutakuwa na maana kwa maslahi ya soka nchini Tanzania. Na ndio maana ikajengwa hoja hapo juu kwamba kwa msimu ujao haya mambo yaangaliwe kwa kina ili kuondoa.

Huo ni mtazamo wa Mzee wa Busati na wala si hitimisho la mawazo. Wenye akili zao wanao uhuru wa kuweka wazi fikra zao kwani kwa kufanya hivyo soka ya Tanzania itasonga mbele.

Mwandika Busati anaishia ukingoni lakini hawezi kuondoka hivi hivi pasipo kugusia jambo jingine japo kwa ufupi. Anaiacha safu hii kwa kuwapa salamu vigoli walio kwenye maandalizi ya kumsaka kisura bora wa Tanzania siku chache zijazo.

Salamu zake ni kwa waandaaji. Kwamba hizi hitilafu zinazojitokeza katika mashindano zifike ukomo. Hivi karibuni imesikika kuwa mrembo fulani kutoka Arusha si wa Bongo.

Magazeti yakaweka wazi kuwa kimwana huyo ambaye pia alipata ajira njema katika kampuni moja jijini humo ni raia wa Kenya. Hapo ndipo palipoleta mshangao kwa walio wengi.

Kwamba iweje mgeni kutoka nje aje kushiriki mashindano ya raia hapa kwa Wadanganyika? Tatizo li wapi?

Kuna ulazima kwa waratibu wa mashindano hayo kuwa makini katika maandalizi yao. Isije siku akatangazwa Miss Tanzania mwenye uraia wa Bosnia.

Huku kuangaliana usoni pasipo kujiridhisha na uhalali wa mtu kuishi nchini kutaliponza taifa katika sekta nyingi na si katika urembo tu.

Vinginevyo kila la heri warembo kwa maandalizi ya kuwania taji la taifa. Endeleeni kunoa viuno vyenu ili wenye mapenzi mema wapate kukenua meno kwa vicheko.

Wasalaam,

No comments: