Na Innocent Munyuku
WAHENGA walipata kusema kuwa penye nia pana njia. Hivyo ndivyo ilivyo kwa mwanamuziki wa kujitegemea Abiud Sikapizye wa jijini Arusha.
Gitaa lake aina ya galatoni na uwezo wake wa kuimba nyimbo za wasanii wengine duniani ndiyo silaha yake katika vita ya kuelekea maskani ya mafanikio.
Kazi zake anafanyia katika baa mbalimbali jijini Arusha na kwa hakika ni maarufu kwa wakazi wengi wa jijini humo. Ni hodari katika kuimba nyimbo zilizowahi kuvuma zamani na hata zinazoendelea kufyatuliwa miaka hii.
Omba wimbo wa Daudi Kabaka, Bob Marley, Simba wa Nyika, Lionel Richie au Moro Jazz hatasita kukupa burudani kwa gharama ya Sh 500 kwa kila wimbo.
Nilipokutana naye jijini Arusha siku chache zilizopita niliduwazwa na uwezo wa mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 32.
Lakini cha kufurahisha ni kwamba mwanamuziki huyo aliamua kuachana na matakwa ya babaye ya kulitumikia kanisa. Baba wa Abiud wakati huo alikuwa Mchungaji wa Kanisa la Moravian Jimbo la Mbeya.
“Nilianza muziki nikiwa darasa la nne. Baadaye nikaanza kupiga ngoma kanisani na kujaribu kupita gitaa pia,” anasema Abiud.
Anapozungumzia kilichomtumbukiza kwenye muziki ni kitu gani, anaeleza kuwa alivutiwa na uimbaji wa Dk. Remmy Ongala.
Mara baada ya kumaliza elimu ya sekondari kidato cha nne Mbozi mwaka 1991, msanii huyo alitimkia mjini Morogoro kwa ajili ya kusaka maisha bora.
“Niliondoka nyumbani kwani niliona kama nina nafasi ya kujitafutia maisha sehemu nyingine. Hivyo nikaenda Morogoro nikafikia kwa mama mdogo.
“Huko ndoto yangu ya muziki ikawa bado ipo lakini hakuna wa kuniongoza na sikuwa na fedha za kuanzisha bendi.
“Nilichofanya ni kuuza chips na wakati mwingine kuuza machungwa mitaani,” anasema.
Anaeleza kuwa matarajio yake yakaanza kufifia na hivyo kuchukua uamuzi wa kubadili makazi. Safari hii akapanda basi hadi jijini Arusha Mei mwaka 1995.
Mwaka mmoja baadaye akapata bahati ya kuimba kwaya katika Kanisa la Moravian na kwamba huo ukawa mwanzo wake wa kufufua ndoto zake.
Mwaka huo akakutana na mtu anayemtaja kwa jina moja la Fadhil aliyemwongezea mwanga katika fani ya muziki.
Lakini vile Mbeya alitoroka, babaye mzazi akamlazimisha arejee huko. Akatii amri ya baba lakini kichwani mwake akiwa na nia ya kutokaa huko kwa muda mrefu. Hakukaa sana Mbeya na badala yake akaelekea jijini Dar es Salaam.
“Nilichonga gitaa langu nikaelekea Dar es Salaam lakini kwa bahati mbaya pesa niliyokuwa nayo ikaishia kulipa malazi kwenye nyumba ya kulala wageni.
“Nikaona hali inakuwa ngumu, sikukata tamaa nikawa napiga baa mbalimbali na kwa vile sikuwa na pesa nilikuwa nalala Kwa Macheni…nakesha hapo kwa sababu nilishatimuliwa kwenye chumba.
“Mwaka 1997 nikalazimika kurudi Mbeya, huko nikakuta shinikizo kwamba lazima nioe. Nikakubaliana na wazazi na Novemba 27 mwaka huo huo nikafunga ndoa kanisani na mke wangu Neema Silungwe.”
Anasema alipoona hali ya maisha ya kijijini ni ngumu akatamani kurudi Dar es Salaam. “Bahati nzuri kulikuwa na Mchungaji wa kanisa anahamishiwa Arusha, tukadandia gari lake nasi tukashuka Chalinze ili tuunganishe usafiri kwenda Dar es Salaam.”
Kwa vile alishaanza kuzoea mji akaamua kupanua maeneo ya upigaji gitaa. Akapiga maeneo ya Masaki, Coco Beach akiwa na msaidizi wake.
“Siku moja wakati nawajibika pale Rose Garden, mwanamke Mzungu raia wa Norway akathamini sana kazi yangu, akaniahidi kunipa gitaa la kisasa na akatimiza ahadi.
“Tenda zikawa nyingi, nikapiga Casanova, Shivers na kwa vile kazi ilikuwa inalipa, tukakodi vyombo ili kuweka vionjo vingine vya muziki.
“Lakini kwa bahati mwenzangu akarubuniwa na watu akajiondoa na kunidhulumu gitaa langu. Nikaamua kuja Arusha ambako Mungu alinishika mkono nikapata mkataba wa kupiga Hotel 77,” anasema.
Baadaye mkataba huo ulikoma na alichofanya ni kurejea mtaani kupiga sehemu mbalimbali.
Ameshaandaa nyimbo kwa ajili ya kutoa albamu yake ya kwanza lakini tatizo ni mtaji wa kumwezesha kuingia studio.
Sunday, April 29, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment