Na Innocent Munyuku
HAKUNA jambo jema katika jamii kama uwazi na ukweli. Kwamba ili mambo yasiende upogo sharti mojawapo ni kuwa wazi na mkweli daima.
Kaya au jamii isiyo wazi mara zote itakuwa katika migogoro ya aina mbalimbali kwa sababu tu mambo mengi yamefichwa.
Kipato cha baba au mama kwa familia kikiwa siri basi hakuna shaka kwamba familia hiyo itakuwa kwenye mikwaruzo ya hapa na pale.
Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa rais na wabunge mwaka 2005 kulikuwa na hoja kutoka kwa vyama vya Upinzani kwamba Chama Cha Mapinduzi kiliendesha kampeni zake kwa fedha ‘haramu’.
Watoa hoja hawakunyamaza bali wameendelea kulisema hilo hata baada ya uchaguzi kwamba sehemu kubwa ya fedha za kampeni kwa CCM hazikufahamika zimetoka wapi.
Wananchi wanaounga mkono upande wa Upinzani nao wanalijadili hilo vijiweni kila wanapopata muda wa kufanya hivyo.
Baada ya Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete kufunga Mkuu wa Nane wa chama hicho, mjini Dodoma siku chache zilizopita akiwa jijini Dar es Salaam alitoa kauli iliyonivuta kuandika waraka huu mfupi.
Rais Kikwete aliwahutubia wananchi waliomlaki Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba jijini Dar es Salaam ambako pamoja na mambo mengine alisisitiza umuhimu wa chama kuwa na vitega uchumi.
Alichosema Rais Kikwete siku ile ni kwamba CCM ijipange kutafuta namna ya kuwa na vipato mbadala ili wakati wa kampeni kusiwe na minong’ono kuhusu vyanzo vya fedha.
Bila shaka kauli ya Rais imekuja baada ya kuzuka minong’ono kuhusu mapato ya CCM wakati wa kampeni kwenye uchaguzi uliopita.
Rais kanena umuhimu wa kuwa na vyanzo vya fedha vilivyo wazi kwa chama chake lakini kwa mtazamo wangu zumari alilopiga mkuu wa nchi ni vema likasikilizwa na vyama vingine pia.
Kwamba vyama vyote vya siasa nchini viwe wazi kuhusu mapato yake. Wawaeleze wananchi wanakopata fedha za kuzunguka nchi nzima kumwaga sera zao kwa ajili ya kujiongezea uhai wa chama na wanachama.
Leo hii ni jambo lisilohitaji mjadala mrefu kwani vyama vingi sasa vinaangalia namna ya kupata ushindi katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010.
Kama inavyofahamika, kampeni zozote za uchaguzi kote duniani zinahitaji fedha za kutosha ili kuwafikia wapigakura. Hii maana yake ni kwamba vyama vinajipanga sasa kuangalia ni namna gani wanatunisha mifuko yao.
Lakini kwa bahati mbaya sana hapa kwetu hakuna utamaduni wa kuweka bayana juu ya vyanzo vya mapato kwa vyama vya siasa badala yake utasikia minong’ono kwamba mfanyabiashara fulani katoa kiasi fulani cha fedha.
Ingawa wapo wafanyabiashara wanaojitangaza wazi kwamba wametoa kiasi fulani cha fedha kwa chama fulani, bado ni haki ya wananchi kujua fedha nyingine zimetokana na nini.
Nasisitiza uwazi wa vyanzo vya fedha kutokana na ukweli kwamba yawezekana ikaja siku, fedha za kampeni zikatokana na mauzo ya dawa za kulevya au njia nyingine haramu hatarishi kwa taifa lililo huru.
Tuelezwe pasipo kificho kwamba mabilioni haya yametokana na michango ya aina hii au msaada kutoka taasisi fulani iwe ya ndani ya nje ya nchi.
Kama ni fedha za wafadhili pia tuelezwe ni wa aina gani na zimetolewa kwa masharti gani.
Kukaa kimya hakuna maana nyingine zaidi ya kuendelea kuzua minong’ono ambayo ingeweza kufutwa kama kila kitu kingewekwa hadharani.
Nalisema hili kwa sababu mwaka 2010 si mbali kutoka hivi sasa na bila shaka baadhi ya vyama vya siasa vimeshaanza kukusanya fedha kwa ajili ya uchaguzi ujao.
Hivyo basi, wakati ukifika ni busara kuwaeleza wananchi nani kafanya kipi kufanikisha mizunguko ya kampeni.
Vinginevyo ipo siku tutashuhudia wafadhili wa siri wakidai kulipwa fadhila kwa mtindo wa kuliangamiza taifa. Tusifikishane huko.
Sunday, November 18, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment