KAMA kuna mambo ambayo Rais Yoweri Museveni wa Uganga yanamwumiza kichwa basi uwepo wa waasi wa LRA ni mojawapo.
Lakini ukiachana na jambo hilo, hakuna shaka kwamba katika utawala wake wa zaidi ya miaka 20, Rais Museveni hatasahau namna mwanamke mmoja alivyoichachafya Serikali yake mwanzoni kabisa mwa utawala wake.
Huyu ni Alice Auma ambaye baadaye alijipachika jina la Alice Lakwena. Lakwena likiwa na maana ya mjumbe maalumu.
Kwa nguvu ya Museveni na namna alivyokuwa ameanza kujijengea ngome kuu katika utawala wake, haikuwa rahisi kuamini kuwa angetokea mwanamke kuupinga utawala wake nchini Uganda.
Alice aliyezaliwa mwaka 1956 kutoka kabila la Acholi aliendesha mambo yake kwa staili ya imani za mizimu na katika hilo aliungwa mkono na wengi.
Hata alipoanzisha chama chake cha Holy Spirit Movement (HSM), haikuwa kazi ngumu kupata wafuasi kwani walio wengi waliamini kuwa Alice ana maono ya hali ya juu.
Kutokana na imani hiyo, akaingia mwituni kuupinga utawala wa Museveni kati ya Agosti mwaka 1986 hadi Novemba 1987.
Katika uhai wake, hakuwahi kupata mtoto ingawa aliolewa mara mbili. Baadaye akaachana na imani za kijadi na kujiunga na Kanisa Katoliki.
Hata hivyo, Mei 25, mwaka 1985 akaingiwa na pepo na kuwa mwendawazimu. Uendawazimu huo ukamfanya akose uwezo wa kusikia na kuzungumza pia.
Babaye akalazimika kumkimbiza kwa waganga wa jadi wapatao 11 kwa ajili ya tiba lakini hakuna aliyeweza kutatua tatizo hilo.
Zipo simulizi kwamba baada ya wataalamu hao wa tiba za asili kushindwa kumtibu Alice, babaye mzazi alimpeleka katika Mbuga ya Paraa ambako inaelezwa kuwa alitoweka kwa siku 40 na aliporejea aliambatana na mzimu.
Akawa miongoni mwa watu wenye nguvu za mizimu walioaminika karibu na eneo la Gulu nchini Uganda. Alikuwa na uwezo wa kutibu magonjwa mbalimbali. Inasemwa kwamba mzimu aliorejea nao baada ya kutoweka kwa siku 40 ndio uliomwezesha kupona uendawazimu.
Kutokana na nguvu hiyo, Alice alipata sifa kubwa ndani na nje ya Uganda. Wakati wa mapigano makali baina ya waasi na majeshi ya Serikali inaelezwa kuwa mwanamama huyo alielekezwa na mizimu kuacha kazi za tiba na badala yake aanzishe chama cha kuwakomboa Waganda.
Amri hiyo ya mizimu inadaiwa kutolewa Agosti 6, mwaka 1986 na kwamba kazi iliyokuwa mbele yake ni kusitisha uovu uliokuwa ikiendelea nchini humo.
Kwamba hapakuwa na haja ya kuhubiri au kukaa pembeni wakati kuna damu za raia wasio na hatia zinamwagika.
Katika mpango wake wa awali, Alice alikusudia kuuteka Mji Mkuu Kampala ambao ungekuja kuwa paradiso ya Waganda na bila shaka watu wa kabila la Acholi wangenufaika zaidi.
Alice katika mpango wake huo aliwaeleza watu wake kwamba kila anachopanga kina makusudio mazuri. “Haina maana kuwa daktari na kumtibu mtu leo wakati mtu huyo huyo kesho anauawa.”
Dhamira yake hiyo ndiyo ikamfanya aachane na udaktari na kusimama msitari wa mbele kupinga utawala uliopo.
Alikuja kuwa na msimamo kama wa Joseph Kony ambaye ni kinara wa kundi la waasi la Lord’s Resistance Army. Kwamba lengo ni kumwona Museveni akiachia ngazi nchini Uganda.
Lakini baadaye Alice alionekana kushindwa kutimiza dhamira yake kwani watu wa kabila la Acholi waliendelea kuangamia na ndoto ya kuiteka Kampala ikaanza kutoweka.
Jamii ikaendelea kuingiwa na hofu katika mambo mbalimbali na mbaya zaidi ni kuwa vifo vingi vilihusishwa na uchawi.
Hata hivyo, Alice hakukata tamaa na nguvu yake ikaibuka upya kwani katika hali fulani alipata ushindi kadri alivyoelekea Kampala.
Kwamba licha ya watu wake kuangamia, bado aliendelea kuwa na nguvu ya ushawishi na nguvu hiyo iliwafanya watu wengi kumuunga mkono na safari hii akitangaza kuwa ameongezewa mizimu.
Alifanikiwa kuwashawishi Waganda kwamba Museveni hakuwa mtu sahihi na kwamba aliikalia Uganda kimabavu na anapaswa kuondoka madarakani.
Kwa bahati nzuri kwake, wengi aliowahubiria ni wale ambao waliathirika vibaya na utawala wa Museveni na hivyo kuwa jambo rahisi kwao kumuunga mkono Alice.
Wahenga waliwahi kusema kuwa ngoma ikivuma sana haikawii kupasuka. Ndivyo ilivyotokea kwa Alice na safari yake ya kumng’oa Museveni. Baadhi ya wafuasi wake walianza kumtangaza kuwa ni mchawi.
Kwamba mizimu yake ni ya kichawi inayolenga kuleta maangamizi. Msuguano huo ukaifanya HSM kuzidiwa nguvu na hasa baada ya moto uliowashukia wakiwa mwituni karibu kabisa na Kampala. Alice akaikimbia nchi.
Alikimbilia katika kambi ya wakimbizi ya Ifo karibu na Dadaab kaskazini mwa Kenya na akiwa huko alitangaza kuwa ametengwa na mizimu.
Novemba mwaka 2004 alituhumiwa kusafirisha watoto kutoka Gulu nchini Uganda na kuwapeleka kambini kwake. Hata hivyo, mkono wa sheria haukumshukia.
Miaka miwili baadaye Alice aliibuka na kudai kuwa amegundua tiba ya ukimwi. Hata hivyo, alishindwa kuishawishi dunia katika madai yake hayo. Amefariki dunia Januari 17 mwaka huu baada ya kuugua kwa wiki moja. Haijulikani kapoteza maisha kwa maradhi gani.
Kuna simulizi kwamba mwanamama huyo enzi za uhai wake alikuwa na tabia ya kusema na wanyama au maji juu ya kilichokuwa kikiendelea nchini mwake.
“Nyie wanyama, Mungu kanituma kwenu niwaulize kama mnahusika na mauaji ya Uganda.” Katika simulizi hizo, wanyama walimjibu kuwa hawahusiki na badala yake nao pia waliumia na vitendo hivyo. Ikasemwa kuwa nyati alimwonyesha jeraha mguuni huku kiboko akionyesha jeraha mkononi.
Inaelezwa pia kuwa aliwahi kuyauliza maji kuhusu vita nchini Uganda. “Maji, nimekuja kukuuliza juu ya dhambi na umwagaji damu katika hii dunia.”
Nayo maji yakamjibu kwamba binadamu wenye miguu miwili wana tabia ya kuua ndugu zao na kutupa miili yao majini.
Simulizi hizo zinapasha pia kuwa baada ya majibu hayo, mzimu ulimtuma Alice kuendelea na jitihada za kuleta amani nchini Uganda. Akomeshe dhambi na umwagaji damu.
Wakati fulani alipokwenda katika Mlima Kilak, Alice anadaiwa kupewa nguvu na mlima huo kwenda kuutokomeza udhalimu. Pia alikabidhiwa dawa maalumu ya kuponya wagonjwa.
Baadaye akaja kutangaza pia kuwa kuna ujumbe kutoka kwa Mungu kwamba lipo kabila nchini Uganda ambalo lina damu ya kunguni. Akalitaja kabila hilo kuwa ni la Acholi.
Mbali na jitihada zake hizo, marehemu Alice anafanana na Joseph Kony katika mambo mawili. Mosi wote wawili ni wapinzani wa Museveni na pili, wote wanachanganya dini na uovu.
Alice amewahi kuchanganya mizimu na neno la Mungu kama ilivyo kwa Kony ambaye wakati wa Mfungo wa Ramadhan hufunga ingawa hula nyama ya nguruwe ambayo kwa imani ya Kiislamu ni haramu.
Makala hii imeandaliwa na INNOCENT MUNYUKU kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari.
Sunday, April 29, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment