Na Innocent Munyuku
KAMA kuna masuala ambayo yamekuwa yakipigiwa zumari katika sehemu nyingi duniani, usawa katika jamii na maisha bora huwezi kuviweka kando.
Zipo asasi nyingi nchini zilizoweka mikakati ya kutatua mambo kama hayo na moja ya asasi hizo ni Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) iliyoanzishwa mwaka 1993.
TGNP ni asasi isiyo ya kiserikali na kuundwa kwake kulilenga zaidi kuleta usawa wa jinsia katika jamii, kuwawezesha wanawake, mafunzo, utafiti na kusambaza taarifa muhimu zinazolenga ustawi wa jamii.
Hivi karibuni TGNP ilipata Mkurugenzi Mtendaji, Usu Mallya anayechukua nafasi ya Mary Rusimbi aliyemaliza muda wake.
Je, mkurugenzi huyo mpya ana mkakati gani baada ya kukalia usukani wa kuipeleka asasi hiyo mbele kimafanikio?
Katika mahojiano maalumu na MTANZANIA Jumapili juzi, Usu anasema mbali na kuwa na jukumu la usimamizi wa asasi hiyo, mfumo wa TGNP unamweka katika mazingira ya kufurahia kazi yake.
“TGNP imejengwa kwa namna kwamba kila jambo linafanywa kwa ushirikiano, hakuna maamuzi ya mtu mmoja.
“Lakini pia niko hapa tangu mwaka 1998 kwa hiyo nimejifunza mengi hapa hasa katika mkakati wa kujenga nguvu za pamoja,” anasema Usu na kisha kuongeza:
“Mtandao wetu umejengwa katika mhimili wa pamoja katika dhamira na dira.”
Pamoja na ukweli kwamba manyanyaso au ubaguzi wa kijinsia upo duniani kwa miaka mingi, nchi nyingi za Afrika ikiwemo Tanzania zilipata mwamko baada ya Mkutano wa Beijing Septemba mwaka 1995.
Katika mkutano huo wa wanawake uliazimia mambo mbalimbali ikiwemo kubadili mtazamo wa jamii katika kutendeana haki pasipo kubaguana.
Pia kujali utu na kumpa mwanamke sauti na kwamba wanaume kwa miaka mingi wamekuwa kikwazo katika maendeleo binafsi ya mwanamke.
Lakini je, baada ya miaka 12 kupita, TGNP inatathimini vipi mafanikio ya azimio la Beijing?
“Zipo fursa nyingi kwa wanawake lakini bado Serikali ina changamoto nyingi kufikia maendeleo.
“Katika elimu kumekuwa na jitihada lakini uwiano ni mdogo katika ngazi ya elimu ya juu. Kwa mfano wasichana wanaovuka kwenda kidato cha tano, sita hadi chuo kikuu inashuka,” anasema Usu.
Anaeleza kuwa kushuka kwa kiwango hicho kunatokana na mazingira au mfumo uliopo katika sheria za nchi.
“Sheria ya ndoa kwa mfano inaweka wazi kuwa mtoto wa kike anaweza kuolewa afikishapo umri wa miaka 14 au 15…sasa huu ndio muda wa mtoto kuwa shule. Akishaolewa safari yake inakuwa imeishia hapo.
“Lakini pia sheria kwamba mtoto wa kike akipata ujauzito abaki nyumbani nayo imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi ya wasichana wenye elimu ya chini katika jamii.”
Hata hivyo, anasema maazimio mengine ya Beijing yanakwamishwa na sera za ubinafsishaji nchini.
Kwamba uchumi sasa ni wa utandawazi unaoongozwa na makampuni kutoka nchi tajiri duniani.
“Mikataba mingi katika eneo hilo ni ya kuwakandamiza wananchi, hii mikataba haijengi nchi changa.
“Nitoe mfano wa hapa kwetu, mkataba wa Bi-water umeshatuumiza, angalia suala la Richmond na umeme wetu au madini.
“Haya mambo yote yametuathiri kwa sababu ya utandawazi, angalia nchi kama Afrika Kusini, imeendelea kwa kiwango kikubwa kwa vile wametumia madini yao kujinufaisha. Hali ni tofauti na Tanzania,” anasema.
Anasema kutokana na mazingira kama hayo, hata jitihada za kuwakomboa Watanzania kutoka katika umasikini zinakuwa ngumu.
“Wanawake kwa mfano wako kwenye uchumi mdogo mdogo. Ninachosema hapa ni kwamba kama Serikali imeshindwa kuhodhi rasilimali basi hata hawa wa chini wataendelea kuumia,” anasema Usu.
Anazungumzia pia sekta ya utalii ambayo kwa mtazamo wake haijampa fursa Mtanzania kunufaika nayo.
“Nani anafaidi matunda ya utalii? Bila shaka ni watu wachache sana,” anasema.
Mbali na uchumi kuwa suala gumu katika kuwaendeleza Watanzania, kuna kikwazo katika sekta ya afya.
“Eneo hili ni changamoto kubwa kwa Serikali kwani linatakiwa kuwezeshwa na anayeumia sana ni mwanamke.
“Vifaa au huduma katika sekta hii bado haijamhakikishia mwanamke hatima njema hasa katika uzazi. Kuna takwimu zinazoonyesha kuwa katika wanawake 560 kati ya 100,000 hufariki dunia kila mwaka kutokana na uzazi usio salama.
“Hii ni dalili au ishara kwamba Serikali inakabiliwa na changamoto kubwa katika sekta ya afya hasa kwa afya ya mwanamke.”
Analalamikia uonevu ambao unachukua sura tofauti kila siku dhidi ya mwanamke.
“Kuna manyanyaso kwa wanawake, wengi wana uwezo mdogo wa kufanya maamuzi kuhusu ngono au idadi ya watoto.
“Ni jambo linalofanywa kuwa ni kawaida kwa mjamzito kufanya kazi za nyumbani huku akiwa na lishe duni hii si ajabu ikachangia vifo wakati mwingine.”
Vipi kuhusu nafasi ya mwanamke katika uongozi?
Usu anasema pamoja kuwa na wabunge wanawake kwa asilimia 30, bado kiwango hicho hakitoshi.
“Wapewe sauti au nafasi pia kuanzia kwenye udiwani…lakini pia naweza kusema kuwa wanawake wanahitaji nafasi pia katika sekta binafsi.
“Hata serikalini ipo haja kwa wanawake kupewa nafasi za juu kama vile ukuu wa mikoa, ukatibu mkuu, ubalozi nje ya nchi, ukurugenzi wa bodi au ujaji,” anasema Usu.
Pamoja na hilo, Usu anasema kuna mambo ambayo lazima yasemwe kwa uwazi au kujadiliwa kitaifa kuhusu utamaduni wa Mtanzania kutokana na ukweli kwamba mengi yanatokana na upotoshwaji wa mila.
Anasema jamii mara nyingi inamwona mwanamke kama chombo cha starehe na hata watoto wanapokua, mtoto wa kike tayari ameshajenga dhana ya kuwa wa chini.
“Hili ni suala nyeti linalopaswa kujadiliwa kitaifa, ni kama ilivyo rushwa lazima lijadiliwe. Hili jambo si la TGNP pekee bali Serikali nayo ihusike.”
Tangu kuanzishwa kwake, TGNP imefanikiwa katika kufikisha ujumbe kwa jamii kwa njia ya semina mbalimbali na kushirikiana na wanaharakati katika ngazi mbalimbali.
Mara nyingi imeshirikiana na FemAct katika kuilemisha jamii na ushirikiano huo upo kwa wanaharakati katika wilaya mbalimbali nchini.
“Tunatambua kazi za wanaharakati katika ngazi husika kwa kufanya semina na nafasi ya elimu kwa watu wa rika mbalimbali,” anasema Usu.
Mbali na semina, kila baada ya miaka miwili, TGNP hufanya tamasha la kijinsia ambalo huwapa fursa washiriki kufanya tathimini.
“Watu mbalimbali hualikwa na kinachofanyika ni kuibua mijadala na kushinikiza mabadiliko.
“Kuna sera kama mgawanyo mbovu wa mali katika familia kama vile ardhi au ukatili nazo hujadiliwa.
“Tumeanza kuishinikiza Serikali ibadili pia Katiba ya nchi kwani haimtendei haki mwanamke linapokuja suala la ndoa.
“Kuna mapungufu kwa mfano Katiba inaruhusu sheria za jadi kutambuliwa, sasa katika hali kama hiyo ni wazi kuwa mwanamke anapewa haki na wakati huo huo kumnyang’anya.
“Unaporuhusu kutumika kwa sheria ya jadi maana yake ni kuruhusu unyanyasaji kwani sheria nyingi za jadi zinamkandamiza mwanamke,” anasema.
TGNP imeshatoa mabango ya aina mbalimbali yanayolenga kuielimisha jamii.
Katika Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge mwaka 2005 walitoa bango la ‘Wakati umefika! Uwezo wa kuongoza tunao! Wanawake tujitokeze’.
Yapo mabango mengine kama la mwaka 2001 linalosomeka ‘Jinsia, demokrasia na maendeleo mbinu mbadala za kukabiliana na kufukarishwa’.
Lipo jingine la mwaka 2004 ‘Tatizo la dunia ya leo si umasikini ni mgawanyiko wa rasilimali wa kinyonyaji’.
Mwaka jana walikemea ubinafsishaji holela wa sekta ya maji.
Na mwaka huu TGNP imekuja na bango la ‘Sema hapana kwa ukatili wa kijinsia’.
Mbali na hayo wamekuwa na machapichopendwa kwa njia ya vitabu kama vile, Kwangu Wapi, Vijana Taifa la Leo, Kondomu Yazua Kasheshe, Utandawazi na Wewe na Ahadi za Uongo.
Pia TGNP imekuwa ikitoa vitabu vya kitaaluma kwa watafiti na wanafunzi. Baadhi ni Gender Profile of Tanzania: Enhancing Gender Family, Activists Voices, Against Neo Liberalism na Gender Budget Analysis in Tanzania 1997-2000.
Kuna maktaba ya kisasa na duka la vitabu katika ofisi hizo zilizopo eneo la Mabibo jijini Dar es Salaam na kila Jumatano huendeshwa semina kwa watu wote katika ofisi hizo kuanzia saa tisa mchana hadi 11 jioni.
Usu Mallya alitokea wapi? Alizaliwa mkoani Shinyanga mwaka 1961 na elimu yake ya msingi aliipata Marangu Sembeti Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro. Hii ilikuwa kati ya mwaka 1968-74.
Kati ya mwaka 1975-78 alikuwa Shule ya Sekondari ya Kibosho alikohitimu kidato cha nne. Elimu ya juu ya sekondari aliipata Korogwe mkoani Tanga.
Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikopata shahada ya kwanza ya uongozi wa taasisi za umma, sayansi ya jamii na Kifaransa. Alihitimu mwaka 1985.
Aliwahi kufanya kazi chuoni hapo katika Idara ya Sayansi ya Jamii kati ya mwaka 1990-95.
Alirejea darasani kusomea shahada ya uzamili chuoni hapo akichukua masomo ya sayansi ya jamii. Alihitimu mwaka 1997.
Mwaka mmoja baadaye akajiunga na TGNP.
Sunday, April 29, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment