na innocent munyuku
NI heri uchoke viungo vyote vya mwili kuliko uchovu wa ubongo. Hii ni hatari kubwa inayoweza kukufanya uonekane hamnazo kwenye kaya.
Bila shaka umeshawahi kukumbana na hali hiyo japo mara moja kila mwezi, iwe mwanzo wa mwezi au katikati yake. Ndo yalomkuta Mzee wa Busati juzi.
Mwandika Busati katoka kwenye mihangaiko yake huko mjini kati. Kasaka nyoka hadi soli za viatu zikaimba tungo za maombolezo.
Si mchezo mwanawane kusaga mguu kutoka Posta Mpya hadi Magomeni. Kisa? Kupunguza ukali wa bajeti ili mambo yasizidi kwenda upogo! Si ndo waambiwa mjini shule. Usione watu wana vitambi ukadhani maisha yao supa la hasha. Wengine wameshiba mihogo ilo chacha.
Mambo ya mjini ndivyo yalivyo. Usimwone jirani yako ananukia bia kila siku ukadhani anazo ngwenje za kutosha. Anachofanya ni kupitia kwa Mama Ubaya anaonja glasi zake tatu za machozi ya simba af baada ya hapo anapitia kwa Massawe anameza safari lager mbili kazi imekishwa.
Basi Mzee wa Busati baada ya kufika Magomeni na Sh 200 yake kibindoni akakwea daladala kuelekea maskani. Kutokana na uchovu wa kusaga mguu kutwa nzima mara baada ya kupata kigoda akautandika usingizi.
Yaliko maskani yake ni mbali na ukichanganya na foleni za Darisalama ni wazi kwamba alipata muda wa kuota ndoto pia na yaliyojiri kwenye ndoto ni haya yafuatayo.
Mzee wa Busati kaota eti yu katika kilele cha Mlima Kilimanjaro, kajiviringisha blanketi kuinusuru ngozi yake na baridi kali. Huko kileleni akaziona klabu za soka nchini zikiishi kwa upendo.
Akawaona wanachama wa Simba na Yanga wakipanga foleni ndefu kuwania hisa kwenye klabu zao baada ya kukubaliana kuwa sasa ziendeshwe kibiashara zaidi.
Akaiona pia Ashanti United, Moro United na Mtibwa Sugar zikifuata nyayo za Simba na Yanga. Hakuna tena uzandiki ndani ya klabu.
Wale wanachama waliokuwa wakitoleana maneno ya kejeli na matusi ya nguoni wakawa wameketi pamoja wakinywa kahawa na kupeana mawazo ya kuiinua soka nchini.
Ndoto ya Mzee wa Busati ikakatishwa na kelele za kijana muuza maji kwenye foleni. Hata hivyo, baada ya muda akaendelea kuuchapa usingizi.
Safari hii usingizi ukaja na ndoto mpya. Ndoto ikahamia kwenye filamu Tanzania. Mwandika Busati akawaona wasanii wakisaka elimu ya filamu kwa umakini.
Ile hali aliyozoea siku zote ya mtu mmoja kuamka tu asubuhi na kujiita prodyuza ikatoweka. Sasa hawa wakawa nguli wenye ustadi na kazi zao.
Akaziona filamu zilizopikwa zikapikika na si tena mpango wa kwenda dukani na kukuta video zilizotayarishwa kwa siku 28 eti nazo zikaitwa sinema kali.
Ndoto ikawa tamu kweli kweli manake hata wale wanamuziki ambao Mzee wa Busati alizoea kuwasikia wakiimba mapenzi tu na kusifia mavazi wakatoweka.
Kwenye ndoto yake akawasikia wakikemea ufisadi na wala rushwa waliovimba matumbo kwa sababu ya kula visivyo vyao.
Akasikia tungo zilizojaa uzalendo na kuwakemea wachache wanaouza nchi kwa njaa ya teni pasenti. Hao ambao hawajali kwamba milima ya Uluguru yafaa ilindwe kwa vizazi vijavyo.
Hao ambao wanajifanya hamnazo wasijue kuwa madini yetu ni mali ya kulijenga taifa kwa vitegemezi vyetu ambavyo baadhi yao havijui hata urithi wao.
Ndoto ikawa tamu zaidi manake akajikuta anazuru mitaa mbalimbali na kukutana na Watanzania wakijivunia utaifa wao. Wanateta Kiswahili kwa ufasaha.
Mzee wa Busati akawaona raia wengi wakiwania kuingia kwenye kumbi kuangalia ngoma na michezo ya asili. Wengi sasa wakawa wameyapa kisogo mambo ya Kimagharibi. Hakuna aliyejali tena ya kigeni.
Kina dada wakaachana na nywele za bandia. Sasa wengi wakawa wanalilia nywele zao za asili zenye kipilipili. Midomo ya wanawali hao ikapendeza kwa mdaha huku kucha ziking’aa kwa hina ya mwituni.
Honi ya lori kubwa ndiyo iliyomwamsha Mzee wa Busati usingizini akiwa ndani ya daladala. Anageuka kushoto anajikuta yu kituo kimoja kabla ya kufika anapoteremkia.
Anapangusa uso lakini moyo wake umejaa kero baada ya kubaini kuwa kumbe ilikuwa ndoto na dada aliyekuwa kulia kwake alikuwa na nywele bandia na rangi ya mdomo kutoka dukani.
Wimbo uliokuwa ukitoka kwenye spika za daladala ulikuwa ukimsifia jamaa aliyevaa mavazi ya kifahari kutoka ughaibuni.
Heri angesikia ngoma za Morris Nyunyusa au Mzee Mwinamila. Mzee wa Busati akanywea asipate raha ya ndoto yake.
Lakini je, hatuwezi kuishi kwa ndoto hiyo? Kweli Wabongo hawawezi kuendeleza utamaduni wao na kuacha kukumbatia yanayoonekana kwenye vioo vya luninga?
Hivi ni kweli klabu za soka haziwezi kujiendesha kibiashara na kuacha hii staili ya kushikiana bakora?
Mzee wa Busati amefikia ukomo akiamini kuwa kila mwenye ubongo uliotulia anao uwezo wa kuleta tafakuri na kuweka mwafaka kwenye bakuli.
Wasalaam,
Sunday, November 18, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment