Monday, September 3, 2007

Bongofleva imeguswa mboni?

Na Innocent Munyuku

MBONI ni sehemu ndani ya jicho na kwa kawaida huzungukwa na duara nyeusi inayorekebisha mwanga.

Hakuna aliyepata kuguswa mboni kutokana na ukweli kwamba sehemu hii ikinyemelewa na kitu kigeni basi jicho hulazimika kuziba.

Wiki iliyopita katika safu hii Mzee wa Busati aliandika juu ya umuhimu wa wanamuziki wanaochipukia kujua sheria za hakimiliki. Kwamba wasanii wengi hasa wa kizazi kipya hawajui ama hawataki kujua.

Mwenye Busati akatoa mifano kwamba kuna baadhi ya watayarishaji wa muziki ambao pengine nao kwa kutojua sheria wanadiriki kuiba midundo ya muziki kutoka katika intaneti.

Mwandika Busati hakuishia hapo akasema pia kuwa wanamuziki hawana budi kujifunza kupiga ala za muziki na si kutegemea utaalamu wa kompyuta pekee. Hoja ikawa kwamba ubunifu usisahaulike.

Wenye bongofleva yao wakaja juu. Wengi wakatuma ujumbe kwa njia ya simu na mmoja wao aliyekuja juu ni jamaa aliyejiita Masalu kutoka Mwanza.

Kwamba Mzee wa Busati hakutenda haki kwa wasanii wa kizazi kipya kwani nimejenga ukuta wa ubaguzi. Masalu na wengine hawakunielewa.

Hata pale walipoombwa warejee mstari kwa mstari wakatuma tena ujumbe wakisisitiza kwamba Mzee wa Busati hajatenda haki.

Haikuwa nia ya waraka uliopita kuwatenga wasanii hao na kamwe haitakuja kutokea wakatengwa kwa makusudi. Hilo halitafanyika kwa sababu Mzee wa Busati anaamini mchango wao kwa jamii.

Kinachosisitizwa ni ukomavu katika ubunifu na kulinda haki zao ili huko mbele ya safari wasije kuumbuka. Je, kuwakumbusha mema ni kosa?

Bila shaka kimeleeweka na kwa wakati huu Mzee wa Busati hana jingine la kujadili zaidi ya shangwe iliyoletwa na timu ya taifa, Taifa Stars.

Tuseme nini zaidi ya kunena furaha. Ndimi zimejaa maneno ya furaha na hata uchungu wa bajeti umepoa japo kwa siku chache.

Taifa Stars imebadili mambo. Yaliyokuwa yakionekana kuwa magumu kwa Wabongo sasa ni laini kama mshumaa kwenye joto.

Ni chereko zilizotokana na kuinyamazisha Burkina Faso kwa kuinyuka bao 1-0 kwenye ardhi yao ya nyumbani na hivyo kuipa mwanga Stars kuendelea kuikaribia ardhi ya Ghana katika fainali za Kombe la Mataifa Afrika.

Kasi hii kwa timu yetu ni ishara njema kwa mustakabali wa soka ya Tanzania. Kiasi cha miaka saba nyuma au tuseme zaidi ya hiyo haikuwa rahisi kwa Watanzania kuishabikia timu yao.

Kila ilipotinga dimbani walikuwa wakiibeza kwani hawakuwa na imani nayo. Walisikika wakisema ‘aah mambo ni yale yale…kichwa cha mwendawazimu’.

Hata wauza magazeti walipata wakati mgumu siku Stars ilipoingia dimbani. Mauzo yalikuwa mabovu. Nani anunue gazeti wakati timu ishalamba mchanga? Siku hizi hata magazeti makubwa yanapeleka habari za Stars ukurasa wa mbele kwa vichwa vya habari vyenye wino mzito. Hii ni ishara kwamba mambo sasa yanakwenda vizuri.

Lakini Mzee wa Busati anaomba aseme jambo moja katika sherehe hizi za Stars. Kwamba badala ya kubaki kushangilia tu iwekwe mikakati sasa ya kujenga vitalu vya soka.

Kubaki kushangilia tu hakutakuwa na maana yeyote. Badala yake itageuka hadithi ya mama ambaye kwa miaka mingi alilia kupata mtoto bila mafanikio. Siku alipojifungua akaacha kumhudumia mtoto na kwenda kwa majirani akitangaza kwamba safari hii kapata mtoto.

Akasahau kuwa mtoto mchanga alihitaji uangalifu wa hali ya juu. Aliporejea kutoka kutangaza furaha yake ya kupata mtoto akakuta kichanga kimeshafariki dunia. Furaha ikageuka matanga.

Kwa mfano huo furaha ya Stars isiishie kula pilau na soda za baridi. Tuwakumbushe vinara wa Shirikisho la Soka Tanzania-TFF kwamba huu ni wakati wa kuitayarisha timu nyingine ya taifa. Hawa waliopo wanakaribia kufika ukomo.

Na kwa vile timu hii imepata bahati ya kupendwa na Mkuu wa Kaya pale kwenye jengo jeupe sehemu ya Magogoni jijini Darisalama basi tuutumie mwanya huu kunyanyua soka nchini.

Huu mpango wa kuyapunguza mashangingi umepokewa kwa shangwe na Mzee wa Busati kwani anaamini fedha sasa zitakwenda moja kwa moja katika mahitaji ya walalahoi na moja ni kujenga michezo.

Huu mpango wa kupunguza semina nao hakuna shaka kwamba fedha zitakazookolewa zitakwenda sehemu nyingine ikiwemo soka. Tuitumie nafasi hii vema.

Mzee wa Busati anafika mwisho kwa juma hili. Wiki iliyochanganyika furaha na shubiri. Mjadala wa bajeti na ushindi wa Taifa Stars.

Wasaalam,

No comments: