na innocent munyuku
ALITOKOMEA kusikojulikana na mbaya zaidi ni kwamba hakuwahi kuaga wala kusema kipi kilimsibu hadi akaingia mitini. Mzee wa Busati kaibuka na sijui aanze kujitetea kimtindo gani.
Pengine awe mtii kama ngamia kwa kusema kuwa alitenda kosa kuacha kuteta na wadau wake kama ilivyokuwa miaka ya ile ya neema. Miaka ambayo nchi ilifurika maziwa na asali ya mwitu.
Mzee wa Busati ameshaweka wazi kwamba yu radhi kwa adhabu lakini adhabu hiyo isiwe ya kumlaza njaa au kuutokomeza uhai wake kama alivyofanyiwa sahiba Saddam Hussein.
Huu ni mwanzo wa makazi yake mapya na kwa uweza wa Allah, Mwenye Busati atakuwa akinguruma hapa kila Jumatatu ambayo wengi wameipachika kuwa ‘Blue Monday’.
Juma hili analianza kwa kuwapa pole na pia kuwapa moyo Wana wa Jangwani ambao juzi walipigwa mweleka katika kuwania taji la Klabu Bingwa Afrika. Wameshindwa kufurukuta mbele ya Waarabu wa Esperance ya Tunisia.
Katika kipute chao mara ya kwanza mjini Tunis, Yanga ililala kwa mabao 3-0 na hapo shughuli ilipoanza kuwa ngumu. Kwani sasa kibarua cha Yanga kikawa lazima wawaadabishe Esperance kwa mabao 4-0 ili wasonge mbele.
Zikaja soga za kijiweni kwamba kipigo hicho cha Yanga kilitokana na mchezaji wake Hamis Yusuf kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
Wenye akili zao walishangaa na kuguna. Kwamba hivi kweli kuondolewa kwa mchezaji huyo kuliwachanganya Yanga kiasi cha kushindwa kulinga lango lake? Hivi ni visingizio ambavyo havina maana kwa wanaojua soka.
Juzi Wana wa Jangwani wameumbuka kwa kauli hiyo ya visingizio kwani katika mechi yao ya marudiano kwenye Uwanja wa Kirumba jijini Mwanza, Esperance ikakumbwa na dhahama baada ya wachezaji wawili kulimwa kadi nyekundu.
Kwa bahati mbaya sana Mzee wa Busati hakuwapo uwanjani lakini alikuwa akifuatilia kipute hicho kwa njia ya redio na njia nyingine za mawasiliano na kwa hakika aliposikia kuwa wachezaji wawili wa Esperance wako nje kwa kadi nyekundu akaamini sasa neema kwa Yanga imetimia.
Hakika Mwandika Busati aliamini hivyo kwa kigezo cha Tunis kwamba kwa vile Yanga ilifungwa baada ya kuwa na wachezaji 10 dimbani basi kwa vyovyote mwisho wa Esperance ulishawadia kwani wako tisa dimbani. Dakika zikayoyoma na hakuna bao lililopatikana.
Mzee wa Busati hapendi unafiki. Kwanini mwaleta visingizio visivyo na kichwa wala miguu? Najua wenye kuipenda Yanga watafura kwa hasira lakini ukweli lazima usemwe ili kuepuka aibu kama hii ya juzi.
Mliporejea mlisema waamuzi waliwabeba Waarabu na je, vipi ya Kirumba mwasemaje? Mambo yanapoenda upogo ni heri mkakiri kwamba maji yamezidi unga. Semeni kwa uwazi ili hata wasojua soka wakaja kuwakebehi kwa vijembe vya kuchoma mitima yenu.
Waraka huu hauna lengo la kuwaumiza washirika wa Jangwani bali walenga kutoa changamoto ya moto ili siku zijazo msije mkaleta visingizio ambavyo mwisho wa siku vinawaletea aibu. Naam badilikeni kwani husemwa kwamba johari za mtu ni mbili, akili na haya.
Baada ya kuangukia pua katika Klabu Bingwa Afrika, Yanga sasa ina nafasi nyingine kuwania Kombe la Shirikisho. Huu ni muda wa kujipanga upya ili kufuta aibu iliyotokea.
Neno la Mzee wa Busati kwenu ni kuwa badala ya kuanza kusaka wachawi, Yanga ijipange upya kwa umakini wa hali ya juu. Huu usiwe muda wa kulala makaburini, sikilizeni na kutekeleza mafunzo ya makocha ili msije mkachacha.
Vinginevyo Mwenye Busati anakaribia kufika mwisho kwa leo hii akitafakari namna ya kuumalizia mwezi huu uliombatana na maumivu. Pasaka imefuja mifuko ya wengi, ngwenje zimeyeyuka na wanaokula mkate mchana si kama wamependa bali ni hali ngumu za maisha.
Mshirika mmoja kule Tabata Relini sasa amekuwa mpole kama aliyenyeshewa mvua. Kazizima na moyo wake huyo ajiitaye ‘mzee wa kutibua’ unatweta kwa hofu kama atafanikiwa kufika mwisho wa mwezi. Miayo imezidi na madeni yanazidi kipimo. Pole mwanakwetu kaza buti.
Wasaalam,
Monday, September 3, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment