Monday, September 3, 2007

Si makomandoo ni wazandiki hawa

na innocent munyuku

MWENDO mdundo. Husema vijana wa kisasa kwenye mazungumzo yao wakimaanisha kwamba harakati za maisha zinasonga mbele. Wengine husema hakuna kulala mpaka kieleweke.

Hao ni vijana wa kisasa wanaokua kwa nyama za kuku wa kompyuta na maziwa ya ng’ombe yanayonuka dawa za Kimagharibi.

Mzee wa Busati kama alivyoapa anaendelea kuwajibika kwenye safu yake kwa juma jingine lenye mchanganyiko wa furaha na huzuni.

Wiki ambayo sahiba zake wenye kushabikia watoto wa Jangwani wameinamisha vichwa chini wakitafakari kipigo kutoka kwa El Merriekh ya Sudan. Ni huzuni kubwa lakini neno la faraja ni kwamba hayo hayana budi kutokea katika ulimwengu wa soka.

Lakini kubwa lililomweka Mwandika Busati hapa leo si kujadili kipigo cha Yanga bali mtazamo mwingine wa makundi ya soka ambayo kwa miaka mingi yanaendelea kuua mchezo huo hapa kwetu bongoland.

Mzee wa Busati alishaacha kushabikia soka kwa kiwango kikubwa kama enzi zile. Siku hizi anapenda kukaa pembeni na masuala hayo kwa sababu yanapasua kichwa. Kila ukifungua kurasa za magazeti matatizo ni yale yale.

Sikiza redio au tumbua macho kwenye luninga nako utakutana na kero sugu ambazo ziko katika soka kwa miaka nenda rudi. Hakuna mabadiliko. Kama kuna mabadiliko basi ni ya wafadhili na wanasoka.

Kiasi cha majuma mawili yaliyopita Mzee wa Busati alisikia jambo lililomfanya achefuke rohoni. Ni juu ya jamaa mmoja kati ya wale wanaojiita makomandoo. Kwamba huko jijini Mwanza alitaka kumshikisha adabu mfadhili wa Yanga, Yusuf Manji. Kisa? Mfadhili huyo alinunua mechi dhidi ya El Merriekh na kwa hiyo hapakuwa na mtu wa ‘kuthibiti’ mapato mlangoni.

Husemwa kwamba kama mechi ina kiingilio jamaa hao hunufaika sana na mapato mlangoni. Humo watapata fedha za komoni au chimpuni kama si wanzuki.

Mzee wa Busati anaamini kuwa jamaa huyo alikuwa mwakilishi wa hao wanaojiita makomandoo katika klabu hiyo.

Habari hiyo ilikuwa kama porojo lakini yenye kuonyesha uhalisia wa mambo yalivyo katika maendeleo ya soka nchini. Wengi wamekaa kusubiria vya bure, hawana kazi nyingine.

Hao hawako Yanga tu, klabu ya Simba nako wamejaa tele wakipiga kelele ambazo zinaonekana kutokoma milele.

Suala la kuwaondoa laonekana kuwa gumu kama walivyo wapigadebe wa daladala na stendi kuu ya mabasi ya Ubungo. Wameganda na vigumu kuwabandua kwani mfumo uliopo unawalea hawa.

Lakini Mwenye Busati haoni sababu ya hawa kuendelea kuitwa makomandoo. Hakika hakuna haja hiyo kwa sababu kwa miaka tele hajaona kipi hasa kinachowahalalisha kuitwa makomandoo.

Ukamandoo wao juu ya nini? Je, ni juu ya uhodari wao wa kuiba mapato mlangoni? Ni kipi hasa kinawapa kofia hiyo?

Mzee wa Busati hana haja ya kuwa mwoga kutoa msimamo wake kwamba hawa si makomandoo bali ni wazandiki. Hawana jema katika maendeleo ya soka nchini.

Hawa ni wanafiki wachonganishi na ifike mahala wasikumbatiwe. Waondoke katika ramani ya soka kwani uzoefu unaonyesha kuwa wanaharibu kila jema.

Ni wazandiki kwa sababu wengi wao wanaongoza makundi ya maasi katika klabu husika. Iwe kwa Yanga au Simba. Hawa wanajali kula yao ya leo.

Kwa maana hiyo wanachoangalia ni maneno gani matamu ya kuwarubuni wenye nacho ili wapate kuufikisha mkono kinywani. Kwanini wasitimuliwe?

Kuwalea hawa mnaowaita makomandoo ni kulea uhuni ndani ya klabu za soka nchini. Kuwakumbatia hawa ni sawa na kufanya mapenzi yasiyo salama. Watupeni nje ya kapu au wabatizwe kwa maji mengi wapate kubadilika.

Wasalaam,

No comments: