na innocent munyuku
‘UNLUCKY LUCKY DUBE’ (Dube mwenye bahati aliyekosa bahati) yalikuwa maneno ya mwandishi mkongwe Balinagwe Mwambungu ambaye sasa ni mhariri mshiriki wa gazeti dada la Mtanzania.
Mwambungu ambaye hupenda kuitwa Big Mwa, alikuwa akiteta na Mzee wa Busati mara baada ya kusikia taarifa ya kifo cha mwanamuziki nguli wa muziki wa reggae barani Afrika, Lucy Dube.
Dube alipigwa risasi na majahili mbele ya wanawe wawili katika kitongoji cha Rossettenville jijini Johannesburg na hivyo kusitisha uhai wake.
Katika mazungumzo kati ya Mzee wa Busati na Big Mwa kilichojadiliwa ni namna mwanamuziki huyo alivyopoteza bahati ya kuishi kutokana na ufedhuli wa majahili hao.
Afrika imetikisika na dunia kwa ujumla imeshtushwa na taarifa ya msiba wa mwanamuziki huyo aliyepoteza maisha akiwa na umri wa miaka 43.
Alikuwa kinara na hata sifa zake zikakubalika katika kila ya mabara. Amepotea lakini sifa zake zingali zikienea.
Mzee wa Busati kwa asili yake ni mwenye imani ya rasta akiamini juu ya umoja, upendo na mshikamano. Ndicho alichoshikilia Dube katika tungo zake. Kahubiri haki za binadamu na umuhimu wa kujali wengine pasipo kubaguana.
Kilio kimetanda na hakuna shaka kwamba wengi wanaomlilia Dube wanahuzunika kwa vile wamepoteza kiini cha busara.
Mwanamuziki wa reggae nchini, Ras Innocent Nganyagwa maarufu kama Ras Inno juzi Jumapili alikuwa anatimiza umri wa miaka 42. Mzee wa Busati alikuwa miongoni mwa waliomtumia ujumbe wa kumtakia maisha mengine marefu. Katika majibu yake, Ras Inno alisahau sherehe na alichosema ni kwamba ana majonzi ya Dube.
Wasanii wengi wameshaingia studio kurekodi nyimbo za kumuenzi Dube. Wanahubiri mema yake na namna ya kuishi katika uadilifu.
Dube kishazimika lakini ukweli wa mambo ni kwamba tungali na uwezo wa kuendeleza mema aliyoyaanzisha kama vile amani na mshikamano.
Tuendelee kulia lakini tusisahau kuwa wema katika mitima yetu. Midomo iseme juu ya umoja na kujali shida za wengine. Tusiishie kulia.
Maisha ya reggae kwake yalianza katika miaka ya 1980 akipaza sauti kukemea ubaguzi wa rangi ndani ya Afrika Kusini.
Ni wazi kwamba kutokana na umahiri wake, Dube alikuwa katika nafasi za juu kwenye mauzo ya albamu zake.
Alipoamua kuimba juu ya ubaguzi wa rangi, wazungu walimwona kuwa ni mbaya wao. Akapata upinzani wa hali ya juu.
Upinzani huo ulikwenda mbali ikiwa ni pamoja na kuufungia wimbo wake wa Rasta Never Die usipigwe redioni.
Hakukata tamaa na ndio maana akaendelea kufyatua nyimbo nyingine kibao zikiwa na uzito katika jamii kama vile, Think About The Children na Slave.
Alikuwa mfuasi mkubwa wa Peter Tosh na hata alipofanya ziara nchini Jamaica, baadhi ya mashabiki walistaajabu uwezo wake jukwaani.
Mashabiki hao wakasema kuwa Peter Tosh yu hai akifanya kazi zake barani Afrika. Walimaanisha kwamba uwezo wa Dube ulifanana na wa Tosh.
Alale unono Dube, apumzike kwa amani lakini kuna mengi ya kukumbushana kwamba wafuasi wa mwanamuziki huyo wazidi kuhubiri mema.
Kemeeni ufisadi na ushenzi katika jamii zinazopaswa kuishi kistaarabu. Kuombeleza pasipo kufuata mwelekeo wa Dube ni kukosa nidhamu.
Huu ndio mtazamo wa Mwandika Busati wiki hii. Kwamba Dube katoweka lakini sauti na maneno yake yangali yakiishi.
Mzee wa Busati anafikia ukomo akiamini kwamba wadau wake wanaendelea katika neema hasa katika wakati huu wa mageuzi.
Wengine sasa wameacha ubishi na wamekubali kwamba bila matumizi ya kompyuta dunia haiendi sawia. Hongera Mzee wa Kutibua kwa kuanzisha bulogu yako.
Hiyo ni njia ya kutanua mawasiliano lakini Mzee wa Busati ana hofu na bolugu hiyo kama kweli itaendeleza mema au ni mwamko wa kuleta migogoro katika jamii hasa kwenye klabu za soka asizozipenda.
Vingingevyo Mwandika Busati anaweka kalamu chini akisubiri mwezi ugote arekebishe masuala yake. Si wajua Masiha yu jirani? Pasipo ngwenje kwa wakwe hakuendeki.
Wasalaam,
Monday, October 22, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment