Monday, September 3, 2007

Kiswahili ni chetu, tukikumbatie

Na Innocent Munyuku

“SIKUTARAJIA kukuta mkusanyiko mkubwa wa watu kiasi hiki. Nimezoea mikusanyiko mikubwa kama hii huwa katika majadiliano ya Kiingereza.”

Hiyo ilikuwa kauli ya Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Muhammed Seif Khatib aliyoitoa Jumatano wiki hii mara baada ya hotuba yake wakati wa uzinduzi wa kamusi ya Kiswahili kwa shule za msingi iliyochapishwa na Shirika la Uchapaji la Oxford University Press East Africa Ltd.

Alipomaliza kutamka kauli hiyo ambayo ilijaa utani, wageni waalikwa kwenye Ukumbi wa Kibo wa Hoteli ya Kilimanjaro Kempinski waliangua kicheko.

Bila shaka kicheko kilimaanisha kukubaliana na hoja ya Waziri Khatib kwamba katika mikutano mingi nchini, si ajabu kusikia ikiendeshwa kwa Kiingereza hata kama wanaohudhiria mikutano hiyo ni Watanzania.

Hatutaki tena kusikia Kiswahili kikitumika katika hafla hizo na kwa mtazamo wangu wanaoendesha mikutano lengo lao kuu ni kuwapa wepesi wa kuelewa wageni kutoka ughaibuni ambao kwa uzoefu wangu idadi yao haizidi Watanzania ukumbini hapo.

Hili si jambo la kuendelea kulikumbatia kwa sababu madhara yake ni makubwa. Leo hii Watanzania tumefika mahala tunakidharau Kiswahili kwa makusudi.

Watanzania wengi sasa wanadhani kwamba kuwasiliana kwa Kiswahili ni ishara ya udumavu wa akili. Si ajabu mtu kuchekwa pindi atakapojieleza kwa lugha hiyo.

Pengine hao wamesahau kwamba kujua Kiingereza si ishara ya ustaarabu. Kuifahamu lugha hiyo si kielelezo kwamba wewe ni makini kuliko wote. Au mwataka kusema kuwa hamjui kwamba hata kwenye chimbuko la Kiingereza wapo wendawazimu wanaowasiliana kwa lugha hiyo?

Ninachotaka kusema hapa ni kwamba isifike mahali tukazidi kukidharau Kiswahili kwa mtazamo hasi. Ni vema kujifunza lugha nyingine za kimataifa lakini wakati huo huo tuhakikishe kwamba lugha yetu inakuzwa.

Kwa mlolongo huo hatuna budi kukikuza Kiswahili na kama alivyoasa Waziri Khatib kwamba mbali na kamusi hiyo kwa ajili ya shule za msingi, zinahitajika pia kamusi ndogondogo katika fani na nyanja mbalimbali zinazoelezea istilahi za maeneo hayo.

Kwamba kwa njia hiyo itakuwa rahisi kwa mtu kutafsiri kwa Kiswahili maelezo yaliyoandikwa kwa lugha ya kigeni hasa katika fani mbalimbali.

Kuna haja ya kujivuani Kiswahili kwa vile kinazidi kuenea katika maeneo mbalimbali ndani ya bara la Afrika na katika mabara mengine.

Ni jambo lililo wazi kwa Watanzania wengi kwamba lugha yao inapanda hadhi kwani leo hii ni moja ya lugha rasmi katika Umoja wa Afrika na miaka michache ijayo kitaingia katika Jumuiya ya SADC.

Kama alivyosema Waziri Khatib kwamba kukua kwa kasi kwa lugha hii kote duniani kunahitaji misingi imara na moja ya nguzo ni kuzitumia kamusi.

“Jamii ielewe kwamba kamusi ina matumizi mapana na kwa sababu hiyo ingefaa kila familia iwe na kamusi zaidi ya moja kwa ajili ya kujifunza,” alisema Khatib.


Mbali na maneno ya Waziri Khatib kingine kilichonivuta kuandika makala hii ni maoni kutoka kwa mmoja wa wataalamu wa Afrika Mashariki, Sheikh Abdillah Nassir aliyetahadharisha kwamba Kiswahili kinapoteza uasili wake.

Kwamba kila siku watumiaji wa Kiswahili wanapotosha kwa kuzungumza Kiswahili cha Kiingereza. Ametoa mifano ya vituo mbalimbali vya redio vya kimataifa ambavyo vinatumia Kiswahili kwa upotoshaji.

Alichokuwa akisema Sheikh Nassir ni kwamba ujenzi wa Kiswahili sasa unategemea nguzo nyingi kutoka katika Kiingereza jambo ambalo ni hatari kwa ukuaji wa lugha yetu.

Hii ni hatari kwa kizazi hiki na kijacho kwani kama mambo yataendelea kwa kasi hii ipo siku lugha hii ikapotea kwa muda mfupi. Tukijenge Kiswahili kwa dhamira moja kwa manufaa ya kulinda historia yetu.

Kukiacha Kiswahili kipotee ni sawa na kuukataa umoja wetu. Kuachana na lugha hiyo hakuna tofauti na kujikana. Twahitaji kukienzi kwa manufaa ya jamii.

Tukifanikiwa katika Kiswahili naamini tutadhibiti mambo mengine potofu yanayoinyemelea Afrika Mashariki na bara zima la Afrika.

Tutaachana kuamini kuwa kila kitokacho Amerika au Ulaya chafaa kuigwa na kupandikizwa katika jamii zetu.

Kuishikilia lugha yetu ni silaha mojawapo katika kujenga umoja wetu na kuthibiti udhalimu katika kaya zetu. Kujitambua katika masuala hayo ni ushindi kwa wanaotudharau.

Kujitoa kwa moyo wa dhati kulinda mambo yetu ni ishara ya kuharakisha maendeleo binafsi na ya taifa. Kiswahili ni chetu, tukikumbatie.

No comments: