Monday, September 3, 2007

Lucy Kihwele: Akumbuka alivyopokwa taji Miss Tanzania 1994

na innocent munyuku

IJUMAA ya Oktoba 6 mwaka huu nainua simu kumjulia hali mwanamama ambaye kutokana na pilika za jiji la Dar es Salaam sijamtia machoni kwa miaka kadhaa. Huyu ni Lucy Kihwele ambaye kwa furaha ananieleza kuwa siku ya pili yake anatimiza miaka 11 ya ndoa yake na Beraldo.

Kabla ya ndoa hiyo iliyofungwa Oktoba 7, mwaka 1995 katika Kanisa la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam, mwanamama huyo alijulikana kama Lucy Tabasamu Ngongoseke. Mrembo aliyepamba kurasa za magazeti mbalimbali ndani na nje ya nchi kutokana na ushiriki wake katika medani ya urembo.

Ni mmoja wa warembo walioshiriki mashindano ya Miss Tanzania kwa mara ya kwanza mwaka 1994 tangu yapigwe marufuku na Serikali katika miaka ya 1960 kwa maelezo kuwa hayakuwa na mema katika kuendeleza mila ya Mtanzania.

Kujiamini kwake na namna alivyokuwa amejiandaa katika mashindano hayo mwaka huo kuliashiria mengi katika kambi yake na kubwa ni kwamba angeweza kuibuka na taji la Miss Tanzania. Lakini kwa bahati mbaya haikuwa hivyo kwani aliishia nafasi ya pili huku nafasi ya kwanza ikienda kwa Aina Maeda.

Hadi hii leo Lucy anasema ushindi wa Aina ulikuwa na kigugumizi kwani aliingia katika kinyang’anyiro hicho zikiwa zimesalia siku tatu kabla ya fainali. “Nashukuru kwamba nilipata nafasi ya pili lakini mimi na wenzangu tulishangaa mtu anakuja kambini siku tatu kabla ya mashindano na anakuwa mshindi..kwa nini hakupitia hatua tulizopitia sisi, nadhani haikuwa sahihi kwa kweli,” anasema Lucy.

Pamoja na uchungu huo Lucy anabaki kuwa mmoja wa warembo wa Tanzania ambaye hadi sasa anasikika katika huduma za jamii kwa nafasi yake ya Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Multi Choice alikoajiriwa tangu Agosti mwaka 1997 akitokea Dtv ambako alifanya kazi ya utangazaji, mauzo na utawala kwa nyakati tofauti.

Kuhusu rushwa ya ngono katika mashindano ya urembo nchini, Lucy anasema kuwa mambo kama hayo yanakuwa hayana ushahidi na kwamba kama yapo wanaotakiwa kuyakemea ni washiriki wenyewe.

“Huwezi kupata ushahidi, mimi nasikia kwamba yapo lakini siwezi kuthibitisha na nikizungumzia kwa upande wetu sisi hapakuwa na mambo kama hayo,” anasema.

Kuhusu kuboronga kwa warembo wa Tanzania kwenye mashindano ya Miss World, Lucy anasema lazima hatua za makusudi zichukuliwe hasa katika kuangalia warembo wenye vipaji.

“Tusikate tamaa lakini ukweli ni kwamba tuwapeleke wasichana wenye vipaji na watafute vigezo vya kimataifa. Mrembo awe na vipaji walau viwili na hapa ieleweke kuwa kipaji si kuimba na kucheza muziki pekee.

“Lakini pia kuna tatizo jingine katika safari ya kwenda mashindanoni, sisi watazamaji tumekuwa tunawafanya hawa watoto wayumbe kwa kuwalazimisha wazungumze Kiingereza jukwaani.

“Tunawasukuma waseme Kiingereza hata kama hawakijui kwa upana zaidi, msichana akizungumza Kiswahili anachekwa…hii inashangaza sana.”

Pamoja na uelewa wake wa masuala ya urembo, Lucy mama wa watoto wawili anakerwa na mabinti wanaoshika mimba huku wakiendelea na masomo yao.

“Hili jambo linanikera sana na kwa hakika linanisumbua moyoni. Huwa najiuliza inakuwaje msichana apate mimba wakati akijua kuwa ana masomo yanamkabili?

“Na mpango kwamba wakishapata mimba waondoke shuleni na kisha warejee na kuendelea na masomo ni sawa na kumwaga petroli kwenye moto. Watazoea na wasichana wengine wataona kuwa ni jambo la kawaida.

“Unaporuhusu jambo la aina hiyo ni wazi kuwa unatetea pia maambukizi ya ukimwi. Mimi nawashauri hawa watoto wachague jambo moja shule au mimba na wajue kuwa mimba wawaachie wenye ndoa.”

Anasema kwa vile wavulana wanaohusika na mimba hizo huendelea na shughuli zao na wengi wao pasipo kubughudhiwa, hilo linaweza kuwa funzo kwa wasichana kuacha ngono zembe kwani ni wao ndio wanaokosa mtiririko mzuri wa masomo yao.

“Kwa mfano mvulana aliyempa mimba binti anaendelea na masomo na msichana analea mimba na baadaye mtoto sasa hapo kwa akili ya kawaida binti lazima ajifunze kuwa suala la kukimbilia maisha ya aina hiyo lazima liepukwe,” anasema Lucy.

Lakini kwa upande mwingine Lucy anaeleza kuwa wazazi wanastahili lawama kwa mimba za utotoni pamoja na maambuziki ya magonjwa kwa watoto. Kwamba wapo wazazi na walezi ambao hawajishughulishi na utoaji wa elimu ya uzazi kwa mabinti zao.

“Si jambo geni, wapo kina mama ambao hadi sasa hawako tayari kumweleza binti hali ya maungo yake na jinsi yanavyofanya kazi, wanaona aibu. Sasa aibu hiyo ndiyo inayosababisha watumbukie katika mimba zisizotarajiwa.

“Mabinti wengi wanarubuniwa na wanapojaribu wanajikuta wameshanasa kwa sababu hawakuwa na elimu ya uzazi. Hawajui jinsi ya kujikinga,” anasema.

Pamoja na hilo amewaasa wasichana kutokubali kuingia katika mtego wa wanaume wanaotaka wawape mimba kabla ya ndoa. “Kama anakupenda kwa dhati atakusubiri na ukiona mtu anakimbilia uzazi kwamba jua kuwa hana mapenzi ya kweli.

“Binafsi nilianza uhusiano na Beraldo tangu mwaka 1984 tukafunga pingu za maisha mwaka 1995, miaka 11 baadaye. Wazazi na ndugu wakatarajia kuwa baada ya ndoa tu tungeanza kuzaa, nikawaambia kuwa sijafuata kuzaa bali mapenzi.”

Lucy alizaliwa miaka 34 iliyopita huko Magu mkoani Mwanza na alipata elimu yake ya msingi Shule ya Msingi Kinondoni na Lyalamo iliyoko Tosamaganga, Iringa. Alisoma shule ya Sekondari ya Wasichana ya Masasi na Jangwani na mwaka 1987 alikwenda nchini Marekani kwa elimu ya juu.

Ana watoto wawili Regina mwenye umri wa miaka minane na Reginald mwenye umri wa miaka minne.

Mbali na mapenzi makubwa kwa familia yake, Lucy ni mpenzi wa kuimba, kupika, safari na kupumzisha mwili wake katika pwani ya bahari au ziwa.

“Lakini katika kuimba huwa napenda kufanya hivyo nikiwa bafuni,” anasema na kisha kuangua kicheko kinachohitimisha mazungumzo baina yangu na mwanamama huyo ambaye ni mcheshi na sura ya tabasamu kwa muda mrefu.

No comments: