Na Innocent Munyuku
SIKU moja katika kijiwe fulani cha kahawa jijini Darisalama Mzee wa Busati alizusha mjadala ambao wengine wakadiriki kupendekeza apige mawe au anyongwe hadi kufa.
Ulikuwa mkusanyiko wa wasanii na watu wa fani nyingine. Kilichosemwa na Mwenye Busati siku hiyo ni kwamba vijana wa siku hizi akili zao zimekuwa kama dodoki.
Kwamba pamoja na kazi nzuri ifanywayo na dodoki kwa kusugua miili ya watu wakati wa kuoga, bado halina uwezo wa kukataa kunyonya maji yenye taka. Litasomba mengi kwenye maji bila lenyewe kufaidika.
Leo hii si kitu kigeni kumwona kijana akiwa na hereni masikioni. Si ajabu tena kuwaona wanaume waliosuka wakafanana na wanawali. Hawa wamejaa tele.
Jamii imegeuka dodoki au sponji kwa kufyonza mambo wayaonayo kwenye vioo vya televisheni. Yasikika mahala pengine kwamba wapo wanaume wanaovaa siniguse kwenye viuno vyao! Si ya kucheka haya. Shanga kiuononi mwa mwanamume?
Mzee wa Busati alizua mjadala huo akitaka ujadiliwe kwa kina na kwanini hasa wasanii hawayakemei haya? Kumbe miongoni mwa waliozushiwa mjadala walivaa hereni na wakati fulani waliwahi kusuka nywele zao.
Ikawa kazi kubwa. Ikaonekana kwamba hoja ya Mwandika Busati ililenga ‘kuwakejeli’ wanaume wasuka nywele na wavaa hereni. Shughuli ikawa pevu kiasi ambacho ililazimika busara zaidi kuyamaliza.
Ukaja mshangao mkubwa kwamba hivi hata wale wasanii wa muziki waliokuwapo katika hadhira ile hawakuona umuhimu wa kuyakemea yale? Hawa wamegeuka mabahau pia? Dira yao i wapi?
Hawa ndio wanaovaa suruali mlegezo wakionyesha nguo zao za ndani kama wafanyavyo wasanii wa kiume huko Marekani na Ulaya. Hawa wa huku Bongo hawajui kiini cha uvaaji huo wa suruali.
Hawaelewi kuwa huko ughaibuni mtindo wa kuonyesha nguo za ndani unawaingiza mamilioni ya dola za Marekani kwani huwa wanatangaza biashara ya waliotengeneza mavazi hayo ya ndani. Si kazi bure, wanajaza ngwenje kwenye suruali zao nao wakapata shibe.
Baadhi ya wasanii wetu hawalioni hilo, badala yake wamekaa kuimba mapenzi na kusifia mavazi. Hivi mna faida gani kwa kizazi hiki na kijacho? Ya nini basi tukuite msanii wakati huna mwongozo kwa watu wako?
Mzee wa Busati huangalia sinema, husikiliza nyimbo na mara nyingi hakosi sanaa za maonyesho katika sehemu mbalimbali nchini. Kinachoonekana huko wakati mwingine ni vituko. Ndipo maswali yanapokuwa mengi kwamba ni kweli tu makini katika kuifanya sanaa kuwa mwongozo wa jamii?
Leo hii mwaimba mapenzi tu kwenye tungo zenu. Leo hii mwaigiza maisha ya kifahari na kusahau kuwa filamu za aina hiyo hazina maana kwa jamii ya Watanzania.
Mwaigiza fulani kafumaniwa ili iweje? Lakini Mzee wa Busati ana hofu nyingine nayo ni kwamba baadhi ya filamu si mawazo ya waigizaji na watayarishaji. Kwamba mengi yanaigwa hasa kutoka sinema za Nigeria.
Filamu nyingi za kibongo zilizowahi kunasa katika macho ya Mwandika Busati ni maigizo ya Nigeria. Hivi ni lini sinema ikatayarishwa na kuingizwa sokoni ndani ya majuma manne?
Huko nyuma ilishawahi kunenwa na Mzee wa Busati kuwa kuna uhuni unafanyika kwa baadhi ya watayarishaji wa filamu nchini, achilia mbali ubora wa filamu zenyewe na maudhui yake.
Twalipeleka wapi taifa letu? Twakurupuka na kuyaficha yanayopaswa kutambulika mbele ya jamii. Yanayopaswa kukemewa yanavishwa kofia ya kifalme. Huu mwendo si sahihi.
Kwa vile baadhi ya wasanii wetu wameendelea kuyakumbatia yasiyofaa si rahisi kumshawishi kijana acheze sindimba au lizombe.
Leo hii ukiwaambia vijana kuna tamasha la ngoma za utamaduni hakika watasita. Wengi wao watakwambia hawana muda mchafu wa kuangalia au kusikiliza mdumange.
Hawa si wa kulaumiwa hata kidogo. Hawapaswi kulaumiwa kwa sababu katika makuzi yao waliambiwa juu ya umahiri wa Madonna, Lionel Richie na wengine wafananao na hao. Hawakupewa nafasi ya kumjua Mwinamila au Morris Nyunyusa. Mambo ya jadi walifichwa wakafunguliwa vioo vya luninga waangalie ughaibuni kunani.
Hamjasikia habari ya Watanzania kuyakataa majina yao ya ukoo? Si ajabu Anyimike akajiita Any Mike, Mloka akajibadili kuwa M-Look. Si mambo ya kucheka yanatokea kila leo. Yanatokea kwa sababu akili zimejazwa imani kwamba ya ughaibuni ni mema kuliko yetu.
Huo ndio mfumo uliojengwa kwa sasa. Yafaa sanaa ikamate nafasi yake kukemea uharibifu huu. Hilo lifanyike mapema iwezekanavyo.
Mzee wa Busati huuguza majeraha moyoni mwake anapoona panchari iliyotokea katika sanaa haizibwi haraka.
Vinginevyo, Mwenye Busati anaomba afike tamati kwa juma hili. Wiki ambayo wenye vibali maalumu watajihalalishia ustawi wa jamii. Mwisho wa mwezi huo waja.
Kwa wengine yaweza kuwa wiki ya maumivu, foleni ya madeni kila mahala. Waamka maskani saa 10 alfajiri na kurejea saa saba usiku. Usingizi hauji kwani yasemwa kuwa usiku wa deni haukawii kucha.
Wasalaam,
Monday, September 3, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment