Na Innocent Munyuku
NIMESHAKUTANA naye zaidi ya mara tatu akiwa katika pilika zake za kurekodi nyimbo studio. Lakini kwa bahati mbaya sikuwahi kupata muda wa kuteta naye kwani mara nyingi ni msanii wa pilika tele.
Huyo ni mwanamuziki wa reggae anayekuja kwa kasi nchini anayekwenda kwa jina la Pestman. Lakini mara zote hizo tunaposalimiana nadhani kwamba msanii huyo ni raia wa Jamaica kutokana na lafudhi yake. Kiingereza anachokitumia hakina tofauti na kile cha Wajamaica.
Jumatano wiki hii nilifanya mahojiano na Pestman ambaye jina lake halisi ni Dennis Mwakyanjala ambaye ana umri wa miaka 25.
“Kaka hapa nilipo watu walishaniita mimi kuwa ni Mjamaica, wengine wakasema mimi ni Mganda na wapo wanaodhani kuwa ni Mkenya na wengine wanasema mimi natoka Malawi.
“Lakini ukweli ni kwamba mimi Mnyakyusa wa Bujonde Kyela, mama yangu ni Mndali na baba Mnyakyusa kwa hiyo mimi ni Mtanzania halisi,” anasema Pestman.
Kwanini akadhaniwa kuwa si Mtanzania?
“Nimepata elimu yangu ya sekondari nchini Malawi wakati huo nilikuwa nikipenda pia muziki wa hip hop na wala sikuwahi kujua kama nitaingia katika reggae.
“Nilipenda maikrofoni sana nikaanza kuiga nyimbo za kina BIG, Scarface na Black Positive Soul na kazi yangu ilikuwa ni kukusanya kaseti za wasanii hao na kuiga staili zao.
“Sasa likizo moja nikiwa Mbeya wakati nikisaka kaseti za hip hop nikakutana na kaseti moja imeandikwa BB hii ilikuwa ya msanii wa ragga Buju Banton nikainunua.
“Nilipoisikiliza nikalipuka moyo kwani nilipata kitu kipya kwa hakika moyo ukadunda kutokana na namna alivyokuwa akiimba nilipenda sana mtindo na lugha ya Banton,” anasema Pestman na kisha kuongeza:
“Kuna rafiki yangu Nick Mrenga huyu alikuwa akijiita Iron Man akanipa maneno ya Kiingereza cha Jamaica, ndugu zangu walinicheka lakini baada ya muda mfupi wakatamani kuzungumza kama mimi.”
Anasema hata aliporejea Malawi kuendelea na masomo katika Shule ya Sekondari ya Livingston lafudhi yake iliendelea kuwa ya Kijamaica.
Akiwa huko alitunga wimbo wake wa kwanza wa reggae uliojulikana kama Thabita Carina. “Niliuandika kwa penseli nakumbuka,” anasema.
Kutokana na umahiri wake katika uimbaji, alipata mashabiki wengi shuleni kwake na hivyo kuwa nguli wa muziki katika matamasha mbalimbali.
“Lazima nikiri kwamba wanafunzi wenzangu walinipenda sana na nilikuwa mahiri katika uimbaji na hivyo kujitengenezea marafiki wengi.
“Hata nilipohitimu kidato cha nne mwaka 2001 mwalimu wangu wa burudani aliniambia kuwa watakumbuka sana mchango wangu. Hii ilinifariji na kuona kuwa nina mwendo mzuri katika sanaa.”
Alirejea nyumbani nchini Tanzania lakini baada ya muda mfupi akaamua kurudi Malawi kumfuata binti ambaye alidhani angekuwa naye katika mapenzi badala yake mpenzi wake huyo alichukuliwa na jamaa mwingine.
Anasema akiwa huko akajiunga na kundi la muziki la Royal House of King David lililoundwa na vijana wenye itikadi ya Kirasta. “Maisha yalikuwa magumu kutokana na kipato kutotosheleza lakini kilichonichanganya zaidi ni uhusiano mbaya na mpenzi wangu.”
Baada ya kuona mambo hayaendi sawa Pestman aliamua kuunda kundi lake la muziki lililojulikana kama The Son of Moses na wakati fulani alifanikiwa kutumbuiza kwenye tamasha la Cross Roads.
Pamoja na hilo akaona kuwa kuna umuhimu wa kurudi nyumbani Tanzania na kuendelea na muziki.
“Nilipoingia tena Tanzania niliimba wimbo wa ‘Njoo Mpenzi’ huu wimbo ulikuwa ukielezea namna nilivyokuwa namhusudu msichana mmoja ambaye hata hivyo alikuwa anafuatwa na kijana mwingine.
“Nilishinda na niko naye hadi hii leo. Kilichofuata nikaimba wimbo mwingine niliouita ‘Mpenzi’ katika wimbo huo nilikuwa naweka ahadi kwamba sitaimba tena juu ya mapenzi,” anasema Pestman.
Mwaka 2005 aliibuka na kibao cha Rise Ghetto Yut. Lakini wimbo aliutunga baada ya kupata kisanga cha aina yake maeneo ya Mwenge jijini Dar es Salaam.
“Nilikuwa Mwenge alfajiri moja hivi namsubiri dereva wa lori twende tukabebe mchanga kuupeleka uwanja mpya wa taifa kwa ajili ya ujenzi.
“Sasa nikiwa pale wakaja wahuni wakanizunguka. Nikawaambia mimi pia ni mtu wa ghetto kwa hiyo wasiniumize wachukue wanachotaka lakini waniachie uhai wangu.
“Wakanisachi wakabeba na simu yangu lakini walipoondoka nikahisi baridi mkono wangu wa kushoto, nilipoangalia nikaona damu zinatoka kumbe walishanichanja na wembe.
“Sikushangaa sana kwani katika maisha ya aina ile lazima umtoe mtu damu japo kidogo ile ni imani yao,” anasema.
Hata hivyo, Pestman hakuripoti polisi na badala yake akaamua kutunga wimbo wa Rise Ghetto Yut akiwataka vijana kuamka na kufanya kazi halali.
“Nilijiuliza kwanini wanaishi hivi? Nilishangaa lakini baadaye nikabaini pia kuwa vijana hawajasaidiwa kiasi cha kutosha…hawa wanaona giza mbele yao na ndio maana wengine wanatumia bunduki kuishi,” anasema Pestman na kuongeza kuwa hakuna kijana anayependa kuishi maisha hayo bali wanalazimishwa na shida za maisha.
Msanii huyo kwa sasa ni mmoja kati ya wasanii waliopo kwenye programu ya kuibua vipaji vya reggae nchini chini ya Umoja Records.
Tayari ameshiriki katika albamu ya kwanza ya mpango huo iitwayo Bongo Riddims and Style (I) yenye nyimbo 12.
Pestman ameimba Kneel & Pray akielezea umuhimu wa kusali na kwamba kila unaposali Mwenyezi Mungu anajibu kwa mema.
Anawaasa watu kujenga tabia njema ya kumkumbuka Mungu katika pilika zao za kila siku na kwamba kwa njia hiyo kila kitu kitakuwa sawa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment