Monday, September 3, 2007

Msimpige ngwara Rais Kikwete

na innocent munyuku

TASAUFI husemwa kuwa ni elimu imtakasayo mtu na mambo ya kidunia na kujishughulisha zaidi na masuala ya kidini. Pengine huitwa tasaufu.

Kwamba kama mtu alikuwa na kawaida ya kugida ulabu kuanzia alfajiri hadi mwachweo basi ataachana na habari hiyo hali kadhalika kwa wazinzi, wezi na watenda maovu wengine.

Wajuzi na wachambuzi wa mambo ya dini husema pia kuwa katika eneo lililo gumu kwa wanadamu walio wengi ni elimu hiyo ya tasaufi. Mabadiliko huwa magumu kiasi kwamba wengine huishia kurejea kwenye shimo la kale.

Mzee wa Busati ameishikilia tasaufi kwa juma la leo baada ya Rais Jakaya Kikwete kuzindua kampeni ya kupima virusi vya ukimwi kwa nchi nzima Jumamosi iliyopita.

Alichosema Rais Kikwete katika hotuba yake ya uzinduzi ni kwamba upimaji huo ni wa hiari lakini akawasihi Watanzania kujitokeza kwa wingi kwani Tanzania isiyo na ukimwi inawezekana.

Mwenye Busati alikuwa akifuatilia tukio hilo lililofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja Darisalama, kupitia luninga na akashuhudia Mkuu wa Kaya kutoka kwenye Jumba Jeupe akipima virusi pamoja na mama watoto wake.

Kwa Mwandika Busati hilo likawa tukio lililomkuna kwani kwa kawaida wananchi huiga mambo ya viongozi wao. Kama padri atakuwa cha pombe unategemea waumini nao waache kuharibu bongo zao kwa ulevi? La hasha!

Lakini kuna jambo moja ambalo linampa shida kidogo juu ya utaratibu wa kueneza kile kilichofanywa na mkuu wa nchi.

Mzee wa Busati anaamini kuwa katika kufikisha ujumbe kwa wananchi wengine hakuna shaka kwamba wasanii watatumika kwa kiwango kikubwa kuwahabarisha raia juu ya umuhimu wa kujua afya zao.

Je, wasanii hawa wataleta tungo zipi au maonyesho gani kwa ajili ya kufikisha ujumbe wao? Wataendelea kutuimbia nyimbo za kujisifu kwa mavazi na kuchukuliana wachumba kama ishara ya ujanja?

Hofu ya Mzee wa Busati ni hiyo kwamba hawa wasanii hasa waimbaji na watunzi hawatakuwa na kipya zaidi ya kuleta kichefuchefu kwenye tungo zao. Wamezoea kuimba uozo na kutajana majina kwenye nyimbo zao. Kwa ujumla hakuna ujumbe mzuri katika tungo nyingi.

Angalia video zao uone namna wanavyoharibu jamii. Hawa ndio wasanii tunaowategemea kupeleka ujumbe kwa wananchi?

Katika video hizo kinachoshuhudiwa na watazamaji ni uozo, uchafu na wakati mwingine ulimbukeni wa waandaaji wa kazi hiyo. Hakuna elimu inayofaa kwa jamii ya Watanzania.

Wanenguaji kwa mfano ambao mara nyingi ni kina dada, mavazi yao si ya kuyaonyesha mbele ya hadhara. Sehemu kubwa ya miili yao i wazi hakuna shaka kwamba kwa jamii hii ya kwetu hali hiyo inachochea wanaume wanaoangalia kufikiria ngono.

Hatuwezi kuhubiri kuachana na matumizi ya bangi wakati tukiendelea kupalilia miche shambani. Hatuwezi kuhubiri juu ya kuachana na gongo wakati viwanda vyake tunaviwekea ulinzi huko mafichoni. Huu utakuwa wendawazimu.

Kwa mlio na mipini ya sanaa sikieni. Kama kazi yenu ni kuhabarisha Watanzania juu ya athari za ukimwi basi enendeni katika njia mpya. Badilikeni katika uwasilishaji wa mada zenu.

Kama mwanena juu ya athari za ukimwi basi onyesheni kwa vitendo na si kushika vipaza sauti huku mkionyesha maungo yenu.

Mwakemea ukimwi huku tungo zenu zikisifia uzinzi na mauno ya kina dada? Huku ni sawa na kuwachokoza nyuki kwenye mzinga. Mwategemea nini?

Tusiufanyie mzaha ugonjwa huu wa ukimwi kwani umeshaharibu mengi katika jamii. Waangalieni watoto yatima wanavyoteseka, kaya zimeyumba, wengi wamepoteza matumaini kwa sababu ya ugonjwa huu.

Kama dhamira ni kuifanya Tanzania isiwe na ukimwi basi wasambazaji wa ujumbe wawe makini katika jukumu hilo. Tusiteme mate kushoto na kufukia kulia.

Huu si wakati kucheza michezo isiyo na faida kwa Watanzania. Tuungane na Rais Kikwete kwa nia ya dhati ya kuutokomeza ukimwi kwani ni doa kubwa katika maendeleo ya taifa.

Itashangaza kuona kwamba wenye kupiga zumari la kuutokomeza ukimwi watakuwa wakifanya ndivyo sivyo. Msiige hadithi za kale eti iga nisemacho na si nilitendalo. Kauli ziendane na matendo.

Kutakuwa na faida gani basi kama mtaimba habari njema za kuulaani ukimwi huku mkiwa uchi jukwaani? Hivi kweli ujumbe utaingia kwenye akili ya msikilizaji?

Hima tuikumbatie tasaufi kwa maslahi ya kaya zetu na vitegemezi vijavyo. Tunakwisha na tusipoangalia wageni watakuja kuijaza nchi miaka michache ijayo.

Hakika watakuja kwani ardhi itabaki tupu. Wageni kutoka Ulaya na kwingineko safari hii hawatahitaji kutumia peremende au bunduki kuitawala Afrika. Wataingia kwenye mahame kwani tutakuwa sote tumemezwa na ukimwi. Tujihadhari tusifike huko.

Mzee wa Busati anafikia ukomo kwa leo akiamini kuwa alichonena kimeingia kwenye mtima. Tukiungana kwa dhati tutaumaliza ukimwi.
Wasalaam,

No comments: