Monday, September 3, 2007

Usiombe uchomwe kwa mrembe

Na Innocent Munyuku

SALAAM aleikhum. Bila shaka mambo yanakwenda sawia kama ilivyo kwa Mwandika Busati. Mengi yanakwenda kwa mtindo unaokubalika.

Wikiendi hii Mzee wa Busati alikuwa na sahiba yake mmoja aliyezuri nchini kwa muda akitokea kwa Malkia Elizabeth. Rafiki huyu alipata kukaa darasa moja na Mwandika Busati enzi zileeeeee.

Huyo jamaa akawa mjanja na leo hii anatafuna pauni za Uingereza kama hana akili nzuri. Kawahi huyu na hana mawazo mengi kama ilivyo kwetu hapa Bongo ambako tunawaza hata namna ya kumbana konda wa daladala ili atupunguzie Sh 50 ya nauli.

Katika mazungumzo mafupi na sahiba, Mzee wa Busati akadokezwa kuwa kuna watu huko ughaibuni wanapata fedha kwa mgongo wa wasanii wa kibongo. Kivipi? Jamaa akawa wazi kwamba kuna wajanja huko ambao kazi yao ni kuangalia kuna nyimbo gani mpya zinavuma.

Wakishazibaini huzikusanya na kuanza kuziuza kwa bei kubwa. Yasemwa kuwa soko la nyimbo hizo za Kibongo ni kubwa ile mbaya.

Hiyo ni ajira tayari kwa wajanja hao ambao bila shaka ni wabunifu pia. Mzee wa Busati alipouliza kwanini basi wasanii husika wasikomae na kudai haki zao, jamaa akaangua kicheko hadi meno yote ya mtu mzima yakaonekana.

Akadai kuwa hawawezi kufurukuta kwa sababu hata hao wasanii wenyewe baadhi yao kazi si zao. Wameiba kazi za wengine kwa hiyo hawana ubavu wa kupayuka kudai haki zao.

Mzee wa Busati hakushangaa sana na badala yake akaunga mjadala kwa kasi ya ajabu. Kwamba si mara moja au mbili ameshawahi kunena juu ya umuhimu wa wasanii kuwa na hakimiliki.

Lakini kwa bahati mbaya walio wengi wao hawataki kusikia juu ya umuhimu wa hakimiliki na matokeo yake ni hayo sasa kwamba wajanja huko ughaibuni wanakula sehemu ya kazi zenu.

Hakika wanafaidi kwa sababu wanatambua wazi udhaifu wenu. Kwamba ni nadra sana kwa mwizi kulalama pindi naye anapozidiwa ujanja na mwizi mwingine. Mambo huenda kimya kimya.

Hivi nani atasimama na kudiriki kulia mbele ya hadhara baada ya gari aliloiba nalo kuibiwa? Kama yupo basi hakuna shaka kwamba huyo ni hamnazo. Si mzima kichwani.

Ndiyo hayo sasa yanayoendelea katika fani ya muziki hasa huu wa kizazi kipya ambao wengine huuita bongofleva. Wanakauka makoo kwa kuimba lakini wengine wanalainisha koo kupitia tungo hizo.

Mzee wa Busati alipata kuandika hapa mfululizo wiki chache zilizopita kwamba kama wanamuziki hawa wataendelea kung’ang’ania kuiba midundo kutoka katika intaneti basi umahiri wao utaishia Bongoland.

Watafika wapi wakati wanajua kuwa muziki si wao? Wataishia kuzindua albamu pale Diamond Jubilee halafu kwisha habari yao. Wakishazindua wanapeleka kwa wasambazaji ambao nayo kama ilivyo ada wanakandamiza nakala kadhaa wapate kununua magari ya mtumba.

Alikokulia Mzee wa Busati kuna wawindaji. Enzi zile akiwa bado shamba, alipata kushuhudia wawindaji hao wakiwa wabunifu kila siku. Siku ya kumwinda nguruwe kwa mfano, walichukua mikuki mingi.

Lakini si kila mkuki ulifaa kwa mawindo. Katika mikuki upo mmojawapo uliopewa jina la mrembe. Mkuki sampuli hii ni kiboko ya njia. Ni aina ya mkuki wenye ncha kali na aghalabu ukipenya kwenye ngozi ya mnyama hakika ndio mwisho wa uhai wake.

Kwa wawindaji wa sanaa ndani na nje sasa nao wameanza kutumia mrembe ili wakamilishe furaha yao. Wanazidi kutumia mkuki sampuli hii. Wataendelea kutumia mirembe kwa sababu washajua udhaifu wa baadhi ya wanamuziki.

Mzee wa Busati lazima aweke wazi msimamo wake na bila shaka hii si dhambi hata kidogo. Kwamba yeye ni mpenzi mkubwa wa sanaa. Ni nadra kumwona kwenye viwanja vya soka au kwenye ulingo wa ngumi.

Sanaa ni sehemu ya maisha yake na siku zote wasanii ndio marafiki zake. Ukikamata simu yake na kuanza kupekua si rahisi kukuta namba za wanasoka au wanamasumbwi. Za wasanii zimejaa hadi kutapika.

Aliacha kushabikia soka baada ya kubaini kuwa migogoro haielekei kumalizika. Wenye maslahi na mitafaruku wanazidi kuzaliwa kila siku. Hiyo ni ajira yao. Migogoro ikiisha watakula wapi?

Kwa hiyo anapoona sanaa inapotea kwa kukosa maarifa, mtima wake huumia. Mbona hawa hawaambiliki? Tatizo li wapi?

Hivi kweli wanashindwa kujifunza kupiga marimba au kupuliza filimbi? Ni kweli kwamba hawana muda wa kupiga gitaa au ngoma? Amkeni wajameni. Vinginevyo mtaendelea kunasa kwenye tope la umasikini.

Amkeni sasa kwani kukaa kwenu mafichoni ndiko kunasobabisha wajanja waanzishe utaratibu wa kuwaibia sehemu ya kazi zenu.

Wana ubavu wa kufanya hivyo kwa sababu wanajua kuwa nanyi pia mmeiba midundo ya muziki japokuwa mashairi ni ya kwenu.

Mkibalika leo kwa kuwa wabunifu na kujiwekea kazi zenu halisi, mirembe inayotumika kuwachoma haitafanya kazi tena na badala yake itawageukia wabaya wenu.

Vinginevyo Mzee wa Busati anaweka kalamu chini ili kupisha tafakuri nyingine kwa ajili ya wiki ijayo.

Wasalaam,

No comments: