Na Innocent Munyuku
NI Jumatano jioni wiki hii, simu yangu ya mkononi inanikumbusha kwamba natakiwa kufanya mahojiano na mwanamuziki Carola Kinasha.
Mvua ya Dar es Salaam inaharibu kidogo utaratibu au ratiba ya siku hiyo, lakini kwa vile nilikuwa na shauku ya kuzungumza naye nafanya kila liwezekanalo kuwahi eneo la mazungumzo.
“Karibu rafiki pole kwa mvua,” ndivyo anavyonikaribisha Carola kwenye kibanda cha mapumziko kilichopewa jina la Kabarega kilichopo Ambassador Plaza, Morocco jijini Dar es Salaam.
Hatuko wawili tu, shuhuda wa mazungumzo yetu ni Mratibu wa shughuli za msanii huyo, Gota Warioba na hivyo kuunda utatu ambao hata hivyo hatuwezi kuuita mtakatifu kwani miongoni mwetu wapo wanaburudika na mvinyo.
Nilishasikia baadhi ya nyimbo zake kabla na wa hivi karibuni wimbo uliozidi kunivutia unakwenda kwa jina la Ni Pendo.
Carola anasema tangu mwaka 1989, nia yake imekuwa ni kuutambulisha muziki wa Tanzania kimataifa na bado ameshikilia msimamo huo.
Lakini jambo moja analoliweka wazi ni kwamba huwezi kuupeleka muziki wa Kitanzania nje bila kuwa mbunifu kwa kuchanganya muziki wa makabila mbalimbali.
“Mtindo wangu ninaoutumia unaitwa Bongo Fusion, ni mtindo ambao nachanganya muziki wa asili na vionjo vya kisasa…huwezi kuipeleka Sindimba kama ilivyo na ikapata soko la kimataifa,” anasema Carola.
Kwa sasa yu katika kundi la muziki lijulikanalo kama Shada linaloundwa na Athanas Lukindo ambaye ni mumewe. Pia wamo Teddy Mbaraka, Norman Bikaka, Miraj Hussein, Mohamed Omar na Seleman Penza.
Alishafanya ziara na utafiti wa muziki katika Zimbabwe, Norway, Angola na Msumbiji akiwa na kundi la muziki linaloundwa na wanawake. Hawa wanajiita Women’s Voice.
“Tulifanya maajabu na binafsi nilijifunza mambo mengi sana na huwa huru kufanya maonyesho nikiwa na wanawake wenzangu stejini,” anasema Carola na kisha kuongeza:
“Kwa hiyo kwa changamoto nilizopata nikazidi kuwa na imani kwamba mawazo yangu ya kuutangaza muziki wa Kitanzania hayatakwisha.”
Lakini kuna tatizo kubwa katika safari yake hiyo nalo ni mtazamo hasi wa baadhi ya Madj katika vituo mbalimbali vya redio nchini.
“Wamekuwa na mtazamo ambao ni kikwazo kwetu…wanapiga bongofleva lakini si nyimbo za asili. Wakati mwingine wanakuuliza muziki wako tuupige katika kipindi gani?
“Wanauliza kwa sababu katika redio nyingi hakuna vipindi kwa ajili ya muziki kama ninaoupiga.”
Carola ndiye yule aliyeimbwa na Dk. Remmy Ongala katika wimbo wake maarufu wa Carola. Ilikuwaje hadi akakutana na Ongala?
“Walikuwa na project fupi ya muziki na lengo lao lilikuwa kufanya ziara barani Ulaya, kwa hiyo Dk. Remmy akanichukua katika mazoezi na hapo nikashtukia siku moja anaimba jina langu nikiwa stejini. Ukawa wimbo rasmi.”
Carola pamoja na kuwa mwanamuziki, inastaajabisha kuona kwamba baba yake mzazi alikuwa Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Longido mkoani Arusha.
Akizungumzia namna alivyoingia kwenye muziki, anasema ilikuwa suala lililompa uamuzi mgumu kutokana na imani ya familia hasa babaye mzazi.
Hata hivyo, kaka zake walimpa ushirikiano kwa kuwaelimisha wazazi juu ya uamuzi wake huo. “Wakati ule kule kwetu umasaini lilikuwa jambo gumu kufikia uamuzi wa jinsi hiyo lakini nilidhamiria.”
Anapozungumzia suala la haki miliki kwa wasanii nchini, anasema kuna tatizo kubwa kwa wasanii wengi. Kwamba wengi wao hawataki kujiunga na COSOTA kwa sababu kazi wanazofanya si za kwao.
“Watayarishaji wa muziki wanachangia hili. Mwanamuziki anakuja na mashairi yake lakini midundo ya muziki imeibwa kutoka katika intaneti.
“Kwa hiyo wanaogopa kujisajili kwa sababu wanajua si kazi zao za asili,” anasema Carola.
Lakini sasa Carola anaandaa kupakua albamu yake mpya ya Maono. Anasema anaamini kuwa kwa albamu hiyo atapata nafasi ya kujitanua kwa mashabiki ndani na nje ya Tanzania.
“Hii albamu ya Maono bila shaka itafungua milango ya fusion kuna hisia za kweli ndani yake na nataka watu wajue kuwa mawazo yangu si ya leo au kesho ni ya muda mrefu.”
Hata hivyo, anasema kazi ya muziki kwa Tanzania ni ngumu hasa kwa mwanamke. Kwamba wapo wanaoamini kuwa mwanamke akiwa mwanamuziki basi ni mhuni.
“Hili jambo linakera nafsi, kudharauliwa imekuwa sehemu ya kazi, ni attitude ya muda mrefu,” anasema.
“Nimeshakuwa sugu na kwa hakika nitaendelea na msimamo wangu na kuiheshimu kazi yangu pia. Na ndio maana nasema fusion itakua na muziki wa Tanzania utajulikana kimataifa.
“Kwanini uimbe muziki ambao tayari uko Ulaya au Marekani? Wanataka kitu kipya, kwa hiyo tupeleke mambo mapya sokoni.”
Carola kichwani kwake amesokota nywele zake kwa mtindo wa rasta staili ambayo anasema inamfanya apunguze safari za saluni.
Mbali na kuimba, anamudu kupiga gitaa la rhythm na baadhi ya ala za kabila la Wagogo.
Mwanamama huyo mwenye umri wa miaka 45 ana shahada ya Uhusiano wa Kimataifa na Kifaransa aliyoipata Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1987. Anaishi kwenye ndoa akiwa na watoto wawili.
Monday, September 3, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment