Na Innocent Munyuku
KATIKA maisha ni jambo la kawaida kwa mwanadamu kupenda mabadiliko chanya. Pengine hili liko kwa viumbe hai wengine.
Kutokana na hali hiyo bila shaka ndio maana bendi ya muziki wa dansi ya Mikumi Sound imeamua kuyaacha maskani yake mjini Morogoro na kuhamia jijini Dar es Salaam.
Katika taarifa yake juzi Meneja wa bendi hiyo, Yona Vegula alisema wameamua kuihamishia bendi hiyo jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujipanua.
“Kusudio au lengo hasa ni kupata changamoto, huwezi kujiita mahiri sehemu ambayo haina ushindani mkubwa katika masuala ya muziki wa dansi, kwa hiyo kuhama kwetu kunajengwa na msingi wa kusaka upinzani wa kweli,” alisema Vegula.
Kwa mujibu wa Vegula, Mikumi Sound itatua jijini Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa Pasaka.
Baadhi ya wanamuziki wanaounda bendi hiyo ni Sadiq Jakaya anayepiga gitaa la solo, Balely Mohamed anayevuma na gitaa la bass, Toto Site (kinanda), Abeid Said anayepiga drums huku Jose Kigenda ambaye ni rais wa bendi hiyo akiwa mtunzi.
Hadi sasa wanazo albamu tatu ambazo ni Cheo ni Dhamana ya mwaka 2004, Mama Mkwe (2005) na Pesa Makaratasi ya mwaka huu.
Kuibuka kwa bendi hiyo kulikuwa faraja kubwa kwa wakazi wa Morogoro hasa kutokana na ukweli kwamba baada ya kufifia kwa bendi maarufu mkoani Morogoro kama Moro Jazz iliyotamba na marehemu Mbaraka Mwinshehe, mkoa huo ulibaki kama yatima katika masuala ya muziki.
Sababu kubwa ni kwamba wadau wa muziki walikosa ari au uwezo wa kumiliki bendi za muziki wa dansi. Matokeo yake, burudani ya aina hiyo ikazidi kushamiri katika jiji la Dar es Salaam.
Umahiri wao jukwaani huwezi kuamiani kuwa bendi hii inaundwa na wanamuziki wenye usongo wa kujitangaza kimataifa.
Kinachofurahisha ni kwamba hawataki kuiga muziki wa Kongo na badala yake wanabuni vionjo vinavyokwenda na utamaduni wa Mtanzania.
Rais wa bendi hiyo, Jose Kigenda katika mahojiamo maalumu anasema kuwa wanamuziki wake wamekuwa wabunifu kutokana na maelewano baina yao.
Kwamba Mikumi Sound si ya wababaishaji na amewaomba mashabiki wa muziki wa dansi jijini Dar es Salaam kuwapa ushirikiano.
“Ndio maana kila siku nawaambia kuwa wanaodhani wamesimama kimuziki wakae chonjo, mwendo wetu ni wa taratibu lakini tuko makini sana,” anasema.
Ili kuhakikisha kuwa inabeba mashabiki wengi zaidi, bendi hiyo imeshazuru mikoa mbalimbali nchini kujitangaza. Moja ya ziara iliyofana ni ile ya kuitangaza albamu yake Mama Mkwe.
Hayo yote yasingewezekana kama si ubavu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Mikumi Sound, Rena Vegula. Huyu kwa watu wengine wanaweza kumwita mwanamke wa shoka kutokana na kutokuwa na woga katika uendeshaji wa masuala ya maendeleo.
Wazo la bendi lilianzia mjini Arusha mwaka 2003 na lengo hasa lilikuwa kuitangaza Mikumi kama mbuga nzuri Tanzania.
Bendi ilianza baada ya baadhi ya wanamuziki waliopo kushawishika na bendi ya Olduvai iliyokuwa ikipiga kwenye Ukumbi wa Ricks mjini Arusha. Baada ya bendi hiyo kufifia Rena akapata wazo na kuanzisha bendi yake ambayo ni Mikumi Sound.
“Baadhi ya wanamuziki wetu wakawa wanaonyesha moyo wa kuendeleza muziki lakini vifaa hatukuwa navyo, ndipo tukaamua kununua vifaa vyetu.”
Sunday, April 29, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment