Na Innocent Munyuku
YAWEZA kusemwa kwamba ni mtu wa watu kutokana na ukweli kuwa ni mwanaharakati ambaye daima ameonyesha dhamira katika kila anachokisimamia.
Huyu ni Richard Mabala ambaye kwa muda mrefu amekuwa mstari wa mbele kutetea haki za binadamu akishirikiana asasi mbalimbali za jamii.
Wiki hii MTANZANIA Jumapili imefanya mahojiano na Mabala na ameelezea mengi juu makuzi ya vijana, maambukizi ya ukimwi na ahadi za Serikali ya Awamu ya Nne kwa wananchi.
Akizungumzia ongezeko la ugonjwa wa ukimwi, Mabala anasema tatizo kubwa linatokana na malezi katika jamii nyingi hasa kwa kaya za kimasikini.
“Kwa mfano maeneo hayo si ajabu kusikia baba anamwambia bintiye mdogo kabisa akafanye maarifa ya kuleta mkate kwa familia.
“Sasa unajiuliza huyu binti mdogo anafundishwa nini? Kwa hiyo hapo ni wazi kuwa binti anakuwa anafundishwa umalaya. Atatoka kwenda mitaani kusaka chochote kwa ajili ya familia.
“Wakati mwingine utasikia msichana anaambiwa ‘aah mbona umeukalia uchumi?’
“Nenda kwenye mashamba ya chai kwa mfano watoto wengi wa kike wameambukizwa ukimwi kwa vile wamekuwa wakipelekwa kwa ajili ya kusaidia kazi. Huko wanakutana na wanaume na kufanya nao ngono isiyo salama.
“Wanaingia karibu kila siku na utasikia wanaume wakishangalia ‘nyama mpya’ imeingia.
“Akishapata ukimwi sasa dada huyo anaanza kulaumiwa na kuitwa malaya. Je, ni mara ngapi tumejiuliza kama huyu binti amepata virusi vya ukimwi baada ya kubakwa?”
Mabala anasema zipo sababu nyingi zinazoleta maambukizi ya ukimwi na hasa mazingira ambayo vijana wanakulia.
“Tuangalie mazingira ya vijana wetu, kuanzia ngazi ya familia. Kama baba atakuwa mwenye kupenda umalaya basi na hata mtoto pia atakuwa malaya.
“Wapo wazazi wa kiume wanaoshabikia mambo hayo na kama kijana wake hajaonekana na msichana wanaanza kuhoji kama kweli mtoto ni mzima katika tendo la ngono.
“Mambo yanayofundishwa kwenye unyago pia ni kikwazo katika harakati za kupunguza kasi ya maambukizi. Wanaambiwa hakuna kumtegemea baba au mama,” anasema Mabala.
Hata hivyo, ipo haja kwa wazazi au walezi kutoa elimu kwa watoto wao kuhusiana na mambo mbalimbali ya kijamii.
Anasema kuna hatari kubwa ya kuwaficha watoto vitu mbalimbali na kwamba siku akijaribu ndipo anaanza kuharibikiwa.
“Tunapowaficha ndio tunazidi kuwaharibu. Tuwasaidie kwa kuwaelekeza mambo ya msingi wakiwa wadogo.”
Mapema Juni mwaka huu wakati katika warsha ya uelewa masuala ya jinsia kwa waandishi wa habari, Mabala alipata kusema kuwa njia nyingine ya kuondoa ukimwi ni kutokomeza umasikini. Warsha hiyo iliandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).
“Shida za maisha na lishe duni huleta ukimwi pia angalia kwa mfano slums (makazi ya hovyo) za Kibera au Mukuru jijini Nairobi, Kenya.”
Lakini anasema pia kuwa kuna umuhimu wa kujali stadi za maisha kwa maslahi ya wananchi wote.
“Kwa bahati mbaya sana watu wengi wanadhani stadi za maisha ni kwa ajili ya kampeni za ukimwi. Stadi za maisha ni kwa ajili ya kila kitu katika maisha yetu.
“Watu wafundishwe kujiamini na hilo likifanyika hata watendaji wetu wakuu watawajibika ipasavyo.”
Kuna jambo ambalo Mabala hasiti kulizungumzia nalo ni deni la Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete.
“Ahadi ni deni, Serikali bado ina deni kwa wananchi wa Tanzania. Sasa hapa nadhani ipo haja ya kuorodhesha yote yaliyokuwa yameahidiwa kabla ya uchaguzi na kuona mangapi yametekelezwa.
“Watu wanataka kuona ahadi zikitekelezwa. Labda niseme kitu kimoja kwamba wakati ule wa uchaguzi nilipata meseji nyingi sana vijana wakiniandikia juu ya matumaini yao kwa Serikali mpya.
“Lakini sasa mambo yamegeuka, wengi wao wamekata tamaa. Hakuna anayeshangilia tena. Wanaona kuwa wameangushwa hata ukizungumza nao hawana matumaini.
“Maisha bora kwa kila Mtanzania yatawezekana tu kama ufisadi utatokomezwa. Hatuwezi kusema juu ya ustawi wa raia wakati kumejaa ufisadi.
“Kuna watu wanaona wana haki ya kujihaki. Wao kwanza wengine baadaye. Kwa mtindo huu wa uwajibikaje tusitarajie maisha bora kwa kila Mtanzania.”
Amezungumzia pia suala la Waziri wa Fedha Zakia Meghji kuvishambulia vyombo vya habari juu ya Bajeti ya mwaka mpya wa fedha 2007/08 iliyopitishwa hivi karibuni.
“Unawezaje kusema kuwa kukosoa si uzalendo? Hii inashangaza sana. Mimi sioni kama alikuwa na haja ya kusasirika.
“Inawezekana kuwa kwa kukosolewa unakuwa mzuri zaidi. Mimi nikikosolewa nafurahi sana. Labda nikupe mfano mmoja. Wakati fulani nikiwa shuleni niliwahi kumkosoa mwalimu akanichukia sana.
“Nilipoona anaendelea kunichukia nikakubali kila jambo lake darasani hata kama nilibaini makosa. Huyu alikuwa anapotoka.
“Kwa hiyo hata kwa Serikali yafaa ikubali kukosolewa. Ikikubali hilo maana yake ni kwamba itapata muda wa kujipanga na kutoa ufafanuzi,” anaeleza.
Mabala amewahi kufanya kazi na Shirika la Kuhudumiwa Watoto Umoja wa Mataifa la (UNICEF) nchini Tanzania kabla ya kwenda Ethiopia kuwa Mkuu wa Idara Kitengo cha Vijana dhidi ya ukimwi.
Kwa sasa ameacha kazi hiyo na badala yake ameanzisha Taasisi ya Maendeleo Shirikishi ya Vijana Arusha (TAMASHA). Makao Makuu yake yanatarajiwa kuwa Arusha.
“Tumepata usajili miezi miwili iliyopita na sasa tunahaingaikia kujenga makao. Tuko watu watatu kama waanzilishi na tutashirikiana na mashirika mengine pia.
“Tumeanzisha taasisi hii kwa ajili ya kuwasaidia vijana wasiozidi miaka 30. Walengwa hapa ni vijana chipukizi.”
Kwa muda mrefu Mabala amekuwa mwalimu, mtafiti na pia mchambuzi wa masuala mbalimbali ya kijamii katika magazeti na vyombo vingine vya habari.
Safu yake maarufu ilijulikana kama Makengeza. Ameandika vitabu vingi kikiwemo Kwangu Wapi na Poems From Tanzania kilichotungwa kwa ushirikiano na washairi mbalimbali wa Tanzania.
Monday, September 3, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment