Na Innocent Munyuku
MAISHA ni mapambano. Kauli hii ambayo ni wahenga imedumu katika vizazi vingi duniani na imekubalika kwa walio wengi kwa miaka mingi.
Wiki hii MTANZANIA Jumapili ilifanya mahojiano na Angela Leyoko mama wa watoto wawili ambaye amepitia misukosuko mingi na sasa anakula kivulini.
Angela ni Katibu Mkuu wa Chama cha Kuweka na Kukopa cha King’ongo Kimara Stop Over Dar es Salaam ambaye kwa umri wake wa miaka 27 ameshafanya mengi na kwa jamii ya Kiafrika anaweza kutajwa kuwa mmoja wa wanawake wenye ari ya kuthubutu.
Chama hicho kilichoanzishwa mwaka jana kikiwa chini ya Mwenyekiti Fatma Iyulu kinaundwa na idadi kubwa ya wanawake.
Lakini safari ya Angela hadi kufikia hapo alipo ina mengi ya kujifunza. Kishajiingiza katika machimbo ya madini na biashara za aina mbalimbali akiwa na lengo la kuweka sawa maisha yake.
“Mwaka 2000 nilipata habari kutoka kwa ndugu zangu kuwa kama nina uwezo wa kujiingiza katika uchimbaji wa madini basi nifanye hivyo na kwamba kinachohitajika sana ni pampu ya maji.
“Hawa walikuwa wametoka kwenye machimbo ya dhahabu wilayani Handeni mkoani Tanga,” anasema Angela na kisha kuongeza:
“Nilinunua pampu ya maji na kuanza safari ya Handeni, nikanunua pia unga wa mahindi na maharage. Safari kutoka Dar es Salaam ilikuwa ngumu sana kwani hadi kufika katika eneo la machimbo huko Handeni tulitumia siku mbili kutokea Handeni mjini.
“Ilikuwa safari yenye misukosuko na watu niliosafiri nao katika msafara walikuwa wanaume. Nadhani tulikuwa kama 15 hivi.
“Tulipofika kwenye machimbo tukatandika mahema na ndani yake tuliweka majani ya migomba kwa ajili ya kulalia. Namshukuru Mungu kwani katika msafara kulikuwa na mjomba wangu.”
Angela anasema kuwa kazi ya kusaka dhahabu ikaanza naye akiwa mstari wa mbele kupiga chepe. Lakini kwa bahati mbaya kazi ilikuwa ngumu kutokana na mvua.
“Watu niliokuwa nimewaajiri kwa muda katika uchimbaji walijitahidi, walichimba na tukaanza kuona dalili ya kupata dhahabu lakini tatizo likawa ni mvua.
“Mvua iliharibu kila kitu. Hata hivyo nashukuru nilipata mawe kadhaa nikaamua kuondoka kutokana na hali ngumu mgodini,” anasema Angela.
Lakini wakati akipanga safari ya kurejea jijini Dar es Salaam mvua kubwa iliyokuwa ikiendelea wakati huo ikaharibu barabara. “Kulikuwa na daraja moja liliharibiwa vibaya na mvua kiasi kwamba tulilazimika kuvuka kwa kuongozwa na wenyeji.
“Sasa kazi ikawa ngumu kwangu kwani wale wenyeji walikuwa wakivusha watu kwa sharti kwamba lazima uwe uchi, walisema nguo zinabeba maji kwa hiyo isingekuwa rahisi kuvuka.
“Mimi niligoma wakaniongoza kuvuka lakini tulipofika katikati ya mto yule jamaa akaniambia kuwa hawezi kuendelea kwa sababu maji yalikuwa yamezidi kwa vile nilikuwa na nguo. Akaniachia mkono.
“Ghafla nikaanza kusombwa na maji. Bahati ikawa kwangu nikakutana na miti ambayo niliing’ang’ania na yalinisaidia kutosombwa tena na maji.
“Walipoona nimenasa wale jamaa wakajitosa mtoni na kuniokoa na wakati huo nikiwa na dhahabu yangu kwenye mfuko wa nailoni,” anasema.
Anaeleza kuwa alifanikiwa kufika Handeni na baadaye Gairo kabla ya kuwasili jijini Dar es Salaam akiwa mchafu ajabu. “Nguo zangu zilikuwa hazitamaniki nilikuwa nimechoka na nakumbuka kutoka Gairo hadi Dar es Salaam nililala kwenye korido la basi bila kujitambua.”
Baada ya kuuza dhahabu hiyo alifanikiwa kufanya mambo mbalimbali ikiwemo kununua nyumba na kiwanja kwa ajili ya familia yake.
Lakini safari ya Angela haikuanzia hapo. Amewahi kufanya kazi katika kampuni mbalimbali ikiwemo ya Shabiby Line ambayo ni ya ushafirishaji na Gooryong iliyokuwa ikitengeneza sare za jeshi.
“Nikiwa na Kampuni ya Shabiby nilikuwa Meneja Mauzo kule Gairo lakini hiyo ni baada ya kuwa Katibu Muhtasi wa Meneja Uzalishaji wa Kampuni ya Gooryong.”
Mbali na kupitia sehemu hizo za kazi, Angela taaluma yake nyingine ni mbunifu wa mavazi na alipata ujuzi huo katika Chuo cha Shelma cha jijini Dar es Salaam kati ya mwaka 1995-96.
“Nilijifunza mambo ya mavazi kwa maana ya kubuni mitindo mbalimbali,” anasema na kuongeza kuwa katika masomo yake alijifunza pia kupamba kumbi.
Angela anasema mwaka juzi baadhi ya kina mama wa King’ongo walijikusanya na kuunda umoja wao wakijishughulisha na upambaji, kupika na uongozaji wa sherehe katika shughuli mbalimbali za kijamii.
Lakini kwanini wakaanzisha SACCOS?
Anasema walikuwa wakiomba mikopo kwa vyama vingine vya kukopa na hivyo kuona haja ya kuwa na chama chao.
“Tulikuwa wanawake 12 tukaamua tuunde SACCOS yetu na hii ilikuwa Julai mwaka jana.
“Ilikuwa kazi ngumu kwa kweli kwa sababu wengi mtaani walinibeza kwamba sitaweza kwa vile umri wangu ni mdogo. Maneno ya kashfa yalizagaa lakini sikukata tamaa,” anasema.
Kwa sasa chama hicho kina wanachama zaidi ya 70 na wanajipanga kukizundua hivi karibuni. “Tuna matumaini ya kujitanua zaidi na tunachokifanya ni kuwapa somo wanachama wetu juu ya mikopo.
“Tunawapa elimu ya biashara wanachama wetu kabla ya kukopa fedha na kama tukiwa makini zaidi tutakuwa na uwezo wa kuwa na benki hivi karibuni.
“Lakini kuna jambo moja niseme kwamba wanawake hatuhitaji kuwa ombaomba na wala hatuna sababu ya kuwa masikini tuungane na tutafanikiwa,” anasema.
Angela amewahi pia kujishughulisha na biashara ya vipodozi na vitunguu. Ameolewa na ni mama wa watoto wawili James na Joreen.
Monday, September 3, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment