Na Innocent Munyuku
ALHAMISI wiki hii nilikuwa na mambo ambayo yalitakiwa yawe yamemalizika kabla ya jana Jumamosi. Ni mengi mno siwezi kuyataja yote pengine niseme moja.
Nilikuwa na ahadi ya kuzuru Active Studio kuangalia maendeleo ya mpango maalumu wa kukuza na kuviendeleza vipaji vya wasanii wa muziki wa reggae nchini.
Ninapowasili katika studio hizo nakutana na mwanamuziki anayesifika kwa tungo zake zenye mafunzo mengi kwa jamii. Huyu ni Vitali Maembe. Alikuwa akiagana na meneja wake Gotta Warioba.
Gotta ambaye pia ni mmoja wa wamiliki wa studio hiyo, ananikaribisha kwa ‘mahubiri’ mengi yenye utani. “Tumekaa hapa tunazungumza na Maembe karibu saa moja na nusu…tunashindwa kuachana.”
Kauli hiyo ya Gotta hainishangazi sana kwani nafahamu umoja wa hawa wawili. Mbali na kuwa makini katika kazi ni marafiki mno na urafiki wao unajengwa na msingi wa umakini wa mambo yao mengi wanayoyapanga. Ndimi zao zinateta amani, umoja na mshikamano.
Maembe anaondoka na kupisha mazungumzo baina yangu na Gotta. Kikubwa kinachozungumzwa ni mpango mpya wa kuendeleza vipaji kwa wasanii wa muziki wa reggae.
“Mambo yameiva tumewakusanya wanamuziki wengi wa reggae na wamefanya mambo makubwa. Tayari tuna albamu iitwayo Bongo Riddims and Style (I) yenye nyimbo 12,” anasema Gotta.
Gotta anawataja wanamuziki walioshiriki katika albamu hiyo kuwa ni Ras Mizizi, Fatma, Drez Chief, Saganda, Pestman, Hardman, Phantom, Carola Kinasha, Ngwandumi, Zanzibar, Chalo na Daxwise.
Kikubwa kinachosemwa katika tenzi za wanamuziki hao ni mawasiliano mema kwa jamii, stadi za maisha, mapenzi na athari za mifarakano au kutokubali mapenzi ya Mwenyezi Mungu.
Kwa mfano Ras Mizizi katika wimbo wake wa Waafrika anasema, watu wa bara la Afrika wamejiharibu, wamepagawa kwa kuacha mambo yao mengi yenye maana na kufuata mikondo isiyofaa.
Anasema juu ya wanaume wanavyowaharibu watoto wadogo kwa kuwanajisi. Wanaume kwa wanaume kuishi pamoja kama wanandoa hali kadhalika kwa wanawake.
Ras Mizizi kwa hisia anaelezea kero nyingi katika maendeleo ya bara la Afrika kwamba Waafrika wengi wamepotoka na ni kama hawajui njia sahihi.
Ni albamu yenye kila aina ya uhondo kutokana na ukweli kwamba kila aliyeingia humo amejaribu kwa kuelimisha, kukosoa na kuiburudisha jamii kwa namna ya kipekee.
Zungumzia mkorogo kwa mfano, mwimbaji Carola Kinasha kupitia kibao chake cha Rangi anashangaa kuona watu weusi hasa kina dada wakihangaika kubadilisha rangi za ngozi zao kwa kutumia vipodozi.
Carola anasema haoni kwanini wanawake wahangaike kubadili rangi zao wakati Mungu kawapa rangi njema ya asili yenye kila sababu ya kujivunia.
Pestman naye hayuko nyuma. Huyu anaimba juu ya sala kwa Mwenyezi Mungu katika kibao chake cha Kneel & Pray. Anasema zunguka kila mahala, fanya lolote lakini si vema kumsahau Mungu.
Anawaasa watu kujenga tabia njema ya kumkumbuka Mungu katika pilika zao za kila siku na kwamba kwa njia hiyo mambo yatanyooka.
Fatma anaimba juu ya kurejea kwa mpango wake wa kurejea kwa mwenza wake wa kale. Si yeye bali maneno kwa mashabiki wake kupitia wimbo wa Narudi Kwako ambao nao ni moto wa kuotea mbali.
Anachoimba Fatma katika kibao chake hicho ni mapenzi kama vile alivyofanya Saganda kwenye wimbo wa Sema Kidogo na Gwandumi katika kibao chake cha Mtarajiwa. Drez Chief naye kachombeza mapenzi katika wimbo wake wa Kishtobe.
Bongo Riddims and Style iliyoandaliwa chini ya Umoja Records ina mengi ya kujifunza. Hakuna kundi la jamii lililotengwa katika tungo zake hizo.
Vijana wanaoishi ghetto wamekumbukwa na kupewa nasaha na msanii Phantom kwenye wimbo wake wa Ghetto Yut.
Anasema ipo siku vijana hao wataibuka na kwamba hawana haja ya kukata tamaa kwa muda huu. Wasali na kufanya kazi kwa bidii na kama kila mmoja atatimiza wajibu wake basi mema watayaona.
Lakini je, mkakati huu wa reggae wa Umoja Records unalenga nini?
Mratibu wa mpango huo, Gotta Warioba anaweka wazi kuwa nia ni kuutangaza muziki huo na kukuza vipaji kwa wasanii nchini na Afrika Mashariki kwa ujumla.
“Hatuko kibiashara sana na ndio maana nasita kusema kwamba tunaingia sokoni lini. Lengo letu ni kuukuza huu muziki,” anasema Gotta na kisha kuongeza:
“Baadhi ya nyimbo zimeshaanza kupigwa katika vituo mbalimbali vya redio nchini.”
Bongo Riddims & Style ni mradi maalumu uliobuniwa kwa pamoja kati ya Umoja Records na Activeaudio studio.
“Lengo ni kuwasaidia vijana wakuze vipaji vyao katika mazingira wanayoishi,” anasema Gotta.
Hawaishii kukuza vipaji tu bali pia wamekwenda zaidi ya hapo kwa kutengeneza sauti za muziki kwa ubunifu wa hali ya juu.
Wakali hao wanaokesha studio kutengeneza muziki ni Dj Shaki na Backstage wakishirikiana na Tony ambaye ni mtaalamu katika ubunifu katika kazi za usanifu.
Katika mradi huo wanashirikiana pia na wadau wa muziki kutoka Nairobi, Arusha, London, Amsterdam na Kingston.
Monday, September 3, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment