Tuesday, September 18, 2007

Dk. Wilson: Shahada si hoja bali juhudi na maarifa (1)

Na Innocent Munyuku

KICHWA chake kimependezeshwa kwa nywele za kahawia na ukiangalia kwa umakini zimechanganyika na mvi. Ni mcheshi mwenye kumbukumbu nyingi pia.

Huyo ni Dk. Eddie Wilson (70) ambaye kwa miaka zaidi ya 32 yuko nchini akiwa mmoja wa wanataaluma waliobobea wakitoa mafunzo kwa wanafunzi vyuoni.

Amepata kuwa mhadhiri katika Chuo cha Uongozi na Maendeleo (IDM) ambacho sasa ni Chuo Kikuu cha Mzumbe kilichopo Morogoro.

Alistaafu miaka michache nyuma kabla ya kuitwa tena mwaka jana kwa mkataba maalumu kuwa mhadhiri wa wanafunzi wa shahada ya uzamili na uzamivu katika kampasi hiyo jijini Dar es Salaam akifundisha sayansi ya jamii.



Dk. Wilson ni mzaliwa wa Marekani aliyeamua kuchukua uraia wa Tanzania daima amekuwa akisisitiza kuwa kumwita yeye kuwa ni Mmarekani Mweusi si jambo linalopendeza na badala yake aitwe Mtanzania.

Katika mahojiano maalumu na MTANZANIA Jumapili wiki hii, Dk. Wilson anazungumzia mengi lakini kubwa ni suala la umasikini kwa nchi za Afrika na katika hili anaizungumzia zaidi Tanzania.

“Kusema kwamba sisi Watanzania ni masikini sidhani kama ni sahihi, kuna mengi yamejificha hapa.

“Watu wengi hapa pamoja na kwamba ni wakarimu, wamejenga tabia ya ajabu kidogo utakuta mtu anaomba pasipo kufanya kazi.

“Lakini kibaya ni kwamba wengi wao wanajiona kuwa wako daraja la pili siku zote na kwamba daraja la kwanza ni maalumu kwa watu fulani. Kwa hiyo hii maana yake ni kuwa hawathubutu.
“Siku hizi tunalalamika hapa kwetu kwamba ubinafsishaji ni mbaya. Hilo laweza kuwa sawa kwani ni maoni ya mtu.

“Mimi nadhani kusema kuwa ubinafsishaji ni mbaya tunakosea kabisa. Sasa hivi tuko katika mageuzi ya kidunia na Tanzania kama nchi ndani ya sayari hii haiwezi kukwepa utandawazi,” anasema Dk. Wilson.

Anaongeza: “La maana hapa tuangalie namna ubinafsishaji wa mashirika unavyokwenda, tuangalie wawekezaji wanaopewa nafasi je, wanastahili?

“Kwa mtazamo wangu naona watu wameamua kuulaani ubinafsishaji kwa sababu pengine njia za kuhalalisha hayo mambo hazikuwa sahihi.

“Na ndio maana najiuliza kama kweli tunaelewa maana halisi ya ubinafsishaji. Jambo hili halina maana kwamba watu kutoka nje waje na kuchukua mali na kutuacha masikini si hivyo.”

Dk. Wilson anasema kitu cha muhimu kinachoweza kufanywa ni kuweka mazingira katika uwazi hasa mikataba. Kwamba wananchi wanayo haki ya kujua rasilimali zao zinawanufaishaje.

Anasema kama raia wa kawaida haelewi ananufaika vipi basi atakuwa wa kwanza kuhubiri kwamba uwekezaji au ubinafsishaji haufai.

Lakini pia anaeleza kuwa kuna ulazima wa kuwapa nafasi Watanzania kuwekeza katika maeneo yao na hivyo kutoa fursa nyingi za ajira.

“Wako wafanyabiashara wenye uwezo na zipo sekta ambazo wanazimudu kwa hiyo tuwape nafasi kwanza hawa tuone.”

Vipi kuhusu mwamko wa vijana katika kuliendeleza taifa?

Katika eneo hilo Dk. Wilson anasema kuna kikwazo nchini hasa linapokuja suala la vijana kujali taifa lao.

“Wakati mimi nakuja Afrika, nilifurahia sana Tanzania kwa namna watu walivyokuwa Wazalendo. Ukikutana na mtu anasimama na kusema ‘mimi ni Mtanzania naipenda nchi yangu’ ilifurahisha sana.

“Lakini sasa kwa muda huu tulionao hali imebadilika watu hawajali hilo, wengi wameacha kujivunia nchi yao tofauti na zamani,” anasema Dk. Wilson.

Akielezea hilo, Dk. Wilson anasema huenda limechangiwa na vijana kukata tamaa na sasa wanaangalia namna ya kutoka nje ya mipaka.

Anasema suala la kuiacha nchi yao na kwenda kusaka neema sehemu nyingine si dhambi lakini usitoke nchini kwa kukata tamaa.

“Watu sasa wanasema juu ya ajira za Rais Jakaya Kikwete. Wengi wanaozungumza ni vijana wadogo wanasema hawazioni.

“Inawezekana ajira hazionekani lakini sidhani kama Rais anaweza kumpa kila mmoja kazi ya kufanya. Kikwete ni mtu mmoja hawezi kila jambo peke yake.

“Nadhani tumwache hadi 2010 atakuwa na nguvu ya kutupeleka pazuri. Tatizo hapa ni kwamba vijana wana haraka na hilo si dhambi ni mazoea ya jamii. Kila mahala kijana akitaka jambo basi lazima liwe leo leo.

“Kwa hiyo hata kama kijana akijenga wazo la kwenda Marekani afahamu kichwani mwake kuwa Marekani ya leo haikujengwa kwa siku moja, imechukua miaka mingi sana tuseme zaidi ya miaka 300. Si jambo rahisi.

“Na ndio maana nasisitiza kuwa vijana waipende nchi yao kabla ya kukimbia. Kuichukia nchi yako ni dhambi.

“Huwa nazunguka sehemu nyingi mjini nakutana na vijana ambao ni mahiri sana katika ususi, ushonaji na kutengeneza vitu vingi vya mapambo. Hawa hawakwenda shule lakini elimu yao ni kubwa.

“Kutokana na hilo mimi nadhani suala hapa si shahada nyingi kichwani bali kutumia maarifa yetu kujinasua katika umasikini.

“Bado niko na vijana na Watanzania kwa ujumla tuwe na mawazo chanya daima. Tusijidanganye kwamba tutapata neema kwa uharaka.

Lakini Dk. Wilson anasema hana budi kuonya kuwa kufanya kazi kwa bidii si jambo rahisi ni kitu mtu anadhamiria. Hii ni tabia ambayo wengine huzaliwa nayo na wengine husukumwa kuipenda.

“Kwa vile vijana ndio wanaotakiwa kuijenga nchi yao lazima wapewe elimu wajijue wao ni nani katika jamii. Wasiachwe hivi hivi.

“Ipo mifano kama Nyerere (Julius Nyerere Rais wa Kwanza wa Tanzania) au Nkrumah (Kwame Nkrumah Rais wa Kwanza wa Ghana) hawa hawakuzaliwa na kujua kama ni viongozi au watu maarufu.

“Walizaliwa kama watu wengine lakini kutokana na mafunzo wakajitambua wao ni kina nani na wanaweza kusisima wapi katika jamii,” anasema Dk. Wilson.

Dk. Wilson pamoja ucheshi wake jambo moja ambalo unaweza kumchefua akatapika kahawa yake yenye maziwa ni iwapo ana mpango wa kurejea Marekani.

“Unaniuliza ni lini nitarudi kwetu? Hebu acha kuninyanyapaa,” anasema na kisha kuongeza: “Kwangu ni hapa, mimi kuzaliwa Marekani lisiwe jambo la kuniona kuwa sistahili kuwapo hapa.

“Nimezaliwa Marekani lakini historia inajieleza wazi mimi nimetoka Afrika kwa hiyo ni Mwafrika na Tanzania iko Afrika.

“Ngoja nikwambie kitu,” anasema kwa kicheko na kisha kuongeza: “Nina makazi yangu Morogoro eneo la Mazimbu na tayari nimeshapanga kaburi langu likae wapi.”

No comments: