na innocent munyuku
JANGWANI kilio, Msimbazi kicheko. Hii ni hali halisi baada ya watani wa jadi katika soka Simba na Yanga kumalizia kipute cha Ligi Ndogo juzi kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Wenye Simba yao sasa wanatembea kwa mbwembwe wakila upepo mwanana uliotokana na ushindi dhidi ya wapinzani wao.
Wamezidisha tambo, vifua navyo vi wazi wakitembea kwa matao kuliko hata twiga kule mwituni. Acha watambe kwani huu ni wakati wao.
Hapa kwa Mzee wa Busati mambo yanazidi kumwendea sawia. Hakuna matata kwani ngwenje ya viazi mbatata haipigi chenga na kaya nzima haijasahau neema itokanayo na shibe.
Leo hii Mwenye Busati hoja yake kuu ni kero iliyomwadhibu moyoni kwa siku tele. Kero hiyo sasa imehalalishwa na jamii kuwa msemo rasmi kwa watenda maovu.
Kwamba siku hizi mtu mbaya, tapeli, mtu wa hovyo kabisa ambaye pia ni mwongo huitwa msanii. Hakika jambo hili linakera mtima wa Mwandika Busati kwa kiwango cha hali ya juu.
Haijapata kusikika wasanii wakipaza sauti zao juu kukemea hali hii. Wengi wamekaa kimya na hata walioibuka kusema hawajaweka mkazo kuhusiana na tabia hiyo chafu.
Iweje sanaa itumike kama joho la waovu? Kwanini tapeli, laghai aitwe msanii? Kigezo kinachotumika hapa ni kipi? Huku ni kudhalilisha sanaa. Huku ni kuwatukana wasanii na mashabiki wake.
Mzee wa Busati ameamua kuinua midomo na kusema kwani mengine hayavumiliki. Kwanini basi hao waovu wasiite mawakili, madaktari au walimu?
Kwanini waovu wasiite maprofesa, mabaharia, marubani au wavuvi? Kitendo cha wasanii kugeuzwa kapu la maasi kinatia doa katika wigo huo. Twawafunda nini watoto wetu?
Kwa mtindo huu wa kuwaita waovu kuwa ni wasanii si ajabu hata vitegemezi vya Mzee wa Busati vikadharau sanaa katika siku zijazo. Hawatajishughulisha nayo kwa sababu tayari watakuwa wamelishwa mabaya na kuiona sanaa kuwa jambo la kishenzi.
Taifa litapoteza vipaji na kama vitaendelea kuwapo basi vitakuwa vyenye hali tete. Wengi hawataona fahari kuingia katika sanaa kwa sababu wameshafunzwa kuwa usanii ni kitu cha hovyo.
Nilitegemea Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) au vyama vingine vya sanaa vitoe tamko kukemea jambo hili. Nilitegemea wasanii wakae pamoja na kulaani falsafa hii.
Mzee wa Busati kwa bahati nzuri ni mpenzi wa sanaa za kila aina. Sanaa ni sehemu ya maisha yake. Sanaa ni ugali wake na furaha yake na kutokana na hilo hawezi kukaa pembeni. Lazima athubutu kupayuka kadiri awezavyo.
Kwa waraka huu, atafurahi kuona wasanii kwa umoja wao wanalaani falsafa ya kuuhusisha usanii na udhalimu, ufisadi au ushenzi wa aina yoyote. Huu ni msimamo wa Mzee wa Busati kama atabaki peke yake hatajutia dhamira yake atatumia njia nyinginezo kuhakikisha kuwa sanaa inabaki kuwa yenye heshima.
Kama yasemwa kwamba kuna baadhi ya wasanii ni wahuni mbona kwenye fani nyingine wahuni wapo? Nani atasimama na kusema kwamba hakuna wachumi wahuni? Nani mwenye kuthubutu na kutamka kwamba katika fani ya udaktari hakuna waovu?
Ajitokeze wa kusema kwamba kwenye ualimu hakuna waovu au hata kwenye sekta ya habari. Kila mwanadamu ana upungufu katika eneo lake. Hilo haliepukiki. Hivyo, kumtoa kafara msanii kuwa kioo cha uovu ni kutomtendea haki.
Kuihusisha sanaa na uhuni ni kuidhalilisha fani hiyo na watu wake. Ni kuwavunja moyo wanaotaka kutumbukia humo. Twawafifisha vipaji vyao wasiwe na uthubutu wa kusimama mbele ya hadhira na kutambia sanaa kama fani yenye heshima.
Mzee wa Busati kama alivyonena awali, jambo hili limechefua mtima wake kiasi cha kumfanya akaribie kutapika mbilimbi zake.
Kama wahusika au waathirika wataendelea kukaa kimya pasipo kuwakemea wanaochafua jina zuri na sanaa basi Mwenye Busati ataamini kwamba ipo namna.
Iweje mtu akuvue nguo nawe ubaki kumwangalia kama vile bahau? Mwavuliwa nguo pasipo upinzani tuwaeleweje wasanii?
Kama hili dogo lawashinda kulikemea ni nani basi kati yenu atumwe kuokoa jahazi la masilahi linalokwenda mrama? Nani atasimamia haki zenu kama mwashindwa kuwakemea wahuni wanaochafua maana halisi ya usanii?
Vinginevyo Mzee wa Busati amefikia tamati kwa juma hili na Jumanne hii anaweka tai yake vema kwani kaalikwa mahala fulani kutafuna vipapatio vya besidei bila shaka na vimiminika vyenye rangi ya dhahabu havitakosekana.
Lakini pia amalizie kwa nasaha kwa wana wa Jangwani kwamba kufungwa kwenu na Wekundu wa Msimbazi kusiwe njia ya kuwekeana mizengwe.
Hakuna haja ya kumsaka mchawi. Wenye macho wameuona mpira Morogoro. Kuleta chokochoko kwa wakati huu ni kujimaliza. Huko vijiweni wameshaanza kudai kuwa kuna mpango wa bakora Jangwani. Hakika msifikie huko kila mmoja aendelee na majukumu yake na kwa hakika Yanga imara inawezekana.
Wasalaam,
Monday, September 3, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment