na innocent munyuku
MAPEMA wiki hii nilikuwa mmoja wanahabari walioalikwa kuhudhuria kikao cha 17 cha Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) jijini Dar es Salaam.
Katika hotuba yake fupi kwa wajumbe wa Baraza, Mwenyekiti wa BASATA, Dk. Frowin Nyoni alizungumzia umuhimu wa wajumbe kuchangia ajenda zilizopo ili kuwa na maamuzi yenye kujenga sanaa nchini.
Mengi yalisemwa na wajumbe kuchangia ajenda hizo ambazo nyingi zilielekeza katika ukuzaji wa sanaa na kuinua hali za maisha ya wasanii Tanzania ambao wengi wao wanaishi kwa taabu.
Lakini moja ya hoja iliyonivutia katika kikao hicho ni azma ya BASATA ya kuifufua taarabu asilia hapa nchini.
Dk. Nyoni alitamka kuwa kwa miaka ya hivi karibuni wamebaini muziki wa taarabu asilia unapotea na wenye uwezo wa kuanzisha vikundi vya taarabu wamebadili ladha ya muziki huyo kwa kile kilichopewa jina la modern taarabu.
ÒTaarabu asilia imekosa mashabiki lakini bado ipo nafasi ya kuwahamasisha wananchi kuipenda taarabu,Ó alisema Dk. Nyoni.
Hata hivyo, Dk. Nyoni aliongeza kuwa kuna vikwazo vya muziki huo kusonga mbele na anavitaja kuwa ni pamoja na ukosefu wa ala halisi kwa ajili ya taarabu muziki.
ÒHatuna maduka ya vyombo vya asiliaÉkwa hiyo mtu mwenye kikundi chake atakimbilia Kariakoo kununua gitaa lake na kinanda, jioni anafanya onyesho.
ÒHakuna duka linauza vifaa kama vile violin au akodiani,Ó alieleza Dk. Nyoni.
Kauli ya Dk. Nyoni kuhusu kufufua muziki wa taarabu ikanikumbusha maneno ya rafiki yangu marehemu Issa Matona kwamba taarabu ilishapoteza mwelekeo.
Matona alipozungumza nami zaidi ya zaidi ya miaka mitano iliyopita alisema anapata uchungu mkubwa kwa kuona muziki wa taarabu unaharibiwa kwa kuleta kile kinachoitwa modern taarabu.
Nakumbuka Matona alisema ÒMuziki wa taarabu una miiko yake, taarabu haichezwi kwa kukata mauno kama ndomboloÉmashairi pia wameyaharibu. Siku hizi wanaimba matusi ya wazi wazi.Ó
Matona ambaye atakumbukwa kuwa mwanamuziki aliyebobea katika taarabu na mkali wa mashairi alikuwa akijaribu kuwahimiza wanamuziki kwenye reli hiyo waache kuuharibu.
Kwa upande wa BASATA, ukuzaji wa muziki huo umewekewa programu ya miaka minne (2006-2010). Mpango huo utagharimu shilingi bilioni 1.6.
Katika hilo, wasanii mbalimbali watahamasishwa ili kutimiza lengo la kuupa hadhi yake muziki wa taarabu asilia.
Kwa mujibu wa historia, muziki huo uliletwa Zanzibar na Waarabu wa Oman katika karne ya 19 wakileta vifaa, tungo na hata lugha iliyotumika ilikuwa ni Kiarabu.
Lakini pia miiko ya muziki huo ni kwamba si muziki wa kucheza kwa nguvu bali uliundwa ili usikilizwe.
Baadaye watunzi wa Kizanzibari nao walianza kutunga mashairi wakitumia Kiswahili kwa kutumia melodia za Kimisri na Kihindi na inaaminika kuwa mwaka 1930 muziki huo ukaingia Tanganyika na kujikita katika miji ya Morogoro, Dodoma, Tabora, Mwanza na Kigoma.
Tangu wakati huo, muziki huo ulianza kukua na kuenea sehemu nyingi za Tanzania lakini kwa bahati mbaya uasili wake ukaanza kupotea siku hadi siku.
Kumekuwa na matatizo yaliyochangia muziki huo ukafa kama ilivyodokezwa awali lakini vikwazo vingine ni ukosefu wa wawekezaji na udhaifu katika uongozi na utawala.
Pamoja na matatizo hayo, BASATA imeweka mkakati maalumu wa kuboresha ufahamu na taaluma na kuhakikisha kuwa upatikanaji wa vifaa vya muziki huo hauwi kikwazo tena.
Lakini pia imepangwa kufanya uwekezaji na kutenga mfuko maalumu wa kusaidia ukuaji wa muziki wa taarabu asilia.
Sunday, April 29, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment