Monday, September 3, 2007

Tunahitaji kina Mwamnyenyelwa watatu tu

na innocent munyuku

KAMA kuna taarifa iliyonifurahisha katika mwaka huu wa 2006, basi hii ya Watanzania kugoma kuhutubia kwa lugha ya Kiingereza huko Nairobi nchini Kenya imenikuna zaidi.

Niliposoma kwenye magazeti na mitandao mingine ya habari kwenye intaneti juu ya habari hiyo nilivutiwa mno kiasi cha kunilazimu nisake nafasi ya kuwapa pongezi Watanzania waliodiriki kuitetea lugha yao wakiwa ughaibuni.

Bila shaka msimamo wa aina hiyo uliotolewa na Watanzania hao kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Vijana wa Afrika umewafurahisha pia na raia wa nchi hii. Wenzetu hao waliweka msimamo kwamba hawatahutubia kwa lugha nyingine zaidi ya Kiswahili katika mkusanyiko huo wa zaidi ya vijana 100 kutoka nchi mbalimbali barani Afrika.

Katika mkutano huo, waandaaji walipanga uendeshwe kwa Kifaransa au Kiingereza jambo ambalo wajumbe kutoka Tanzania hawakukubaliana nalo.

Aliyeanza kuwashtua washiriki wengine ni Hassan Bumbuli ambaye aliweka wazi msimamo wake katika utambulisho kuwa hakuwa tayari kuitumia lugha ya Kifaransa au Kiingereza katika kutoa mada mkutanoni hapo.

Kwa heshima na taadhima, Bumbuli akawataka radhi wajumbe wengine na akaeleza kuwa kwa vile mkutano huo ni wa Pan Africans na pia unafanyika kwenye ardhi ya Afrika Mashariki ambako Kiswahili ni nyumbani kwake hakuona sababu ya msingi kutoa hoja zake kwa lugha nyingine tofauti na hiyo.

Naamini kwa dhati kuwa Bumbuli wakati anatoa msimamo wake huo alihitaji akili ya ziada kuweka hadharani kile anachoamini katika mtima wake. Kwamba uhodari aliouonyesha mbele ya hadhira ile ulitokana na uchungu na uzalendo wa kukiweka Kiswahili katika mstari wa mbele.

Gazeti la kila siku la Majira katika toleo lake la Novemba 3, 2006 lilimkariri Bumbuli akisema “Nitaomba mnisamehe kwani sitopenda kuzungumza Kiingereza wakati huu ni mkutano wa Waafrika na tayari kama Afrika tunayo lugha ambayo tunaitazamia kuwa ya pamoja ambayo ni Kiswahili.

“Sasa mimi nitazungumza Kiswahili na lazima niwaeleze kwamba nimesikitishwa sana na waandaaji wa mkutano huu kuchagua lugha mbili tena za Wazungu kuwa ndizo lugha za kujadili hisia zetu Waafrika.”

Kutokana na msimamo huo, waandaaji wakaahidi kumweka mkalimani lakini kwa sababu ambazo hazikusemwa, mkalimani huyo hakuwekwa. Inawezekana walidhani kuwa nguvu ya Bumbuli ingeyeyuka kama povu la sabuni kwenye upepo wa jangwani.

Ikaja zamu ya mwakilishi mwingine kutoka Tanzania. Huyu ni Dadi Kombo aliyetakiwa kutoa mada ya Ushiriki wa Vijana katika Siasa. Naye bila ajizi akaanza kutoa mada kwa Kiswahili na hata juhudi za kumtaka abadili lugha hazikuzaa matunda. Aliendelea kuteta kwa Kiswahili na hapo ikabidi mada yake iahirishwe.

Wakati wajumbe wakiendelea kutafakari msimamo huo, mjumbe mwingine wa Tanzania, Mgunga Mwa-Mnyenyelwa aliyetakiwa kutoa mada juu ya sanaa kwa vijana pia akasimama na kuwaeleza wajumbe wengine kuwa kamwe asingewasilisha mada yake kwa Kifaransa au Kiingereza na kwamba angetumia Kiswahili.

Mgunga akawauliza waandaaji kwamba iweje atumie lugha tofauti na Kiswahili wakati mkutano huo ni wa Waafrika? Akaongeza kuwa asingekuwa tayari kuungana na waandaji katika kukidharau Kiswahili.

“…Kwa nini tunadharau mambo yetu ya Kiafrika na kuthamini Wazungu? Kiswahili kina nguvu sana na ni lugha inayotumiwa na watu wengi sana katika ukanda huu wa Maziwa Makuu, tusipoipa thamani lugha yetu katika mambo kama haya je, tutaithamini wapi na lini?”

Kwa msumari huo wa Mwa-Mnyenyelwa, waandaaji hawakuwa na haja ya kupinga hoja ya Watanzania kutaka kutumia lugha yao ya Kiswahili katika mkutano huo na hapo ndipo wakalazimika kumweka mkalimani na mambo yakaenda sawia.

Sitasahau tukio hili lililofanywa na Watanzania hawa na kamwe sitafumba mdomo wangu au kuuzuia ulimi wangu kunena pongezi juu yao. Naam wanastahili pongezi kwa ushujaa wao tena wakiwa nje ya ardhi ya kuzaliwa.

Mpigania uhuru wa Afrika Kusini marehemu Steve Biko katika harakati zake dhidi ya siasa za ubaguzi wa rangi nchini humo alipata kusema kuwa kitendo cha kujitambua kuwa wewe ni Mwafrika tayari umeanza vita dhidi ya wadhalimu!

Biko ambaye mara nyingi alipenda kujitambulisha kuwa ni Bantu Steve Biko alikuwa na kauli nyingine za hamasa juu ya kujitambua na kupigania kilicho chako. Katika hili alikuwa wazi kutamka katika mikutano yake kuwa mtu Mweupe hakuna maana kwamba wewe ni bora kuliko Mweusi hali kadhalika kuwa Mweusi hakuhalalilishi kuwa duni mbele ya mtu Mweupe.

Mwa-Mnyenyelewa na kundi lake wamejiweka katika mstari wa kupigania kilicho chao na kwa hakika wanapaswa kuwa miongoni mwa Watanzania wa kuigwa katika kukitetea Kiswahili ndani na nje ya nchi. Kwamba usipothamini chako si rahisi mtu mwingine akithamini.

Tumejikana vya kutosha katika miaka mingi, tukisahau mema ya kwetu. Tumejipunja uhuru wa nafsi kwa siku tele zilizopita. Ingawa maelfu wangali wakikana vya kwao, huu uwe mwanzo au mwendelezo wa vita dhidi ya wanaotaka kufifisha mila na utamaduni wetu. Huu ni wakati wa kujitambua kwa dhati kabisa na kukana ulofa na utumwa wa akili wa kukumbatia kila kitu kutoka ughaibuni. Kiswahili ni chetu hivyo lazima tujenge umoja katika kukitetea na kuhakikisha kuwa lugha hii inapanuka.

Kilichofanywa na Watanzania jijini Nairobi ni kuwakumbusha baadhi ya Watanzania ambao binafsi nawaita waasi ambao kazi yao ni kuthamini kila kitu kutoka nje ya mipaka yao. Hawa ni wale waliosahau lugha yao, hawataki pia mavazi achilia mbali vyakula vyenye asili ya Kiafrika. Hawa wamejaa tele!

Nimekuwa shuhuda na msikivu makini wa vioja vya lugha mitaani. Utakuta mtu Mzungu anajaribu kuwasiliana na Mtanzania kwa lugha ya Kiswahili lakini ajabu ya Mungu ni kuwa Mweusi huyo badala ya kuzungumza Kiswahili atapinda na kumjibu Kiingereza. Kwa mtazamo wangu Mtanzania wa aina hii hana na tofauti na askari anayewaua wenzake katika mapambano vitani.

Vita ya kukitetea Kiswahili wasiachiwe kina Mgunga pekee, Watanzania wote tushiriki na bila shaka hata waasisi wa taifa hili wazima kwa wafu watakuwa na furaha kuona kuwa lugha yetu imewaunganisha Waafrika na hapo ndipo mshikamano na umoja wa kweli wa Afrika huru utakapokuwa na maana pana. Afrika moja lugha moja! Kila jambo linawezekana katika uso wa dunia, ni suala la kuthubutu.

Ndio maana nasema twahitaji kina Mwa-Mnyenyelwa, Bumbuli na Kombo wengine ili kufanikisha vita hii mbele yetu.

Lakini kwa upande mwingine huu ni mwanzo tu wa vita ngumu iliyo ndani ya damu ya Waafrika katika kujivunia mambo yao ya asili. Kwamba tukimaliza ya Kiswahili twende kwenye majina yetu ya asili. Badala ya Innocent tujiite Navali, badala ya Charles tujiite Nangomo, badala ya Alfred tujiite Nandule.

Tusione soni kujiita Tuhwachi na kamwe tusiyafumbie macho majina kama Andulile, Anyimike au Nkungu. Haya ni ya kwetu na tusitarajie kuwa kina Smith kutoka Uingereza watayatangaza majina haya. Wataendelea kuyaita ya kishenzi!

No comments: