Monday, September 3, 2007

Ni watani au ‘wachawi’ wa jadi?

na innocent munyuku

KWA miaka mingi sasa, unapozungumzia upinzani wa soka nchini Tanzania, mashabiki wengi wa mchezo huo hawasiti kuzitaja timu za Simba na Yanga kuwa zenye upinzani wa kweli. Hawaishii hapo watasema pia kuwa timu hizo zina utani wa jadi.

Wanasema hivyo kutokana na historia ya timu hizo kongwe nchini kwamba kila zinapokutana kama si mmoja kufungwa basi hutoka sare ya mabao ama suluhu na kuna wakati moja ya timu hulazimika kuweka mpira kwapani.

Kwa Simba na Yanga mambo kama hayo ni ya kawaida. Kwamba si ajabu kusikia moja ya timu kati ya hizo ikitangaza kutoingiza timu uwanjani kwa sababu fulani na kweli ikafanya hivyo au wakati mwingine huwa ni tishio na wenyewe hudai kuwa ni moja ya mbinu katika soka.

Timu hizo mbili kila zinapojiandaa kukutana katika mashindano mbalimba iwe Ligi Kuu au michuano ya kuwania vikombe vingine, mashabiki wa pande zote mbili huingia mchecheto wa hali ya juu lakini kubwa ni kwamba majigambo hutawala wakati huo wa maandalizi.

Hata hivyo, homa ya maandalizi ambayo mashabiki wa Simba na Yanga wanakuwa nayo huambukizwa pia wachezaji wa timu mbili kwani kwa wakati huo hata wachezaji wa timu hizo huwa kwenye wakati mgumu. Katika miaka ya hivi karibuni ambako kuna teknolojia ya simu za mikononi, wachezaji hao kunyang’anywa simu zao mikononi ni jambo la kawaida.

Wanaoendesha utaratibu huo ni viongozi wa timu hizo na kama si hao basi ni wanachama watiifu wa klabu hizo ambao kimsingi hawapingwi katika utekelezaji wa kazi zao. Lakini kinachofanyika hapa ni kulinda maslahi ya klabu isihujumiwe na mpinzani.

Ipo minong’ono pia kuwa kuna wakati fulani wachezaji hulazimika kulala makaburi au kupakwa dawa za jadi zitakazowasaidia kuwa imara uwanjani. Kwa ujumla wakati wa kuelekea mechi za Simba na Yanga kila jambo husemwa ili mradi kuwa katika porojo za maandalizi ya mechi.

Lakini jambo moja ambalo liko wazi ni kwamba kinachoangaliwa katika mechi ya Simba na Yanga ni kujijengea heshima kwa mashabiki wake. Hakuna anayekubali kuchekwa kwa kipigo uwanjani na hii ndio asili ya madoido yote hayo kabla ya mechi.

Hata zinapotoshana nguvu, mashabiki wa timu hizo hawakosi maneno kwenye ndimi zao. Watasema kila linaloonekana kuwa lafaa kuwa kejeli kwa wapinzani wao.

Mfano ni katika mechi ya Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Yanga wanadai Simba walikuwa na ‘mzigo mzito’ wa ndumba kutoka Bagamoyo huku wapinzani wakisema kuwa ‘uchawi’ wa kipa wa Yanga, Ivo Mapunda wa kubadilisha viatu uliwapa nguvu dimbani.

Kabla ya mechi hiyo, gazeti la Daily News katika ukurasa wake wa nyuma lilikuwa na habari kwamba mechi hiyo iligubikwa na uchawi wa hali ya juu. Katika habari hiyo, kuna picha zinawaonyesha watu wawili ambao hawakujulikana ni wa timu ipi wakiwa katika jitihada za kufukia vitu kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Ninapoyaangalia mambo kama haya yakiendelea kufanyika katika uso wa dunia kwa karne hii huwa naduwaa. Lakini kuduwaa kwangu si kwamba sina jawabu la hasha! Jibu lipo, nalo ni ufahamu kuwa jamii yetu haitaki mabadiliko hata kwa wakati huu ambao hatuhahitaji kuamini masuala ya ndumba katika soka.

Nani alishaona ndumba zikitembea wakati au kabla ya mechi kati ya Manchester United na Machester City huko Uingereza? Au ni nani atasimama na kunena kwamba ameshaiona Liverpool na Arsenal zikishindania uchawi kabla ya mechi yao?

Ninachotaka kusema ni kwamba suala la uchawi katika soka halina maana kwa soka ya Tanzania leo hii. Huu si muda wa kurusha manyonya ya kuku au kutupa pembe za ng’ombe uwanjani. Wachezaji hawana budi kufuata mafundisho ya makocha na hakuna haja ya kuendekeza imani za kishirikina katika soka.

Kwa mtindo huu mwadhani akina Gaudence Mwaikimba au Emmanuel Gabriel wataweza kung’ara ughaibuni? Watatamba vipi wakati walishazoea kuamini kuwa pasipo ndumba mpira hauchezeki? Sisemi kwamba kwamba hawa wawili ndio vinara wa ndumba bali timu zao zimekuwa zikionyesha hali ya ushirikina kabla ya mechi.

Kama kuna kiongozi kati ya timu hizo atasema hahusiki na mambo kama hayo, mbona hajawahi kujitokeza na kulaani mambo kama hayo? Ukweli ni kwamba imani kama hizo zimejengwa ndani ya klabu hizi na bila shaka na zingine zilizojaa hapa nchini.

Huu uwe wakati wa kusema hapana kwa mambo kama hayo. Nyakati za kuamini kuwa shuti kali halitalenga golini eti kwa sababu milingoti imemwagiwa maji ya maiti zimepitwa na wakati. Tuwaachie makocha wafanye kazi zao na wachezaji wawajibike kwa kufuata maelekezo uwanjani.

Ninapoona watu wanapoteza pesa kwa ajili ya ushirikina wa kujipatia ushindi uwanjani huwa nabaki mdomo wazi kwa kuwaonea huruma wahusika na hapo ndipo ninapoona kuwa Simba na Yanga si watani wa jadi bali ni ‘wachawi’ wa jadi.

Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni suala la kukimbiana limeanza kutoweka tofauti na miaka ya nyuma kama ilivyokuwa Novemba 26 mwaka 1966 pale Yanga ilipoondoka uwanjani zikiwa zimesalia dakika tatu mpira uishe.

Katika mechi hiyo mchezaji Awadh Gessani aligoma kutoka nje licha ya kuamriwa na mwamuzi Jimmy Waldon baada ya kumchezea rafu mchezaji wa Sunderland (Simba). Sunderland ilipewa ushindi wa mabao 2-0 huku nahodha wa Yanga, Mohammed Hussein Hassan ‘Msomali’ akifungiwa na FAT kucheza soka kwa miezi 12.

Lakini pia katika mechi ya Machi 30, 1968 mchezo uliishiia katika dakika ya 28 baada ya mshambuliaji wa Sunderland, Emmanuel Albert Mbele ‘Dubwi’ kumvamia mwamuzi Jumanne Salum. Yanga ilipewa ushindi.

Pia Machi 3, 1969 Sunderland haikutokea dimbani na hivyo kuipa ushindi Yanga huku Sunderland wakipigwa faini ya sh 500. Hata Machi 21 mwaka 1971, Sunderland iligoma kuendelea na mechi kunako dakika ya 70 kwa madai kuwa kipa wao John William Semainda aliumizwa. Mgomo kama huo ulitokea katika mechi ya Juni 18, 1972 wakati Yanga ikiongoza kwa bao 1-0 liliwekwa kimiani na Leonard Chitete.

Agosti 26 mwaka 1992, Yanga ilileta ‘jeuri’ kwa kutokubali kucheza na Simba kwa madai kuwa tayari ilishatwaa ubingwa. Mgomo waom huo uliwagharimu faini y ash 250,000

Hiyo ni mifano michache tu ya mambo ambayo timu hizo zimekuwa zikijihusisha nayo katika ulimwengu, masuala ambayo hayana mema kwa maslahi ya soka nchini.

Na ndio maana wakati mwingine nashawishika kusema kuwa Simba na Yanga ni makaburi ya wachezaji kutokana na vitendo vyao ambavyo havina misingi ya kuimarisha soka kwa wanasoka wake.

No comments: