na innocent munyuku
KWA wajuzi au wataalamu wa mapishi hasa katika Ukanda wa Pwani si wageni na neno pishori.
Pishori au pengine huitwa pisori ni aina mchele ambao ni mweupe, mwembamba na huaminika kuwa bora katika uso wa dunia.
Mzee wa Busati kama ilivyo kawaida yake si mtu wa kuridhika kupitwa na mengi ya mjini, iwe umbeya au nong’ono za kila kona. Yote huyadaka na kuyachuja.
Mwishoni mwa juma lililopita jiji la Darisalama liligubikwa na kila aina ya starehe lakini kubwa likiwa ni mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Taifa Stars ‘JK Boys’ dhidi ya Uganda Cranes na shindano la kumsaka Miss Tanzania.
Kwa vile shughuli zote mbili zilikuja tarehe nzuri basi wengi walidata kisawasawa na bila shaka wakakumbwa na wakati mgumu katika kuchagua wapi pa kwenda kujipa raha. Utawaambia nini wakati ngwenje zinafoka kibindoni?
Wabongo bana wakiwa nazo utawaambia nini? Kwenye soka walijaa na hata katika shindano la kumsaka mnyange bora nako wakafurika ili kuwa mashuhuda wa mchuano huo.
Kwenye Uwanja Mpya wa Taifa mambo yalikuwa safi kwani vijana walitoa raha kwa ushindi wao wa bao 1-0 na hiyo ni dalili njema kwamba uwanja umeanza kwa neema kwa Wadanganyika. Bila shaka wa Nchumbiji wakija nao watakula kichapo cha Kiyahudi.
Kwa upande wa shindano la warembo yasemekana mambo yalikwenda upogo baada ya Richa Adhia kutangazwa kuwa mrithi wa kiti cha Wema Sepetu.
Mashabiki wengi walilalama kwamba haki haikutendeka katika shindano hilo kwani liligubikwa na utata na ndio maana baadhi yao wakadiriki kuwavaa mabosi wa Kamati ya Miss Tanzania wakihoji uhalali wa matokeo hayo.
Wadadisi wa mambo na ambao ndimi zao haziogopi kunena wanasema kuna uhuni ulifanyika hasa katika kipindi cha maswali kwa warembo.
Hao wana hoja na mfano ni pale mnyange Victoria Martin aliposhtukizwa swali ambalo lilibuniwa fasta jukwaani.
Kwa kawaida mrembo zamu yake ya kuulizwa swali huchagua kikaratasi kimoja katika ‘kapu’. Karatasi hiyo huonyesha aina ya swali analoposwa kujibu.
Kwa Victoria hilo halikufanyika kwa mwongozo mzuri kwani karatasi yake ilikuwa tupu. Je, hii maana yake ni kwamba hakustahili kujibu lolote usiku ule? Tuachane na hilo.
Mzee wa Busati sasa anazidi kujiweka pembeni na masuala hayo ya urembo hasa linapokuja suala la mashindano kama hayo. Kwamba Kamati ya Miss Tanzania kila mwaka ni vurugu mechi.
Hamkuwahi kusikia kuwa hata mnyange wa mwaka juzi, Nancy Sumary hakuwa chaguo la kamati hiyo? Mwenye Busati hana uhakika kama kina Lundenga walipata kukanusha hilo. Lakini ukweli ni kwamba Nancy aliweka historia mpya kwa kunasa taji la Miss World Africa.
Lakini Lundenga usiku ule wa juzi baada ya kumalizika kwa shindano alitoa kauli ambayo ni tata kwa upande wa Mzee wa Busati. Alipoulizwa juu ya utata wa shindano akajibu kwamba yawezekana baadhi ya wasichana wana kasoro.
Hilo halipingiki! Kwamba katika kila shindano lazima kuwapo na washiriki wenye kasoro. Lakini kinamchomshangaza Mwandika Busati ni ile kauli eti baadhi ya warembo wana ukurutu ambao hauwezi kupona!
Hivi si kina Lundenga hawa hawa ndio waliowahi kutamba kwamba warembo wote wana ubora? Au walikuwa wanatoa hadaa kwa washiriki na umma wa Wadanganyika kwa ujumla?
Haya basi tukubali kwamba kuna wenye ukurutu sugu. Je, na hili la kumbambikia swali binti Martin nalo linazungumzwaje?
Potelea mbali lakini bila shaka kina Lundenga mwaka huu wameona ni vema wapeleke pishori Miss World ili taji litue bongo.
Kila la heri lakini kumbukeni kuwa wakati mwingine pishori ikienda Usukumani haiwezi kupikwa vema kwani huko wanatarajia wapewe unga wapike ugali na si mchele kwa ajili ya wali.
Watu wa Kagera wakimsubiri mgeni wa Kimakonde wanataraji atakuja na ndonya au chamaki nchanga vivyo hivyo kwa Mhaya atakwenda Mtwara na senene na si asali ya Tabora!
Wasalaam,
Monday, September 3, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment