Monday, October 1, 2007

Safari hii msikubali matege

na innocent munyuku

KUMEKUCHA na bila shaka mambo yanakwenda katika unyoofu wake. Kama kuna matatizo hayo hayakwepeki kwa vile ni mpango wa maisha ya kila siku.

Mzee wa Busati yu katika mlolongo wake wa kuwapa porojo zake za kila wiki. Hii yaweza kuitwa wiki ya vicheko kwani walio wengi nafuu ingalipo. Mapato ya mwezi Septemba yangali yakionekana kibindoni. Si haba!

Linalomweka Mwandika Busati leo hii ni huu ujio wa kocha mpya wa Yanga Wojciech Lazarek wa nchini Poland. Kocha huyo mpya anakuja kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Milutin Sredejovic `Micho`.

Kwa wapenzi wa mpira hasa mashabiki wa Yanga kuja kwa Mpoland huyo ni ishara ya pambazuko kwa masilahi ya timu hiyo.

Mzee wa Busati kama walivyo wadau wengine katika eneo hilo hana budi kutoa mawazo yake kuhusiana na ujio wa kocha huyo mpya. Hasemi kwa mabaya bali kuwekana sawa ili mambo yakiwa sivyo basi wenye Yanga wasilalame kwamba hawakuambiwa.

Kwa mtazamo mwepesi tu ni kwamba licha ya kuwa Mpoland huyo wasifu wake unatia moyo katika soka, bado anahitaji kupewa nafasi ya kujitanua katika kutimiza wajibu wake.

Kuna hila ndani ya klabu za soka nchini Tanzania. Kwamba hapa kwa Wadanganyika kila jambo hufanywa kwa mazoea tena mazoea mabaya.

Kazi kubwa ya hao wanaojiita mashabiki na wenye Yanga yao ni kutoa kasoro kwa walimu hata kama kocha huyo ana siku mbili kambini na wachezaji.

Jukumu lao ni kupiga soga barazani wakipanga kile wanachokiita ubora wa timu lakini ukweli wa mambo ni kwamba wengi wao ni watengenezaji wa fitina ndani ya soka.

Hawana lolote la maana ndani ya mitima yao. Badala yake wamejaa porojo zilizokosa miguu na fikra pevu. Hawa ndio wa kwanza kupiga kelele kwamba fulani hafai lakini ukiwauliza mbadala hawana.

Hupayuka kwamba timu fulani ni yao lakini ukiwaambia watoe hapo senti 10 kwa ajili ya wachezaji wanakimbia mithili ya duma nyikani. Hawataki majukumu huku wakisisitiza kuwa hiyo ni timu yao.

Basi kama mambo ni hayo, kocha mpya ajaye Yanga apewe nafasi ya kutimiza majukumu yake na kamwe asitengenezewe vigingi vya hapa na pale.

Ni wazi kwamba mpira wa Kibongo ni mgumu kutokana na ukweli kwamba hakuna mwekezaji makini aliyejitokeza na kuweka vitalu vya soka.

Timu zote zimebaki kuwakusanya wachezaji kwa kutumia vigezo dhaifu na ndio maana si jambo la ajabu kusikia Mwambungu kasajiliwa Simba leo na kesho ukaambiwa kiwango chake kimeshuka.

Wanaosema fulani kashuka kiwango ni mashabiki na hapo kama mwalimu si makini basi kesho yake ataanza kumweka mchezaji benchi badala ya kumsaidia mwanasoka huyo arejee kileleni.

Hoja hapa ni kwamba midomo ya mashabiki kwa kawaida imekuwa ikiwaponza hata viongozi wa klabu husika na kufanya maamuzi yasiyofaa.

Kwa maneno mengine ni kwamba imefika pahala viongozi wa soka nchini wakafanana uamuzi na mashabiki wao. Hapo hakuna jipya zaidi ya kupanga timu wapendavyo.

Hujapata kusikia kuwa mchezaji fulani ni kipenzi cha kiongozi fulani? Kwa hiyo kama mchezaji huyo hakupangwa basi hapo kocha huingia matatani. Atasemwa kwa ubaya na hata atengwe na kaya.

Huu si muda wa kuendeleza fitina ndani ya soka kwa maana hiyo ujio wa kocha mpya kwa Wanajangwani kujengwe kwa uzio wa subira na nidhamu kwa mwalimu huyo.

Mzee wa Busati anayasema hayo kwa vile anaelewa baadhi ya mambo ya kihuni ndani ya klabu za soka nchini. Huko kila mmoja ana uamuzi wake atakavyo hata kama ni kupoteza dira ya maendeleo.

Wanachoangalia ni masilahi ya leo na si kujenga soka kwa ajili ya maisha mema ya wachezaji na ustawi wa nchi. Wao wanaharibu na ukiwauliza watakwambia atakayekuja atajenga ukuta baada ya wao kupuuzia nyufa.

Kama mpira wa kusutana na kuwashambulia makocha utaendelea katika uso wa Wadanganyika basi mjue kuwa hiyo ni laana katika mpira wa miguu nchini na hata kama atakuja Dunga kuwafundisha bado mtakwama.

Mtazidi kukwamba kutokana na ukweli kwamba masikio yenu yamejaa nta na hamtaki kukubali kwamba kuna umuhimu wa mabadiliko.

Kinachosemwa na Mwandika Busati ni kwamba suala la makocha kuzikimbia timu baada ya muda mfupi si la kupuuzia. Kuna haja ya kuangalia wapi kuna tatizo.

Hawa wanaokimbia si wendawazimu hata kidogo, wana akili timamu na wanapoona makubaliano hafifu hulazimika kukitoa ili kulinda heshima zao.

Basi kwa wenye upeo wa utambuzi wa mema wadake haya yasemwayo na Mzee wa Busati kwamba safari hii Yanga msikubali matege katika kushirikiana na kocha mpya ajaye.

Wenye dhamana ya kuitawala Yanga, enendeni mkahubiri uvumilivu na moyo wa ushirikiano kwa mashabiki wenu. Vinginevyo itabaki hadithi ile ile ya kale kwamba Jangwani na Msimbazi hakukaliki.

Wasalaam,

No comments: