na innocent munyuku
AKIWA na umri wa miaka 24 tu tayari alishakuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sehemu ya Mlimani akifundisha sanaa. Huyo ni Vicencia Shule ambaye Oktoba 14 mwaka huu alifanya mahojiano maalumu na RAI na kueleza mambo mbalimbali yanayohusu kumwezesha mwanamke kifikra.
Alipojiunga na masomo ya Chuo Kikuu Septemba mwaka 1999 akitokea Shule ya Mkwawa alishiriki kikamilifu katika harakati za kuwatetea wanawake katika mradi uliopewa jina la TUSEME chini ya Profesa Amandina Lihamba. Kuanzishwa kwa mradi kulitokana na hali ya jamii katika kuwakandamiza wanawake katika nyanja mbalimbali.
Kutokana na ukandamizwaji huo, idadi ya wasichana waliokuwa wakipata fursa ya elimu ilikuwa ndogo na waliobahatika kupata elimu ya sekondari wengi wao walishindwa kujiunga na vyuo vikuu kutokana na mfumo mbovu uliowafanya wasipate mwanya wa kufika huko.
Vicensia ambaye ni mchangamfu na mwenye kujiamini katika mazungumzo yake anasema mradi wa TUSEME ulimsaidia yeye binafsi kwani alipata nafasi ya kuendelea kujitambua.
“Lakini hatukuishia kupata elimu na kukaa nayo, baada ya kufundishwa uwezeshaji tukaenda katika shule mbalimbali na walengwa hasa ni watoto wa kike, lengo la huu mradi ni kumweka mtoto wa kike ajitambue,” anasema Vicensia.
Mradi huo ulioanza mwaka 1996 ulianza kuonyesha cheche zake katika shule za sekondari za wasichana za Kilakala, Songea, Korogwe, Msalato, Iringa na shule mchanganyiko ya Bagamoyo na Ruvu.
“Nathubutu kukueleza kuwa wasichana wengi ambao walifikiwa katika mradi huu ni wenye kujiamini katika jamii, hawako legelege kama wengine kwa sababu walifundishwa kujiamini na wana msimamo,” anaeleza.
Tangu wakati huo amekuwa akisimama msitari wa mbele kulinda na kutetea haki za wanawake na watoto na kuvunja ukuta uliowatenga na haki katika jamii.
Je, katika umri huo mdogo anawezaje kuhimili darasa ambalo pia lina watu wazima waliomzidi umri? Anasema kimsingi hajawahi kujenga hofu kwamba yuko mbele ya watu wazima au wanaume.
“Sijawahi kutishwa kwa sababu naamini ninachofundisha ndio moja ya msingi wao katika elimu na kama kuna wanaonidharau sijawahi pia kuwaona.
Pamoja na hilo, Vicensia anakerwa na tabia ya baadhi ya wasomi ambao kwa sasa akili zao zimehamia tumboni badala ya kichwani.
“Sasa hivi walio wengi wanafikiria kutoka tumboni, wanaogopa kuikosoa Serikali na hii imetokana na ukweli kwamba wameathiriwa na donors (wafadhili).
“Wanaogopa kukosoa kwa sababu ya hofu…hawa wanaogopa kama watakosoa watakosa pesa za wafadhili kutoka nje, miradi mbalimbali inapita tu bila kufanyiwa utafiti.
“Kinachoendelea hapa ni kuwalamba miguu wanaokupa pesa za kuendelea na miradi, ndio maana sasa wako kimya hawasemi kabisa.”
Anapozungumza uongozi wa awamu ya nne katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Vicensia anasema Rais Jakaya Kikwete amejitahidi kuwafanya watu warudishe imani kwa Serikali lakini hana budi kuwa makini zaidi na katika hilo asiwaamini sana watendaji wake.
“Sisemi kwamba Serikali zilizopita zilikuwa mbovu hapana. Ninachosema ni kuwa Kikwete katupa kauli wananchi. Sasa hivi mwananchi anasikika tofauti na huko nyuma.
“Lakini safari yake ni ndefu, aendelee kurudisha imani kwa wananchi na si kwa hotuba zenye maneno mazuri bali kwa vitendo. Tumeona moja ya tume yake inafanya kazi, wahusika wamefikishwa mbele ya sheria na kesi inaendelea. Miaka ya nyuma ilifika mahala watu wakasema hatutaki tena tume za uchunguzi,” anasema na kuongeza:
“Suala la umeme nalo si jambo ambalo linataka siasa kwa sababu athari ni kubwa kwa taifa. Ni wazi kuwa waliotangulia walikosea. Hawa planners walikosea na hawataki kukubali, lakini mimi naona kukubali kosa ni uungwana kuliko kuwa mkaidi.
“Haya watasema kuwa vyanzo vya maji viliharibiwa, fine! Sasa wao walikuwa wapi wakati mambo yakiharibika? Kwa mtindo huu tunatingisha uchumi.”
Anapozungumzia suala la maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi, Vicensia anasema pamoja na ukweli kwamba ugonjwa huo ni hatari bado upo umuhimu kwa baadhi ya taasisi kubadilika katika utoaji wa elimu.
“Nimesikia wengine wakisema eti mbio za mwenge zinaeneza ukimwi sasa hapo mimi hushangaa. Hivi kweli mtu atakaa mwaka mzima bila kufanya ngono akisubiri mbio za mwenge? Kwa kweli tusidanganyane,” anasema.
Hata hivyo, anasema kitendo cha baadhi ya viongozi wa dini kukataza matumizi ya kondomu katika mapenzi nacho ni sawa na uuaji. “Wannatukataza tusitumie kondomu, tukifa sadaka zitatoka wapi?
“Njia hapa ni kuangalia jinsi ya kuwaokoa waumini na si kuzuia matumizi ya kondomu kwa sababu kanisa linahitaji watu ili lijiendeshe. Mimi ni Mkatoliki na ninavyojua misaada kutoka Roma haipo na kwa maana hiyo tunajitegemea,” anasema.
Vicensia ni binti mwenye misimamo ambayo lazima umeze mate ndipo uweze kumwelewa. Wakati mwingine unaweza kudhani anatania lakini binafsi husisitiza kuwa anamaanisha anachosema. Mfano ni msimamo wake kuhusu mavazi.
Anasema hakuna mtu atakayeweza kumfunga minyororo ya akili kwamba achague nguo fulani ya kuvaa. Atafanya hivyo kama ataona inafaa kwa wakati huo lakini si kwenda na upepo usiojulikana umetokea wapi.
“Wanasema wasichana wanatembea nusu uchi, kwani sheria ya inasemaje? Kuvaa min skirt si kosa kwa mujibu wa sheria. Itakuwa kosa kama mtu katembea uchi wa mnyama kwa maana bila nguo.
“Kama wanasema tunawatamisha ni sawa lakini hata sisi tunatamani pia. Ukipita mjini mbona wanaume wanatembea vifua wazi? Msimamo kwamba wanawake ndio wazibe miili yao na wanaume watembee vifua wazi huu ni udhalilishaji.
“Hapa wasitake kuchanganya dini na masuala ya kawaida. Imani za dini waachiwe masheikh na mapadri. Mimi kwa mfano siku nikivaa kimini halafu wanishambulie hakika nitapigana hadi kifo, sitakubali.
“Kama wanasema tunawatamanisha itafika siku watazoea kuona mapaja na akili zao zitahamia kwa wanawake waliovaa hijab.”
Akizungumzia kuhusu wanenguaji wa kike katika bendi za muziki wa dansi wanaovaa nguo zinazoonyesha sehemu kubwa ya miili yao huku wanamuziki wa kiume wakivaa suti, Vicensia anasema jambo hili linapaswa liangaliwe kwa upana zaidi.
“Je, watazamaji walishagoma kuangalia dansi kwa sababu ya mavazi? Waajiri waulizwe na hawa mabinti waulizwe na Serikali pia iseme kama kuna sheria inazuia jambo hili. Mawaziri wengi wameshawahi kuangalia maonyesho ya aina hiyo, je, wao wametoa msimamo gani?”
Anasema suala la mavazi wakati mwingine huendana na miiko ya kazi ya mhusika kama ilivyo kwa baadhi ya ofisi ambazo lazima uvae nguo fupi kama hukubali basi unaondoka.
“Nimezaliwa huru na lazima niwe huru, nivae kitu ninachokipenda na ndio maana kama mwanamume nampenda hata kama nimekutana naye kwa mara ya kwanza nitamweleza. Wanawake lazima tuwe wazi kusema kilicho moyoni manake hata sisi tunatamani kama walivyo wanaume.”
Vicensia ambaye katika miaka ya nyuma aliwahi kuuza baa yao ya Safari iliyoko Maili Sita nje kidogo ya mji wa Moshi, alizaliwa Machi 14, 1978 ni kitinda mimba katika familia ya watoto wanane. Sita wa kike na wawili wavulana.
Alilazimika kuuza baa kama mchango wake katika familia ili kutunisha pesa zake za masomo na mahitaji mengine ya msingi.
“Tusiibeze kazi hii ya baa kwa sababu watu wengi inawasaidia kutunza familia na mimi nimefanya kumsaidia mama kufanya hesabu na kuwasimamia wafanyakazi wengine.”
Alisoma Shule ya Msingi Kilimanjaro mwaka 1985 hadi 1991 na kisha Shule ya Sekondari Mawenzi mwaka 1992-1995 kabla ya kujiunga Mkwawa mwaka 1996-1998. Alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuchukua shahada ya kwanza ya sanaa. Alimaliza Shahada ya Uzamili mwaka 2004 miaka miwili tangu aajiriwe katika nafasi ya uhadhiri chuoni hapo.
Vipi kuhusu ndoa? “Hilo ni jambo ambalo halipo kwenye akili yangu kabisa acha nikae kwanza na wala sijali nitakaa kwa muda gani.”
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment