Monday, October 29, 2007

Ole wao wanaoikana michezo ya jadi

na innocent munyuku

BARAKA ziko mlangoni na shari kisogoni. Nyakati za kulalama kwamba maharagwe yanakaribia kuota tumboni zimekwenda likizo. Kilichopo ni tungo na vibwagizo vyenye utamu kwenye ndimi.

Siku kama hizi Mzee wa Busati huwa makini sana katika mikusanyiko. Iwe kwenye daladala au kwenye kilauri. Manake walio wengi wanatembea kwa matao wakijivunia ujazo kwenye mifuko yao.

Tarehe kama hizi, ubabe wa kila aina hutokea na anayekufanyia ubabe hudiriki kutamba kwamba anaweza kukupoteza mjini. Kisa? Anazo za kupandia taksi kwa siku mbili hizi.

Dada zetu ndo usiseme wameshasahu nywele zao za kipilipili. Siku hizi wanapanga foleni kwenye saluni kuzibadili nywele zao zifanane za kina Victoria Beckham au Jennifer Lopez. Si vibaya kwani ndivyo dunia inavyokwenda.

Tulidai uhuru wa kujitawala tukapewa lakini waliotupa uhuru huo wakaongeza mbinu kuhakikisha kuwa wanaziteka bongo zetu. Ndio maana Mzee wa Busati amekuwa akikemea utumwa wa akili ambao ni mbaya kuliko utumwa wa aina nyingine.

Tumefunzwa kuamini kuwa kila litokalo majuu ni jema na halina kasoro. Pita mitaa ya bongo utashangaa kuona kuwa hadi hii leo mitaa hupachikwa majina ya kigeni. Twakimbilia wapi?

Hoja ya Mwandika Busati juma hili ni kwamba jamii ya Kitanzania inapaswa kuthamini utamaduni wake na katika hili michezo ya jadi isisahauliwe.

Husemwa kwamba nchi haiwezi kutambulika kama taifa huru pasipo kuwa na utamaduni wake kama vile michezo na mengine yafananayo na hayo.

Ni kutokana na hilo, mwaka 1967 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria Na. 12 iliyobariki kuanzishwa kwa Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

Lakini kwa bahati mbaya michezo mingi ya jadi imekuwa ikiachwa kando na kuendeleza michezo mingine.

Ipo haja ya kuunda mkakati wa kuendeleza michezo mbalimbali ya jadi na kuifanyia utafiti kama ilivyopata kutamkwa katika sera ya maendeleo ya michezo.

Leo hii twaifumbia macho lakini ukweli wa mambo ni kwamba siku chache zijazo taifa litalia na kusaga meno.

Kuidharau michezo yetu ya jadi ni kujikana na kulisaliti taifa. Huku ni kupotoka na kwenda katika barabara ya giza.

Mzee wa Busati mara kadhaa ameshashuhudia katika matamasha mbalimbali namna Wabongo walivyosahau mema ya kwao. Watapenda kushabikia nyimbo za ng’ambo na kuzifumbia macho ngoma za kwao.

Wasanii wa ngoma za jadi huangaliwa kama wasiostaarabika. Hawapewi nafasi inayostahili kwa ufundi na ubunifu wao. Wamebaki kuwa mawe ya pembeni.

Leo hata vitegemezi vyetu havitaki kusikia mdundiko wala mdumange. Watakwambia wao wanakwenda na wakati kwa kusikiza muziki kutoka Ulaya na Marekani.

Mzee wa Busati hasemi kwamba nyimbo za ng’ambo zibezwe la hasha! Anachosema ni kwamba mkazo uwekwe kujali na kuthamini mema ya kwetu na hakika inawezekana.

Hivi kweli tutaendelea kujikana namna hii hadi lini? Akili zetu zimewekwa nini? au hizi peremende tunazopewa kutoka ughaibuni? Tatizo li wapi?

Leo hii Mmakonde ukikutana naye mjini hataki umsalimie kwa lugha yake. Yu radhi kusema kwa Kiingereza kuliko lugha yake ya nyumbani. Hata Kiswahili nacho huwa shida kwake. Mtasemaje juu ya hilo? Kama si uzumbukuku ni nini?

Basi na tukae tujipange upya katika hili. Watawala wetu waungane na walio chini yao ili kuendeleza utamaduni wetu.

Wasimame na waseme kwamba tujiweke katika mstari wa kufufua akili zilizodumaa na kusahau mambo ya kijadi. Yakipotea tutakuja kuangamia miaka michache ijayo.

Basi na tuhubiri hayo na wala kusiwe na sababu ya kukwepa majukumu. Twauchimbia kaburi utamaduni wetu kwa kile tunachosema kwenda na wakati. Huu ni ulimbukeni.
Mwaona fahari gani kuwaona watoto wa kiume wakisuka nywele na kuvaa hereni masikioni? Hao wanasema wanakwenda na wakati lakini ukweli wa mambo ni kwamba wamekosa bahati.

Kila walionalo kwenye kioo cha luninga basi ni jema tena jema sana. Hivi ni kweli haya hayaepukiki? Hivi ni kweli kwamba twaona sawia tu vijana kuyumba katika ardhi yao?

Mzee wa Busati anafikia ukomo akiamini kuwa mdumange au sindimba zingali na nafasi nchini Tanzania.

Mwandika Busati atakuwa mwenye faraja kusikia kuwa ngoma za kina Vital Maembe au Zemkala zinagombewa huko Marekani na Ulaya. Hilo litafanikiwa kama tutaweka mkakati maalumu wa kufufua akili zilizolala.

Akili hizo zikifufuka ni wazi kuwa hata michezo ya jadi kama pia, tufe, mieleka na mingi ifananayo na hiyo itanguruma na kupendwa na jamii.
Wasalaam

No comments: