Sunday, April 29, 2007

Maembe? Hapana na Manyama pia

Na Innocent Munyuku
WAKATI fulani mwaka jana nilipata kuandika habari ya mwanamuziki Vitali Maembe na kundi lake la Bagamoyo Spirits. Nikamweka msanii huyo miongoni mwa wakali waliopata kutokea katika uso wa dunia.
Huo ni mtazamo wangu kwamba kwa namna anavyosonga mbele kwa kasi ya ajabu, ni wazi kuwa Maembe na kundi lake anayo nafasi ya kufanya vema katika safari yake ya muziki huko aendako.
Hilo linatokana na ukweli kwamba tofauti na wanamuziki wengi wa kizazi kipya nchini Tanzania, Maembe na kundi lake wanapiga vyombo vya asili. Midundo ukiisikiliza huwezi kupata ladha ya Kimagharibi.
Vitali Maembe? Pengine wengi watajiuliza. Ndio ni Maembe yule aliyevuma na kibao cha Sumu ya Teja na baadaye akaja na wimbo wa Kariakoo. Hivi karibuni kaibuka upya na kibao cha Shangilia Taifa Stars pamoja na Mchakamchaka.
Hata hivyo, ukweli wa mambo ni kwamba katika mafanikio yote hayo, Maembe naweza kutamka kuwa anabebwa kwa kiasi kikubwa na mmoja wa wasanii chipukizi. Huyu ni Manyama Nyambasi mwenye umri wa miaka 15.
Pengine neno kubebwa laweza kuleta ukakasi kwa mashabiki wa Maembe ila kusudio langu ni kuweka bayana moja ya siri za mafanikio kwa mwanamuziki huyo.
Nyambasi kwa umri wake huo mdogo ndiye kinara wa upigaji ngoma katika kundi hilo. Kijana huyo ambaye alianza kuchomoza kwenye vyombo vya habari zaidi ya miaka mitano nyuma anamudu kupiga ngoma 12.
Msanii huyo chipukizi kwa hakika ni nuru kwa Maembe na kundi lake. Daima ni makini katika upigaji wa ngoma zake anazozipiga kwa ustadi mkubwa.
Cha kufurahisha ni kwamba licha ya uwingi wa ngoma hizo, Manyama anamudu kuzipiga mfululizo kwa zaidi ya dakika 20.
Pengine huyu aweza kuitwa mrithi sahihi wa msanii aliyewahi kuvuma nchini Tanzania, marehemu Morris Nyunyusa kutokana na umahiri wake huo.
Pamoja na uwepo wa Manyama katika kundi la Bagamoyo Spirits, bado anahitaji msaada wa kunogesha midundo ya ngoma zake. Rafiki yake mkubwa jukwaani ni Salum Mpute.
Mpute kama alivyo Manyama, ana umri wa miaka 15 na kazi yake kubwa jukwaani licha ya kuimba baadhi ya mashairi, hupiga manyanga. Ukali wao waweza kufananishwa na pilipili au moto wa kuotea mbali kama wengine wanavyosema.
Hii ni hazina ya Bagamoyo Spirits kwani kama ulivyo msimamo wa kiongozi wao, Maembe hawana haja ya kukimbilia midundo ya Ulaya na Marekani.
Hawako tayari kusahau asili yao ambayo ni bara la Afrika. Hawabezi ngoma wala manyanga.
Hawataki kuwa miongoni mwa vijana wenye akili za utumwa. Vijana ambao wanaendelea kuamini kwamba kila wakionacho kwenye runinga basi ni cha kuigwa.
Kutokana na hilo ndio maana wengi wao hawajui kupiga ala mbalimbali za muziki. Je, na hawa tuwaite wanamuziki? Hapana!
Kwa muungano huo wa Bagamoyo Spirits, hawana cha kujuta kwa sababu kitendo chao cha kuweka lafudhi za Kiafrika kwenye kazi zao vibao vyao vinavuma katika kona nyingi duniani.
Katika albamu ya BAGAMOYO unaweza kuwa shuhuda wa uhondo wa midundo ya kiafrika katika nyimbo hizo. Kuna vibao kama Afrika Shilingi Tano, Sumu ya Teja, Toka na Asalaam Aleykhum. Hizi ziko katika video huko Mbwa wa Kiombwe, Naropoka, Kipande cha Papa, Kinoo na Hamia Ndege zikisubiri.
Tumwangalie Maembe na Bagamoyo Spirits lakini pia tuwapaishe kina Manyama na Mpute waendeleze vipaji vyao wakiwa ndani ya kundi hilo linalotamba na mtindo wa Motokaa.

No comments: