Na Innocent Munyuku
KWA zaidi ya miezi 12 sasa, Watanzania wengi wamekuwa wakitupa lawama kwa Serikali kwamba imeshindwa kutekeleza ahadi zake kwa maslahi ya umma.
Wanacholalamikia ni hali duni ya maisha waliyonayo. Wengi wao hawana ajira na hivyo kuwawia vigumu kupata mahitaji yao ya kila siku kama inavyostahili.
Wanacholilia ni maisha bora na ajira zitakazowawezesha kuwa na vipato vya uhakika vya kutoshelezesha mahitaji ya msingi katika ustawi wa jamii.
Vilio ni kila mahala, kwani ukweli wa mambo ni kwamba, ukali wa maisha ungali ukiendelea kutokana na hali halisi ya upandaji bei katika bidhaa mbalimbali.
Sehemu kubwa ya Tanzania kinachoimbwa na wananchi ni ugumu wa maisha. Wengi sasa hudiriki kusema ya kuwa, maisha ya leo nafuu ya jana, wakimaanisha kwamba kila uchao mambo yamekuwa ya kukatisha tamaa.
Na ndio maana, hivi karibuni baadhi ya mawaziri walipozuru mikoani kuelezea ‘uzuri’ wa bajeti ya mwaka huu wa fedha 2007/08 walizomewa na wananchi.
Binafsi, habari kwamba baadhi ya mawaziri walizomewa huko mikoani na hivyo kuwa shubiri kwao ilinishangaza kidogo, lakini pia ikanifunza jambo moja kwamba sasa watu wamechoka!
Kwamba kama imefikia mahala wananchi badala ya kusikiliza hotuba za mawaziri wanawatolea maneno ya kejeli na kuwazomea, hili jambo si la kupuuzia au kuliacha hivi hivi.
Sauti zile zina maana yake na kama sitakwenda mbali na ukweli, ni kwamba watu sasa wamekata tamaa na ndio maana mazungumzo katika kila kona ya nchi ni mjadala kuhusu maisha bora.
Mwaka 2005, bei ya mkate wa kawaida kabisa ilikuwa kati ya Sh 200 hadi Sh 300. Leo hii mkate huo unaliwa kwa Sh 500 hadi Sh 700. Si mkate pekee bali karibu kila bidhaa imepanda bei.
Ndicho wanacholalamikia raia wa nchi hii kwamba sasa mambo ni magumu na kwa hakika hawaoni pa kutokea labda kwa nguvu za Muumba.
Sasa hivi kuna hili wimbi la kile kinachoitwa ‘orodha ya mafisadi’. Wananchi wengi wanaendelea na mijadala kila wapatapo nafasi ya kusema juu ya jambo hilo. Wanajadili hoja hizo za wapinzani na kwa vile Serikali imeamua kutulia, nao wanajawa na maswali tele kwenye vichwa vyao.
Wanasema juu ya mfumo mzima wa mikataba ya wawekezaji wa madini nchini. Na ndio maana huko North Mara mwezi uliopita, wananchi waliishambulia kwa jiwe helikopta ya wawekezaji.
Katika shambulizi hilo, kioo cha helikopta hiyo kilitobolewa na rubani wake kuumizwa jicho. Hii maana yake ni kwamba, kama wananchi hao wangekuwa na silaha ya kisasa wangeleta madhara makubwa.
Hawa wana hasira na wawekezaji ambao wanaendelea kuchimba madini yetu na kutuachia mahandaki. Mwananchi wa kawaida haelewi manufaa katika miradi hiyo ya madini, anachojua ni kwamba kuna hitilafu.
Anaamini kuna hitilafu, kwa sababu bado maisha yake yameendelea kuwa ya dhiki. Anachoamini ndicho hicho kwamba nchi inaliwa na wachache.
Hapa kuna ulazima wa kuyaweka haya mambo bayana. Kwamba hakuna maana njema kuendelea kushabikia misaada ya wawekezaji hao kama hakutakuwa na uwiano unaoeleweka juu ya wanachokipata na wanachokiacha kwa wananchi.
Hatuwezi kuchekelea miundombinu kwenye migodi hiyo kwa sababu ni wazi kwamba imewekwa kwa ajili ya kurahisisha utendaji wao wa kila siku.
Pengine nirejee mfano wa kombeo lililotumika kurusha jiwe lililoharibu kioo cha helikopta North Mara. Aliyerusha ni wazi alikuwa amejaa hasira akiamini kwamba nchi yake inafilisiwa. Akashindwa kujizuia akafanya alichofanya.
Leo hii wametumia kombeo, kesho watakamata chupa na jambia mkono mwingine. Wakiona mambo bado hayaendi, si ajabu wakaamua kuingia mitaani wakiwa na kila kinachofaa kubebeka.
Hili halitashangaza, kwani tayari wameshaanza kuvamia vituo vya polisi na wala hakuna mwenye hofu ya kutwangwa risasi za moto. Wananchi wanaonyesha wazi hasira zao kwa dola.
Hawatajali, kwa sababu maisha yao tayari yamekwenda upogo na hawana tena imani ya kufika nchi ya ahadi yenye maziwa na asali ya mwitu. Wataona heri wafe wakidai wanachoamini kuwa ni haki yao.
Wamechoka kwa sababu wanaona kila kitu hakiendi katika mstari unaofaa. Misaada ya nchi za nje inatumikaje? Ndivyo wanavyojiuliza.
Kuna watu leo hii wana vitambi vya ukimwi, magorofa ya ukimwi na hata magari ya kifahari ya ukimwi. Hawa wametafuna fedha za wahisani zilizolenga kuwasaidia waathirika wa ukimwi. Wakageuka wajanja wakaziweka kwenye mifuko yao.
Wajanja hawapo kwenye miradi ya ukimwi pekee, wapo kila mahala wakiwa mahiri wa kuandika ‘proposals’ za kuombea fedha za wafadhili katika miradi mbalimbali. Mingi kati ya hiyo ni yao binafsi wakila na kusaza pasipo woga.
Leo hii, hawa ndio wafalme wanaotembea kwa kujiamini wakikanyaga ardhi ya Tanzania kama ya kwao pekee. Hawa ni wateule ambao wamesimama sawia na si rahisi wakapigwa mwereka.
Lakini, hoja ya msingi hapa ni kwamba dhana ya uwiano wa maisha kwa raia wa taifa hili lazima ijadiliwe kwa mapana kwani uwezo wa kuwawezesha wananchi upo kutokana na ukweli kwamba bado tunazo rasilimali za kutosha.
Nionavyo mimi ni kwamba, kuna haja basi kukawa na jukwaa huru ambalo wananchi wa kawaida watapata mwanya wa kuwaeleza watawala wao kero na dhiki zao.
Watawala wasikae kimya au kupangua hoja kwa msimamo wa kisiasa kwani ni ukweli usiopingika kuwa maisha sasa ni magumu na yanaendelea kuwa magumu.
Wananchi wanahoji mengi na wana shaka kama wasaidizi wakuu wa watawala wanayafikisha kama yalivyo au wanaondoa ukakasi kabla ya Mkuu wa Kaya hajasoma ripoti zao.
Sidhani kama anaelezwa kero kwenye vituo vya polisi, mahakama, hospitalini au katika ofisi nyingine za Serikali ambako usumbufu wa kupewa huduma umerejea kama miaka ya nyuma.
Kama haya yataendelea, basi ni wazi kuwa wananchi watachoka na kitakachofuata ni vigumu kusema kwamba kitakuwa cha heri. Basi na tumwombe Muumba tusiione siku hiyo.
0754 471 920
Friday, November 2, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 comment:
KIUKWER BINADAM ANAFATA KITU AMBACHO FLAN KASEMA LABDA HYO FLANI TU NI MWENYE HESHIMA KUBWA SANA KATKA KIJIJI CHAO NDO MAANA KAMA SIVO WATU WANGEKUWA WANATUMIA AKILI ZAO KUKATAA KITU AMBVACHO HAKINA TIJA YOYOTE KTKA MAISHA Y A MWANADAM
TUBADILIKEN WANADAM
Post a Comment