Thursday, October 18, 2007

Umoja Records yaja na fikra pevu katika sanaa yazidi kujitanua

na innocent munyuku

NILIPOZUNGUMZA naye kiasi cha miezi minne iliyopita, mmoja wa wakurugenzi wa Umoja Records, Gotta Warioba alikuwa na mengi ya kunieleza.

Alisema juu ya mwelekeo wa kampuni yake katika kuinua muziki wenye asili ya Kiafrika na kuusambaza kote duniani.

Midomo yake kwa hakika ilinena kwa kujiamini na alichokusudia kukisema. Wakati huo alikuwa katika kazi ngumu ya kuratibu kazi za wasanii kibao akiwamo Vital Maembe maarufu kama Sumu ya Teja.

Si kama nilikuwa na shaka juu ya msimamo wa Gotta la hasha. Niliwaza mengi na sikuishia kuwaza tu nilimwuliza namna atakavyojipanga katika kutekeleza aliyopanga.

Wakati huo alikuwa na mpango maalumu wa kuandaa albamu ya reggae ikiwakusanya wanamuziki wa aina mbalimbali. Ni wakati huo Gotta alilazimika kulala katika studio za Active ambazo ni sehemu ya Umoja Records.

Katika mpango huo walifanikiwa kupakua albamu ya iliyopewa jina la ‘Bongo Riddims & Style’ ikiwashirikisha wasanii wengi chipukizi.

Wiki iliyopita Gotta amefanya mahojiano na Bingwa na kuelezea mwelekeo wa Umoja Records na maendeleo ya muziki kwa ujumla.

“Umoja Records imetanua wigo wake baada ya kuanza kusaka wanamuziki kutoka Kenya na Uganda,” anasema Gotta.
Anasema ameshafanya mazungumzo na wasanii kadhaa jijini Nairobi zaidi ya wiki moja iliyopita na kwamba makubaliano ni chanya.
Katika ziara hiyo amezungumza na wasanii wengi na kwa kuanzia wawili wanatarajia kuwasili nchini siku chache zijazo kwa ajili ya kuanza kazi ya kurekodi na wasanii wa Tanzania.

“Lengo la ziara yangu lilikuwa kutanua mtandao wa Umoja Records na kusaka vipaji vipya.

“Wasanii watakaokuja wana vipaji vya hali ya juu na tunaamini watashirikiana na hawa waliopo nchini chini ya kampuni yetu.”
Lakini kikubwa anachozungumzia Gotta ni kukuza mkakati wa kampuni yake kwa kuongeza ubunifu katika muziki na kwamba wasanii waliopo wana uwezo mkubwa.

“Tutaangalia namna ya kufikia sehemu nyingine lakini kwa sasa tutaikamata Kenya na Uganda, wasanii hao wakiungana na wa kwetu hakuna shaka kwamba tunakuwa na product nzuri,” anasema.

Lakini anapozungumzia mtazamo mwelekeo wa muziki nchini hasa kwa bongofleva anasema kunatakiwa mapinduzi ya fikra.

“Unakumbuka tulianzisha project hapa ya kuwakusanya wanamuziki kwa ajili ya kutengeneza albamu ya reggae.

“Walikuja wengi na idadi kubwa ni wale wa kizazi kipya, tulielekezana na tukafika mahala tukafanya kazi nzuri pamoja.

“Lakini cha kushangaza kila aliyerekodi wimbo wake aliondoka zake na wengi hawajarudi,” anasema Gotta na kisha kuongeza:

“Walikuja wengi hapa wakarekodi na kuondoka lakini baadhi wamebaki na wana nia ya dhati kuwa nasi.
“Msanii kama Pestman, Ras Mizizi wameonyesha uwezo wa hali ya juu katika kazi zao. Wana fikra pevu na tunajivunia kuwa nao.
“Ras Inno naye anashirikiana nasi na kwa hakika anatupa changamoto nyingi. Kwa hiyo unaweza kuona kuwa ni mchanganyiko uliokomaa,” alisema Gotta.

Anawazungumzia vipi waliorekodi na kukimbia?

“Mimi nasema si tatizo lao, hao waliokimbia ni waathirika wa mfumo mzima wa hali ya utayarishaji wa muziki nchini.

“Kwamba si rahisi sana kuwabadilisha, tunahitaji mapinduzi ya fikra na si kazi ya siku moja.

“Lakini jambo moja liko wazi kwamba kama itatokea siku wakaamua kurejea hapa hatuna kinyongo nao, waje na tutawapokea.

“Wakija bila shaka watakuwa na kitu wamejifunza huko walikokimbilia nasi tutawaonyesha mapya tuliyonayo nadhani hapo tutafundishana na kuwa na kitu bora,” anasema Gotta.

Anapowataja baadhi wa wanamuziki ambao wana mwelekeo chanya katika Umoja Records hasiti kuwataja Pestman, Ras Mizizi, Carola na Ras Mizizi.

“Kwa hakika hawa waliobaki wanaangalia future, nitakupa mfano wa Pestman huyu ana ufahamu mkubwa na mara nyingi hupenda kujifunza mambo mapya.

“Alikuja hapa hajui kupiga gitaa, lakini sasa anaweza kuimba huku akipiga gitaa.

“Cha kufurahisha ni kwamba anaangalia matatizo ya dunia ya kuyajadili na kutoa njia mbadala ya kuyaepuka na wakati huo akiwasiliana na jamii.”

Kwa upande wa Ras Mizizi, Gotta anasema msanii huyo amekolezwa na asili yake ya Afrika na kwamba anapopiga reggae haachi kuzungumzia imani ya rasta na uafrika wake.

“Unaweza kusema kuwa huyu anahubiri imani ya Afrika ndani ya Rastafarian na ni mwepesi katika kurekodi.”

Mbali na hayo, Umoja Records imelenga kuweka uhusiano na mataifa mengine duniani hasa barani Ulaya kwa kuunda sound system na nembo ya pamoja.

“Tutakuwa na production team yetu na kuna kitu kinaitwa mobile disco ambavyo vitatufanya tuwe mahiri katika ziara zetu,” anasema Gotta.

Anasema mpango uliopo ni kuhakikisha kuwa wasanii wanakuwa na uwezo wa kurekodi kwa nembo za nje.

No comments: