Na Innocent Munyuku
AMANI iwe kwenu waungwana wa safu hii. Bila shaka mambo yaenda kwa unyoofu pasipo bughudha. Mzee wa Busati karejea lakini yu mpole Jumatatu hii.
Mwenye Busati kanywea kwa vile anajua kosa kubwa alilowatenda wadau wake. Juma lililopita alizimika na hakuonekana hapa. Alizimika kama mshumaa jangwani. Anaomba radhi kwa hilo.
Bila shaka waliofura kwa hasira kwa kukosa porojo za Mzee wa Busati wametulia kwa furaha baada ya kuona kandanda swafi la Taifa Stars kwenye dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza juzi.
Mbali na kupata matumaini mapya kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Senegal, Mzee wa Busati amefarijika kuona kuwa msimamo wa kocha wa Stars, Marcio Maximo umewaumbua wenye vidomodomo.
Mei 14 mwaka huu katika safu hii Mzee wa Busati aliandika porojo ambazo zilimwongezea marafiki na maadui lukuki. Kichwa cha habari kilikuwa: ‘Mwataka Maximo awakunje samaki wakavu?’
Lilikuwa juma ambalo wanaojiita wadau wa soka walikuwa wamepaza sauti zao kumlaumu Maximo kwa uteuzi wa kikosi kipya cha Stars.
Wadau hao wakamrushia vijembe na kujaza mate vipaza sauti katika studio za redio na vituo vya runinga. Wakawekewa vipindi maalumu kwa ajili ya kutoa hoja kwa kile walichodai eti Maximo katokota.
Walikuwa wakimlaumu wakisema kwamba hakupaswa kuwaacha wachezaji wazoefu katika maandalizi ya kuivaa Senegal katika mechi ya marudiano baada ya Stars kunyukwa mabao 4-0 jijini Senegal.
Bila shaka hofu yao ilikuwa kwamba kama hao ‘nyota’ walikuwa kundini wakati Stars inalambwa mabao 4-0 hali itakuwaje bila wao katika marudiano? Si itakuwa mvua ya mabao?
Wakalalama kweli kweli utadhani wanaomba kura za kuingia bungeni kwenye majimbo magumu kama lile la kule kwa kina fulani.
Hoja ikawa hiyo na kwa vile wengi wao walishapewa heshima na wabongo kwamba wanajua uchambuzi wa soka, lawama zao zikaanza kukubalika.
Ikawa hoja kuu kwenye vijiwe vya wajuzi wa soka na wasiojua. Lakini hiyo haiwezi kuhalalishwa kuwa ni dhambi kwani Katiba yampa nafasi kila mmoja kutoa maoni pasipo kuvunja sheria.
Hoja yao ikawa kwamba Maximo ataumbuka kwa vile kawaacha wachezaji nyota katika timu hiyo! Mzee wa Busati akahoji, hao maarufu ni kina nani? Ni hawa Gaudence Mwaikimbika na Juma Kaseja.
Wenye akili zao timamu wakakaa pembeni wakicheka. Naam walicheka kwa sababu hukumu aliyokuwa akipewa Maximo ilikuwa kama vile kaulisha sumu ulimwengu uteketee.
Watoa lawama hawakuwa na mbadala makini kwani uwepo wa Mwaikimba au Kaseja haukuwa na maana yoyote kule Dakar Senegal. Wakasahau kwamba hawa si maarufu na si lolote. Hivi hawa umaarufu wao ni wa kimataifa?
Umaarufu wao unapimwa vipi? Au walitumia ile falsafa ya kwenda kwenye wodi ya wagonjwa mahututi na kuomba mashindano ya kumsaka mbabe wa dunia katika masumbwi, mieleka au kunyanyua vitu vizito?
Mzee wa Busati moyo wake umeridhika kuona kuwa wenye kupenda lawama sasa wameumbuka na bila shaka almanusura waangukie pua kutokana na matokeo ya Stars.
Ni wazi kwamba kwa kawaida ukianzisha hoja ni lazima uitetee hata kama hoja hiyo haina matokeo mema kwa jamii. Ndivyo binadamu alivyo. Si mnamwona Rais Bush wa Marekani na msimamo wake juu ya Irak? Amesimama kidete hajali maafa anayoyasabisha.
Mzee wa Busati anaomba aeleweke kwamba hajaja hapa kutoa lawama. Anachojaribu kunena ni kwamba tusiwe wepesi wa kulaumiana na kuwaona wawajibikaji kama hamnazo.
Mbaya zaidi ni kwamba hao waliokuwa wakilalama wengi wao walishindwa kuonyesha makali walipopewa nafasi ya kuzinoa timu za taifa au klabu.
Mwenye Busati akaweka wazi kuwa kikwazo kwa soka ya Tanzania si la Maximo, huyu alikuta hawa wachezaji wameshakauka. Je, awakunje wakiwa wakavu? Hapana!
Tulikaa na kuegemea mambo mengine tukasahau kwamba upo umuhimu wa kuwa na vitalu vya soka. Tukajiwekea taratibu za kucheza soka kwa ridhaa na pasipo haraka ya kung’ara duniani.
Watawala wetu hawakusukumwa kujali soka, waliendekeza siasa na pengine kwa kukosa washauri wakaamini kwamba soka ni uhuni wakasusa. Leo hii wamekuja wengine tuwaachie tuone wanafanya nini. Usiwe wakati wa kusutana.
Mzee wa Busati kafika ukomo kwa juma hili. Hakuna matata walau wiki hii kaonja vipapatio vya kuku kwa vile imekuwa wiki ya neema.
Wasalaam,
Monday, September 3, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment