Sunday, April 29, 2007

Zemkala: Twatetea utamaduni wa Mtanzania

Na Innocent Munyuku

NAWAITA marafiki wa sanaa lakini wao hujiita Zemkala. Hili ni kundi la muziki asilia lenye maskani yake jijini Dar es Salaam.

Nimeshakutana nao mara nyingi katika matamasha mbalimbali. Pia wakati mwingine hujumuika nao kwenye mazoezi yao.

Ijumaa ya Aprili 6 mwaka huu nilikutana tena na wasanii hawa katika Ukumbi wa Hoteli ya Rombo Green View barabara ya Shekilango jijini Dar es Salaam. Walikuwa hapo kupendezesha hafla ya kuwatunuku waandishi bora wa habari za utamaduni na sanaa kwa mwaka uliopita.

Tofauti na nilivyowaona kiasi cha miezi miwili nyuma, Zemkala wamepaa. Wameongeza uwezo katika nyanja mbalimbali kama vile kutawala jukwaa na vyombo pia.

Moyo wangu ulifarijika kuona kuwa kile walichonieleza zaidi ya mwaka mmoja uliopita kuwa wameingia ulingoni kwa ajili ya kuhakikisha wanautangaza utamaduni wa Mtanzania.

Lakini mbali na hili walichonieleza siku ya kwanza kuonana nao ni kwamba wanalenga pia kujikwamua kimaisha na kuachana na mpango wa kukaa vijiweni kupiga soga.

Ni kundi linaloundwa na wasanii wanane ambao bado umri wao haujavuka miaka 30. Wangali na damu mbichi katika kueneza mila na utamaduni wa Mtanzania katika nchi mbalimbali duniani.

Wanaounda kundi hilo ni Yuster Nyakachara, Havintishi Baraza, Fadhili Mkenda, Yusuf Chambuso, Maulid Mastir, Kasembe Ungani, Shabaan Mugado na Fred Saganda.

Uzuri wa kundi hili ni kwamba karibu kila msaani ana uwezo wa kuimba, kupiga ala.

Kundi lilianza kupata uhai mwaka 2002, waanzilishi wakiwa Ungani na Mkenda. Hawa walijiengua kutoka Sisi Tambala.

Ni zaidi ya miaka minne sasa tangu liibuke na kwa hakika unapozungumza nao wanasema kila siku inaleta neema mpya.

Hilo lina ukweli kwani wameshasafiri katika nchi mbalimbali kuitangaza Tanzania kupitia ngoma na sauti zao za kuvutia.

Wameshafanya maonyesho Sweden, Msumbiji, Kenya na Zanzibar na katika ziara zote hizo wameacha gumzo kwa mashabiki wao.

Wanachosema Zemkala ni kwamba ifike siku Tanzania ijulikane kupitia ngoma zake kama walivyofanikiwa Wakongo au mataifa ya Afrika Magharibi.

Daima wanajivunia asili yao na utamaduni wa Kiafrika. Hawajatafunwa na utumwa wa akili. Wangali na fikra pevu.

Hushangaa kuona baadhi ya Watanzania hasa vijana wanakataa kucheza ngoma za asili na badala yake kukimbilia disko na kuiga utamaduni wa Kimagharibi.

Lakini kinachowasikitisha zaidi ni kwamba wananchi wengi hawana utamaduni wa kwenda kuangalia ngoma za asili.

“Hapa hakuna ari ya kupenda hizi ngoma, watu wanapenda muziki wa dansi au disko,” anasemaYusta ambaye ni kiongozi wa Zemkala.
“Hakuna kulala tutapigania haki zetu na utamaduni wa Mtanzania na bara la Afrika,” anasema Yusta.

Zemkala ni neno la Kiyao likiwa na maana ya maendeleo. Kwa namna hiyo vijana hawa hawana masihara katika kusaka ujira wao wa kila siku.

No comments: